NewsSWAHILI NEWS

Vijiji ndani ya Ruaha vyabakia vitano kutoka 33

Iringa/Mbarali. Tangazo la Serikali (GN) namba 175, limepunguza idadi ya vijiji vilivyokuwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutoka 27 na hadi vitano, ambavyo mbali na kuwa ndani ya hifadhi, wananchi wanaendelea na maisha kama kawaida.

Wananchi katika vijiji hivyo vitano vya Madundasi, Msanga, Luhanga, Iyala na Kilambo wanaendelea na maisha yao wakijishughulisha na kilimo, ufugaji na biashara za huduma za kijamii kama shule na zahanati zikiendelea kama kawaida.

Kauli hiyo imetolewa jana kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Meing’atak na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Kanali Denis Mwila, wakati wakizungumza na wanahabari za uhifadhi, utalii na mazingira waliotembelea eneo hilo mapema wiki hii.

Hii ni baada ya waandishi hao wa habari kutaka kufahamu ukweli wa taarifa zilizosambazwa katika mtandao mmoja wa kimataifa kuwa wananchi katika vijiji hivyo wamehamishwa kwa nguvu ili kupisha Hifadhi.

Kauli za viongozi hao wawili ziliungwa mkono na baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo, wakiwamo wa Kijiji cha Madundasi, waliosema hakuna aliyehamishwa kwa nguvu na wanaendelea na maisha yao licha ya kujulishwa wako ndani ya hifadhi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Madundasi, Seni Nereshi Nimka amesema japokuwa wameambiwa wako ndani ya hifadhi, lakini mambo yote ya shughuli za kibinadamu yanaendelea kama kawaida yakiwamo ya kilimo cha mpunga.

“Kama mnavyoona tuna mazao ya mpunga tunaendesha kama kawaida na sisi hapa hatujawahi kuambiwa lolote japokuwa tuliambiwa tuko ndani ya hifadhi, lakini bado mambo yote ya kuhusu kuhamishwa hayajafanyika.”

“Hawajawahi kufika hapa kutathmini kwa hiyo tuko kama kawaida na shule vilevile ziko kama kawaida. Shule za msingi, shule za awali ziko kama kawaida. Zahanati ipo. Ila tunaomba Serikali ituongezee barabara,” ameeleza Nimka.

Mkazi wa Kijiji hicho, Judith Tawete amesema mwaka jana baada ya kufika Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana aliwaambia waendelee na maisha yao kama kawaida.

Alichokisema Mkuu wa Hifadhi

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, mkuu wa Hifadhi ya Ruaha, Godwell Meing’atak, amesema GN namba 175 ya Oktoba mwaka jana imepunguza ukubwa wa hifadhi kutoka kilomita za mraba 20,226 hadi kilomita 19, 822.

Amesema kutagazwa kwa GN hiyo mpya kulitokana na maamuzi ya kamati ya mawaziri wa kisekta ambao waliona kilomita za mraba 404 za vijiji 22 kati ya 27 waachiwe wananchi waendelee na shughuli zao.

Hata hivyo, amesema vipo vijiji vitano kati ya 27 vilivyokuwa ndani ya hifadhi kulingana na GN namba 28 ya 2008, vimeonekana kuna umuhimu mkubwa viendelee kubaki kulinda ikolojia ya hifadhi.

 “Lakini kwa sasa hizi maelekezo tuliyopewa sisi ni kuwa hao wananchi waendelee na shughuli zao japokuwa wapo ndani ya hifadhi. Pale hatutekelezi sheria za hifadhi kwa sababu wananchi wanaishi, wanalima, wanafuga mifugo yao.”

“Wapo wanafunzi wanaendelea shuleni, Zahanati ipo na watu wanaendelea na maisha yao kama kawaida hadi hapo Serikali ikifanya maamuzi ndio tutatekeleza sheria za hifadhi. Lakini kwa sasa hakuna mtu ameondolewa hata mmoja.”

Meing’atak amefafanua kuwa mfumo wa Ikolojia ya Usangu una maeneo makubwa mawili, ambayo ni muhimu kwa mto Ruaha ikiwamo Mbuga ya magharibi na Mbuga ya mashariki na vijiji hivyo vitano vipo mbuga ya magharibi.

“Mbuga hiyo ambayo ina vijiji vitano ni upande wa magharibi ambapo maji yakijaa huenda taratibu kutiririka kwenda mbuga ya mashariki ambayo ni kwenye hifadhi ya Ihefu ambako mto mkuu Ruaha unaanzia.”

“Kwa hiyo wakati mwingine ukikosa muunganiko mzuri unaweza kusema hawa mbona hawapo eneo Oevu au mbali sana na chanzo cha mto Ruaha mkuu, lakini ukweli ni kwamba mto Ruaha unapata maji yake kutoka mbuga hii ya magharibi.”

Mkuu wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Kanali Mwila amesema wakati wa ukoloni mwaka 1910, Mbarali yote ilikuwa ni sehemu ya Hifadhi lakini watu wameendelea kuongezeka na kufanya hifadhi ikaendelea kupungua.

“Mwaka 2008 ikapitishwa GN (namba 28) ya hifadhi ya kwanza. Lakini tumekwenda watu wameendelea kuvamia, kupanua mashamba kulima na kufanya kila kitu na mwaka jana imetoka GN namba 175 yote hii ni kulinda hifadhi,”amesema.

“Hifadhi hii ni muhimu sana kwa sababu mabwawa ya Mtera, Kidatu yote asili ya maji yao ni mto Ruaha kwenye hifadhi ya Ihefu. Lakini asilimia 15 ya maji ambayo yatatumika kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere yanatoka hapa Ihefu.”

“Sasa nini kimetokea, kutokana na hali nzuri, wafugaji wakubwa na wadogo  wamekuwa wakileta ng’ombe huku Ihefu, pia wakulima wengi wamekuwa wakilima bonde la Ihefu,”amesema.

“Wakulima hawa wana nguvu ya fedha kwa sababu ninavyowaambia, kilimo cha hapa sio cha kubahatisha, kwanza niwahakikishie hakuna mtu anayelima kwa mikono hapa au ng’ombe,” ameeleza na kuongeza.

“Tunapoongea hapa tuna Power Tiller karibu 4,000 na matrekta zaidi ya 3,000. Kwa hiyo watu wanaolima hapa wanalima kweli na mwaka jana tu tulipata tani za mpunga 620,000. Ni eneo lenye ardhi yenye rutuba kwelikweli.”

“Hivyo watu wenye nguvu za kifedha kuja kulima hapa. Sasa katika kulima huko ikagundulika tunahitaji maji, tunahitaji hifadhi kwa hiyo kupitia hii GN 175 ambayo sasa hivyo vijiji vitano vimeonekana vibaki hifadhini,”amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesema lakini kumetokea watu wenye nguvu za kifedha za kulima na kufuga wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutaka kuonyesha kuwa Mbarali si salama, watu wamehamishwa kwa nguvu, jambo ambalo si kweli.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!