NewsSWAHILI NEWS

Wakazi Dar kuandikishwa Daftari Ia Kudumu Ia Wapiga Kura Machi, 2025

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema kazi ya uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu la Wapiga Kura itafikia tamati Aprili mwakani, huku wakazi wa Dar es Salaam wakianza kuandikishwa Machi, mwakani.

Uandikishaji huo utazinduliwa Julai 20, 2024 mkoani Kigoma na unatarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Awali, ilipangwa kuanza Julai Mosi, kabla ya INEC kutangaza mabadiliko, huku kukiwa na tetesi kwamba uandikishaji huo umesogezwa kutokana na uhaba wa vifaa vya BVR.

Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima ameiambia Mwananchi Digital leo Jumapili Julai 7, 2024 kwamba vyama vya siasa ndivyo viliomba usogezwe kwa siku 20 na Tume ikaridhia.

Amesema, uandikishaji huo utakapozinduliwa,  siku hiyohiyo uboreshaji utaanza kwenye mkoa huo wa Kigoma, Katavi na Tabora, kisha wataendelea na mikoa ya Kagera na Geita.

Kailima amesema awamu ya tatu itakuwa kwenye mikoa ya Shinyanga na Mwanza na ya nne ni Mikoa ya ya Simiyu na Mara na baadhi ya Halmashauri za Mkoa wa Manyara.

“Tutakwenda hivyo hadi tutakapomaliza, mwanzo tulipanga tufikie tamati Machi mwakani, lakini sasa tutafikia tamati Aprili na Dar es Salaam imepangwa peke yake kutokana na changamoto zake na uandikishaji wake utakuwa ni Machi mwakani,” amesema Kailima.

Japo awali kulikuwa na taarifa kwamba uboreshwaji umesogezwa mbele kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya BVR, Kailima amesema sio kweli akivitaja vyama vya siasa kuhusika.

“Tusingeweza kwenda kuendesha mafunzo Kigoma kama tusingekuwa na vifaa, tungeahirisha tangu mwanzo, sisi (Tume) tulikuwa tupo tayari lakini kuna mambo matatu yalisababisha mchakato usogezwe mbele,” amesema.

Ameyataja mambo hayo kuwa la kwanza ni vyama vya siasa ndivyo zilivyoomba usogezwe mbele vikitoa sababu mbili.

“Walisema wanataka wapate fursa ya kutafuta mawakala wa uandikishaji, kwani kwa mujibu wa sheria vina haki hiyo, vilisema nchi ni kubwa hivyo tuwape muda wa kutafuta mawakala.

“Pia tulipokutana nao Juni 7, wakaomba wapate fursa ya kuwahabarisha wanachama wao, wakatuomba tusogeze mbele kwa siku 20,” amesema.

Mbali na vyama vya siasa, Kailima amesema pia asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura nazo ziliomba zipewe muda ili zitafute fedha.

“Hizi asasi huwa zinatoa elimu kwa kutumia ‘fund’ (Ufadhili) zao lakini kwa mujibu wa sheria wanatakiwa waseme vyanzo vyao vya mapato.

“Kilichotushtua zaidi tulipokuwa Kigoma hata baadhi ya vyama kumbe tulipovipa ratiba tukiwa Dar es Salaam, havikuzitoa kwenye vyama vyao mkoani humo, Tume ikaona kuna haja ya kusogeza mbele ili huko mbele vyama visije kusema viliomba muda vikanyimwa,” amesema Kailima.

Kwa mujibu wa Kailima, hivi sasa Tume imewasiliana na vyama na asasi hizo na vyote vimeeleza kuwa tayari, na kazi hiyo sasa itaanza rasmi Julai 20, 2024 kama ilivyopangwa.

Ingawa hivi karibuni, Mwananchi ilidokezwa kuwapo kwa changamoto ya vifaa iliyosababisha mkwamo wa kazi hiyo kufanyika, Kailima amesema si kweli, INEC wamezingatia maoni ya wadau waliyoyatoa wakati wa mikutano iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na Kigoma.

Uandikishaji utakavyokuwa

Kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, INEC inasema wapigakura wapya 5,586, 433 wanatarajiwa kuandikishwa sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari, idadi hiyo ni baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.

Wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na watu 594,494 wataondolewa kutokaa na kukosa sifa ikiwamo kufariki au kuukana uraia na baada ya uboreshaji matarajio ni kufikisha wapiga kura 34,746,638 na zaidi.

Uandikishaji huo utafanyika katika vituo 40,126, ambavyo kati yake, 39,709 viko Bara na 417 vipo Zanzibar huku kwenye magereza kutakuwa na vituo 130 upande wa Bara na 10 Zanzibar.

Kwa mujibu wa INEC, mfumo wa uandikishwaji (VRS) umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi matumizi na kwa mujibu wa INEC, tayari BVR 6,000 zinazotumia vishikwambi ili kuchukua taarifa zikiwamo picha, saini na alama za vidole zimekwishanunuliwa

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!