NewsSWAHILI NEWS

Wanne kikaangoni madai ya kubomoa makaburi Tabora

Tabora. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema vijana wanne wanashikiliwa na jeshi hilo wakituhumiwa kuvunja makaburi 19.

Tukio la uvunjaji makaburi limetokea Julai 6, 2024 katika Mtaa wa Magubiko uliopo Kata ya Kiloleni, Manispaa ya Tabora.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Julai 10, 2024 Kamanda Abwao amesema baada ya msako wanawashikilia watuhumiwa wanne.

“Tulipata taatifa za uwapo wa tukio la makaburi kuvunjwa wilayani Tabora, takribani makaburi 19 yalivunjwa. Tulianza uchunguzi kwa haraka, tunawashikilia vijana wanne ambao walikutwa na vidhibiti, vikiwamo vyuma walivyotoa kwenye makaburi yale na vigae ambavyo havikupasuka wakati vinabadundiliwa,” amesema.

Kamanda Abwao amesema, “hatutaweza kutaja majina yao kwa kuwa bado tunawatafuta wenzao maana waliofanya tukio lile ni kundi kubwa, tukiwataja hawa tutaharibu uchunguzi wetu ambao tunaendelea nao.”

Amewaasa wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto katika malezi yanayotakiwa jambo ambalo litawaepusha na matendo maovu katika jamii.

Kamanda Abwao amesema vitendo vya kubomoa makaburi vinaonyesha maadili kushuka kwa kiasi kikubwa.

Katika hatua nyingine, amesema jeshi hilo linawashikilia ndugu wanne wa familia moja kwa kosa la kupanga njama za kumuozesha binti wa miaka 12.

“Tulipata taarifa za kuozeshwa mtoto wa miaka 12 wilayani Kaliua, tukaweka mtego, tukawakamata ndugu wanne ambao walikuwa wamemvisha shela mtoto huyo kwa ajili ya kumuozesha. Kwa sasa wako mikononi mwa polisi na taratibu zinaendelea kuhakikisha wanafikishwa mahakamani kwa kosa la ukatili wa kumuozesha mtoto mdogo kabla ya miaka 18,” amesema.

“Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuozesha watoto katika umri mdogo kama huo, mtoto wa miaka 12 anastahili kuwa shule akipata elimu kwa yoyote atakayehusika na matukio kama haya hatutasita kumkamata na kumchukulia hatua kali za kisheria,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!