NewsSWAHILI NEWS

Wadau watahadharisha njaa Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Nchi  za Afrika Mashariki zimetahadharishwa kufanya juhudi za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mvua, unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, ili zisiingie kwenye baa la njaa.

Wadau sekta ya nishati safi wamesema kupungua kwa mvua, kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi juhudi za haraka zisipo chukuliwa nchi za Afrika Mashariki zaweza kuingia kwenye baa la njaa.

Juhudi hizo zimetajwa kuwa ni pamoja na kutafuta suluhisho kwa kuwaunganisha wakulima na mifumo ya umwagiliaji inayotumia nishati safi, ili waendelee kuzalisha mazao bila athari za mabadiliko hayo.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayosababisha wakulima wengi kushindwa kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji  imetajwa kuwa ni kodi kubwa ya vifaa hivyo bandarini, hali inayopandisha bei ya vifaa sokoni zikiwemo pampu.

Hayo yamezungumzwa leo Jumatatu, Julai 8, 2024 na wadau wa nishati safi kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda katika siku ya kwanza ya majadiliano yenye lengo la kuendeleza suluhisho za nishati mbadala Afrika Mashariki.

Meneja wa ushirikiano na biashara na Serikali kutoka Sim Solar, Hobokela Mwakabango amesema lazima juhudi za pamoja miongoni mwa wadau na Serikali zichukuliwe, ili wakulima waendelee kuzalisha chakula cha kutosha.

“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi tunaendelea kupoteza mvua kila mwaka, bila kuifundisha jamii yetu mifumo ya umwagiliaji, tukisubiria mvua bila kutafuta vyanzo vya maji chini ya ardhi kuvuta maji chini hatutakuwa salama, tutakumbwa na baa la njaa,” amesema.

Mwakabango amesema kuna haja ya kila nchi kuhakikisha inafikia malengo kwa kusaidia jamii isipotee kwa kuwa na kilimo stahimilivu.

Amesema nchi zitafikia malengo hayo kwa kuondoa kodi zisizo na ulazima, hasa katika uingizwaji wa mashine mbalimbali za masuala ya nishati mbadala.

“Wizara ya Fedha ifikirie kupunguza kodi ya vifaa hivi kuingia nchini, unatoa bandarini kwa fedha nyingi tofauti na nchi nyingine eneo hilo hawalipii kodi kabisa tofauti na sisi.

“Sheria ya kodi inasema kila kifaa kinatakiwa kilipiwe kodi na kwa bahati mbaya vifaa hivi huingia tofauti, hatuwezi kufikia malengo kama Serikali isipopunguza gharama za nishati hizi mbadala,” amesema Mwakabango.

Ametaja miongoni mwa mikakati ambayo imekuwa ikifanywa na wadau nchini ni pamoja na kutafuta wafadhili, ili pampu yenye thamani ya Sh1 milioni, mkulima auziwe kwa Sh700,000 ili kuwafanya wakulima wengine wajifunze kwa wale waliopata ufadhili huo na kuna umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.

Hata hivyo, amesema tofauti na miaka sita iliyopita, wakulima wanaanza kuelewa teknolojia ya nishati mbadala na wameanza kutumia.

“Zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni wakulima na hao wote wanategemea kilimo kuendesha maisha yao, mpaka sasa ni asilimia 5 pekee wanatumia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji,” amesema Mwakabango.

Naye Kamishna Msaidizi wa Nishati mbadala kutoka Wizara ya Nishati, Imani Mruma amesema kuwa matumizi ya nishati hiyo nchini bado madogo, hivyo amewataka wadau kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo kuchochea matumizi ya nishati hiyo.

Mratibu wa programu kutoka Kenya Climate Innovation center, Saumu Ismail amesema ni lazima kila nchi kuhakikisha inatafuta ufumbuzi wa namna ya kushirikisha wakulima walioko pembezoni, ili kuachana na kilimo cha kutegemea mvua.

Ofisa Programu wa Environment Program Advancing Climate Change Solution (ACCS), Dk Robert Ddamulira amesema mkutano huo umewaleta pamoja wadau muhimu wanaojitolea kuendeleza matumizi ya nishati mbadala Afrika Mashariki kwenye sekta ya kilimo.

Amesema mkutano huo wenye kaulimbiu “Kufadhili mfumo wa wajasiriamali wa Agrisolar Afrika Mashariki,” unalenga kushiriki mbinu na mifumo ya ufadhili bunifu ndani ya mfumo wa kilimo, kubaini fursa za ushirikiano, kupata msaada kutoka kwa wafadhili na kuunda mazingira ya sera na udhibiti yanayounga mkono ufadhili wa nishati mbadala.

“Malengo ni kushirikiana mbinu zilizofanikiwa, kubaini fursa za ushirikiano, kupata msaada kutoka kwa wafadhili wa kibiashara kuunda mazingira ya sera na udhibiti yenye msaada, matokeo muhimu, uandaaji wa mbinu za ufadhili bunifu,” amesema.

Dk Ddamulira ametaja malengo mengine kuwa ni kubaini miradi ya ushirikiano, ahadi kutoka kwa wafadhili wa kibiashara na mapendekezo ya sera na udhibiti.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!