NewsSWAHILI NEWS

Wahamiaji wengine wanaswa mashambani Arusha

Arusha. Wakati wimbi la wahamiaji haramu likiendelea kutikisa, wengine watatu raia wa Ethiopia walioingia nchini kwa njia za panya wamekamatwa wakiwa wamejificha kwenye mashamba ya mahindi mkoani hapa.

Idadi hiyo inafikisha jumla ya wahamiaji haramu waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha kufikia 31 baada ya  juzi kukamatwa wengine 28.

Wahamiaji hao walikamatwa usiku wa kuamkia Julai 6, 2024 baada ya lori la mizigo walilokuwa wamepakiwa kupata ajali ya kugongana na lori lingine, hivyo kushuka na kujificha porini.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Julai 7,2024 kwa simu, Naibu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Dickson Mwandikile amesema wahamiaji hao watatu walikuwa na wenzao 28 waliokamatwa juzi ila wao wakajificha.

“Jana wameongezeka wahamiaji wengine watatu, walipatikana eneo lilelile wakiwa wamejificha kwenye mashamba ya mahindi kwa hiyo doria zinaendelea pale kuwasaka, tulipata taarifa kutoka kwa mkazi mmoja wa eneo hilo, inaonekana kuna watu wamewahifadhi,” amesema Mwandikile.

Amesema kwa sasa wanaendelea kuwahoji na kuchukua maelezo yao kwa kutumia wakalimani na baadhi ambao bado hawajaanza kuwahoji, wanaumwa na wakikamilisha watafikishwa mahakamani.

Kuhusu mikakati ya Idara hiyo, amesema wanaendelea kuimarisha doria hasa katika maeneo ya mipakani pamoja na kuelimisha jamii ili kuepukana na vitendo vya kuhifadhi wahamiaji haramu, kwa kuwa ni kosa kisheria na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Moshi, iliamuru kutaifishwa magari mawili yaliyokamatwa yakiwasafirisha wahamiaji haramu 12 raia wa Ethiopia, likiwamo linalodaiwa kumilikiwa na mbunge.

Magari yaliyotaifishwa kwa amri ya mahakama hiyo ni Toyota Land Cruiser namba T 888 BTY ambalo jina la mmiliki linasomeka kwenye nyaraka za umiliki, linafanana na la mbunge mmoja nchini Tanzania. Gari lingine lililotaifishwa ni lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KCV 571Y la nchi jirani ambalo lilikamatwa katika mji wa Tarakea wilayani Rombo, Juni 19, 2024 likiwa na wahamiaji haramu watano.

Pia, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alipokuwa akizungumza bungeni katika Bunge la Bajeti lililohitimishwa Juni 28, mwaka huu, alisema jumla ya wageni 1,223 wamezuiwa kuingia nchini kwa kutumia Mfumo wa kielektroniki wa mipaka (e-border) kwa kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Mei 2024.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!