NewsSWAHILI NEWS

Waliokatwa Soko la Kariakoo waandamana ofisi za CCM Lumumba

Dar es Salaam. Wafanyabiashara zaidi ya 800 wanaodai majina yao hayamo kwenye orodha ya watakaorejea katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wamekusanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kujiorodhesha, kisha wakaandamana kwenda ofisi za CCM Lumumba kulalamika.

Wafanyabiashara hao ni miongoni mwa waliohamishiwa kwenye masoko mbalimbali baada ya kuungua Soko la Kariakoo, kupisha ukarabati na ujenzi wa jingo jipya la ghorofa sita.

Soko la Karialoo liliungua Julai 2021 na kuteketeza mali karibu zote za wafanyabiashara.

Kutokana na hilo, Serikali ilitoa zaidi ya Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati na kujenga soko hilo dogo.

Tayari soko hilo limekamilika kwa matumizi na jana Jumatano, Julai 10, 2024 Shirika la Masoko Karikaoo lilitoa orodha ya wafanyabiashara watakaorejea sokoni na kati ya watu 1,662 waliokuwepo waliokidhi vigezo kurejea ni 891.

Mbali na majina hayo 891, shirika hilo liliwataka waliokuwa na madeni kuyalipa, la sivyo hawatoruhusiwa kurejea sokoni hapo.

Aidha, shirika lilitoa siku tatu kuanzia jana kwa wenye hoja au maoni kuhusu majina yao kutoonekana kwenye orodha ya uhakiki kufika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako maofisa wake watakuwa wanasikiliza madai yao.

Asubuhi ya leo Alhamisi, wafanyabiashara hao wamejitokeza kwa wingi, miongoni mwao ni Beatrice Mmari ambaye amesema idadi ya walioachwa ni wengi akihoji, wanataka watu hao waingie mtaani kuiba?

Sudi Jongo, anayejitambulisha kama mwenyekiti wa Soko la Wazi, amesema siku tatu walizopewa kujiandikisha tena hazitoshi na pia zimekuwa usumbufu kwao.

Jongo amesema katika kuhakikiwa hii ni mara ya tatu kiasi kwamba wao viongozi wamekuwa hawaeleweki kila wanapowatangazia wafanyabiashara kutakiwa kuhakikiwa.

“Mimi niombe hii kazi ifanywe wiki moja, siku tatu hazitoshi, maana walioachwa ni wengi, hii itasaidia kila mwenye haki kurudi sokoni,” amesema Jongo.

Mariam Zuberi aliyefanya shughuli zake miaka 15 sokoni hapo, amesema majina mengi yaliyotoka watu hawayajui na kutaka suala hilo liangaliwe upya hata kwa kuwatumia viongozi wao, kwa kuwa ndio wanawajua.

Baadaye wafanyabiashara hao wamehamasishana kwenda Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), zilizopo Lumumba kupeleka kilio chao.

Kutoka Mnazi Mmoja kwenda ofisini hapo ni kama mita 400 na katika ofisi hizo, watumishi wa CCM wamesikika wakiwatuliza wasiendelee kupiga kelele.

Endelea kufuatilia kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!