NewsSWAHILI NEWS

Waziri Mkuu awapigia chapuo marais usimamizi wa sera za fedha nchini

Morogoro. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk Hussein Mwinyi kwa sera nzuri za fedha na uchumi ambazo zimekuwa msingi wa ukuaji wa sekta ya fedha hususan katika kuleta suluhisho la huduma za kifedha kwa wananchi nchni. 

Amesema kupitia sera hizo, tayari mabadiliko makubwa yameanza kuonekana mpaka kwenye ngazi za vitongoji na kusaidia kusogeza huduma kwa wananchi kupitia taasisi hizo za fedha.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo Jumanne, Julai 9, 2024 wakati akizindua tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Morogoro.

Amesema uzinduzi wa benki hiyo ni mpango wa kuendeleza dhamira ya Serikali ya kuleta maendeleo ya haraka kwa Watanzania kupitia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

“Ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa kila mwananchi,” amesema Majaliwa.

Amesema ufunguzi wa tawi hilo katika Mkoa wa Morogoro utakuwa ni miongoni mwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi katika kuwahudumia wananchi.

Amesema licha ya kutoa huduma za kibenki, uwepo wa benki hiyo unatoa fursa ya kuchangia upatikanaji wa ajira kwa vijana.

“Kwa upande mwingine, tawi hili ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi katika eneo hili kujenga msingi imara wa maendeleo endelevu na ustawi wa jamii yetu,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

“Hii ni pia ni ishara ya maendeleo na uwekezaji katika sekta ya kifedha na ni fursa muhimu kwa Wana-Morogoro kuongeza uwezo wenu wa kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zenu,” amesema.

Hivyo, amewataka wakazi wa mkoa huo  kutumia fursa ya uwepo wa benki hiyo kuchangamkia huduma zinazotolewa ikiwemo mikopo ambayo itawawezesha kupata fedha na kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Hamza Hassan Juma amesema benki hiyo itasaidia kuwaunganisha wakulima wa mpunga waliopo Morogoro na wale wa Zanzibar.

“Wakulima wa mpunga hapa Morogoro ni Wazanzibar, hivyo benki hii itasaidia kuwaunganisha na ndugu zao wengi waliopo Zanzibar,” amesema.

 Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ, Arafat Haji amesema uzinduzi wa benki hiyo mkoani Morogoro utasaidia kuimarisha biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar hasa ikizingatiwa Mkoa wa Morogoro ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo.

“Kwa sasa wateja wetu hawatakuwa na adha ya kusafiri kwenda Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar kufuata huduma za kibenki, hapa Morogoro ni kiunganishi kati ya Dar es Salaam na Dodoma,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!