NewsSWAHILI NEWS

VIDEO: Wananchi 600 wanavyosotea hatimiliki kwa miaka sita-1

Dar es Salaam. Ni miaka sita ya kuhangaika kutafuta hatimiliki bila mafanikio kwa wananchi zaidi ya 600 katika vijiji vitatu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, licha ya kulipa Sh20 milioni kwa ajili ya huduma hiyo.

Vijiji hivyo ni Marogoro, Yavayava na Mfuru Mwambao vilivyopo Kata ya Vianzi, ambako kutokana na maeneo kutoendelezwa yamegeuka kuwa pori.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini wananchi hao walinunua viwanja zaidi ya 9,000 katika vijiji hivyo vitatu na kulipia kupata hatimiliki tangu mwaka 2018.


VIDEO: Wananchi 600 wanavyosotea hatimiliki kwa miaka sita-1

Khadija Ntenje ni miongoni mwa walionunua viwanja hivyo, ambaye katika mazungumzo na Mwananchi anasema kutokana na kuchelewa kupata hatimiliki, wana hofu huenda viwanja vyao vikauzwa mara mbili.

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Said Salehe anasema ucheleweshwaji huo umetokana na sababu nyingi, ikiwamo kutotafsiriwa vyema sheria inayohusu urasimishaji ardhi.

“Viwanja katika vijiji hivi vilianza rasmi urasimishwaji mwaka 2018, lakini baada ya wataalamu kufanya ukaguzi ikabainika sheria inasema eneo lile si la urasimishaji, bali ni la kupanga upya kwa sababu hakuna uendelezaji wowote ulifanyika,” anasema.

“Wananchi walielekezwa wawasilishe maombi mapya, ili kufanya upangaji, wakawasilisha na wakachagua kamati kusimamia zoezi hilo,” anasema Salehe.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Said Salehe akifafanua jambo katika mahojiano na mwandishi wa makala hii. Picha na Geofrey Mlwilo

Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007, kifungu cha 25 inaeleza urasimishaji unafanywa katika maeneo ambayo tayari yana makazi.

“Sehemu hii inashughulikia mchakato wa kuhalalisha makazi yasiyo rasmi ambayo ni pamoja na kuboresha miundombinu na kutoa hatimiliki za ardhi kwa wakazi, ili kuboresha hali zao za maisha,” inaeleza sheria hiyo.

Katibu wa kamati ya walionunua viwanja hivyo, Kamona Twahiri, akizungumza na Mwananchi anakiri kuwepo ucheleweshwaji huo, akieleza wamefikisha malalamiko kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.

“Kimsingi zoezi hili lilianza tangu 2018, tulinunua viwanja kule kijijini (Yavayava, Marogoro na Mfuru Mwambao) na baada ya kuhofia huenda watu watauza mara mbili eneo moja, ndipo tukaona bora tupatiwe hati na Serikali ili eneo liwe salama,” anasema.

Kamona anasema walionunua viwanja eneo hilo walipendekeza halmashauri iwarasimishie, akieleza waliiandikia barua ikakubali kwa sharti kwamba walipe fedha. Anasema kwa wastani kila mmoja alilipa Sh150,000. Kwa mujibu wa Kamona, walitoa fedha na wataalamu walikwenda kukagua, lakini baada ya hapo kumekuwa na mkwamo. “Baada ya hapo tukaanza kuona delay (ucheleweshaji) na hasa ni kwa sababu ya kubadilishwa wakuu wa idara ya ardhi, kila aliyekuja alikuwa na vipaumbele vyake. Kusuasua huko kumesababisha kufika mpaka leo bila kupewa hati miliki tangu mwaka 2018,” anasema Kamona:

“Baada ya kufika kwa waziri, wizara imeshachukua hatua, ilielekeza tukae kikao, tulifanya hivyo na wataalamu tulijadili kwa kina. Tulikubaliana tuanze mikutano na tulishatoa ratiba, lakini tulishindwa kuifanya kwa sababu ya changamoto ya mvua,” anasema Kamona, ambaye anaonyesha matumaini ya kupata hati.

Mwananchi ilifanya mazungumzo na wananchi hao kati ya Aprili na Mei, 2024 ambao ulikuwa msimu wa mvua.

Hata hivyo, anasema: “Tulifanikiwa kukaa kikao Mei baada ya mvua kukata. Tulikaa vijiji vyote vitatu chini ya timu ya wataalamu wa ardhi ya mkoa kwa ajili ya kusikiliza malalamiko yetu. Alituambia ripoti ya kikao kile imeenda kwa waziri.”

Waziri Silaa alipotafutwa na Mwananchi kwa simu mara kadhaa hakupokea.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Geophrey Pinda alipotafutwa alisema suala kama lipo mezani kwa waziri litashughulikiwa.

“Kama watu hao waliwasilisha mezani kwa waziri litafanyiwa kazi, ila kama bado wapatie namba yangu (ya simu) tuone limekwama wapi,” alisema Pinda.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marogoro, Abdallah Lwinde (kulia) akizungumza na mwandishi wa makala hii (kushoto) katika eneo ambalo viwanja vyake kwa miaka sita vinasubiria hatimilki. Picha na Geofrey Mlwilo

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marogoro, ambaye pia ni diwani wa Vianzi, Abdallah Lwinde anasema kuingiliana kwa ratiba ni miongoni mwa chanzo cha kufanya mchakato huo uchukue muda mrefu.

“Kilichokwamisha tangu mwaka 2018 ni kuwa wataalamu walibaini pale hapahitaji urasimishaji bali upangaji, ikabidi zoezi lianze, lakini bahati mbaya mwaka 2019 likasimama kwa sababu ya uchaguzi wa Serikali ya mtaa kwa sababu Ofisi ya Mkurugenzi inahusika katika kusimamia na kuratibu uchaguzi huo na mwaka 2020 tukaingia katika Uchaguzi Mkuu, hapo pia zoezi likasimama,” anasema.

“Mwaka 2021 mchakato ukaanza tena, walikuja kupima lakini ikashindikana kutokana na namna eneo lilivyo, ikahitajika ushirikishaji wa wananchi. Tukaanza tena kutoa elimu, tukakaa vikao kama saba kupitia kamati yao.

“Hata hivyo, kamati ilituma barua wizarani kulalamika kuwa zoezi linachelewa, ndipo waziri aliagiza timu yake mwaka huu (2024) kushughulikia, lakini kutokana na miundombinu walishindwa kufika eneo la tukio na tukakubaliana tusubiri miundombinu ipitike,” anasema Lwinde.

Salehe, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Mkuranga anasema kuchelewa kutolewa hatimiliki kunatokana na sababu kuu tatu.

Anazitaja kuwa ni: “Kamati iliyochaguliwa ilikuwa haihusishi vijiji vyote vitatu, hakukuwa na elimu ya kutosha iliyotolewa kwa wananchi kujua umuhimu wa upangaji, pia kulikuwa na malalamiko kuwa ardhi ya kijiji ilitolewa na kupangwa bila kuwa na ridhaa ya wananchi.

“Pia kulikuwa na barua ya zuio kutoka wizarani, kwa nia njema kabisa iliona kuwa zoezi hili badala ya kufanyika kienyeji kwa kujipangia bei wenyewe ihusishe halmashauri, kwa hiyo Serikali ikasitisha zoezi nchi nzima na kutaka halmashauri iyasimamie,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marogoro, Abdallah Lwinde akimuonyesha mwandishi wa makala hii viwanja vilivyonunuliwa ambavyo bado hatimiliki haijatolewa. Picha na Mpiga Picha Wetu

Ili kukwamua upangaji wa eneo hilo, Salehe anasema kwa sasa suala limefika Wizara ya Ardhi na wameamua kuanza upya vikao na wananchi.

“Kwa hiyo pamoja na changamoto hizo tukaona tuanze upya vikao na wananchi, tukishamaliza tuingie kwenye utambuzi wa maeneo kwenye kila kipande cha ardhi cha kila mwananchi na baada ya hapo tutaingia hatua ya kuweka bikoni,” anasema.

“Wakati tukianza utekelezaji ndipo changamoto ya kukatika barabara ikatokea, kukawa hakupitiki, tunasubiri hali ya barabara ikae vizuri tuendelee na mchakato,” anasema Salehe.

Kwa sasa (Julai, 2024) anasema wameanza upya mchakato wa kutoa elimu kwa wananchi na kusikiliza malalamiko.

“Kwa sasa tumeanza tena mchakato kwa kutoa elimu, kusikiliza malalamiko na tayari timu ya ardhi kutoka mkoani imeandika ripoti, ili tuendelee na hatua ya pili ya utambuzi,” amesema Salehe.

Akizungumzia athari za kuchelewa umilikishwaji ardhi, Ofisa Mipango Miji na Mhadhiri wa Chuo cha Mipango, Gerald Temu anasema kutomilikishwa ardhi kwa watu ni moja kati ya sababu za migogoro ya ardhi, hasa katika Mkoa wa Pwani.

“Migogoro ya ardhi inasababishwa na ardhi kutopimwa na kumilikishwa rasmi, sehemu kama Pwani- Mkuranga, ikiwamo ardhi ya hapo imepata umaarufu kwa sababu ya uwekezaji unaofanyika, na kuwa karibu na Dar es Salaam kunaifanya kuwa na thamani kubwa, hivyo kuchelewa kutolewa kwa hati kunaweza kuwa chanzo cha migogoro,” anasema Temu.

Itaendelea kesho, tukiangazia kutozingatiwa tafiti za ardhi kunavyochangia migogoro.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!