NewsSWAHILI NEWS

Wajawazito wenye dharura kupata usafiri bila malipo

Kibaha. Vifo vya wanawake vinavyotokana na changamoto za uzazi vimepungua kutoka 37 mwaka 2023 hadi kufikia 12 mwaka 2024 mkoani Pwani.

Hatua hiyo imefikiwa kutokana na utekelezaji mfumo wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito wenye matatizo baada ya kujifungua kutoka kituo kimoja kwenda kingine kupata huduma kulingana na changamoto wanazopata.

Mfumo huo wenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga maarufu M -Mama kitaifa ulizinduliwa Juni 4, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye viwanja vya Chinangali mkoani Dodoma.

Uzinduzi wa mfumo huo ni mwendelezo wa maboresho ya mpango huo ulioanzia Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Sengerema kama mradi.

Akizungumza leo Julai 10, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waelimishaji afya ngazi ya jamii juu ya mfumo huo yanayofanyika Kibaha, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, David Vuo ametaja manufaa mengine yaliyopatikana kwa kipindi cha mwaka mmoja kupitia utaratibu huo ni kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 358 hadi kufikia 179 mwaka huu wa 2024.

“Baada ya mafunzo haya mfumo huu utapanuka zaidi na sasa wajawazito wenye dharura na watoto wachanga   watakuwa wanafuatwa kutoka nyumbani hadi kwenye eneo la kutolea huduma au kituo cha afya. Watafuatwa na madereva ambao wamesajiliwa,” amesema.

Amesema jukumu la mjamzito ili kufikiwa na huduma hiyo ya usafiri litakuwa kupiga simu ya bure namba 115.

Amesema watoa huduma ya usafiri watamfikia popote alipo na kumsafirisha hadi kituo cha afya.

Vuo amesema ili kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ufanisi umewekewa utaratibu wa ukusanyaji wa fedha kupitia mfuko wa pamoja.

Amesema fedha zinapatikana kupitia mapato ya ndani na mpaka sasa wamekusanya Sh19.067 milioni kutoka halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani.

Mratibu wa M-MAMA    Mkoa wa Pwani, Alfredy Ngowi amesema hadi kufikia Juni 9, 2024 wenye rufaa za dharura 2,207 wamesafirishwa kupitia mfumo huo.

Amesema safari ziliratibiwa na kubeba wagonjwa 2,084 sawa na asilimia 93.06 na kupitia madereva ngazi ya jamii ni 14 sawa na asilimia 6.38, huku safari ambazo hazikufuata utaratibu ni 16 sawa na asilimia moja.

Mratibu wa M- Mama katika Halmashauri ya Chalinze, Gabriela Mtwale amesema changamoto ya wajawazito ni kubwa na kwamba wengi wamekuwa wakikumbwa na dharura na kutakiwa kufikishwa kituo cha huduma  lakini hushindwa kufanya hivyo kutokana na uwezo wa kifedha.

Hata hivyo, kupitia mfumo huo amesema ni mkombozi kwao.

Amesema utekelezaji wa kuwafuata wajawazito nyumbani utaokoa maisha ya wengi kwa kuwa jukumu lao kubwa ni kupiga simu pekee na kufikiwa nyumbani bila kulazimika kufanya malipo yoyote.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!