NewsSWAHILI NEWS

Usiyopaswa kuyafanya ndani ya treni ya SGR

Dar es Salaam. Kama umezoea kuamua aina ya begi la kusafiria, kubeba kuku, mbwa na wanyama wengine unapokwenda kupanda basi, hali haiko hivyo kwenye usafiri wa treni ya umeme (SGR).

Kwa taarifa yako, begi la shangazi kaja, mizigo inayozidi kilo 30 na wanyama wakiwemo wa kufugwa si sehemu ya vitu unavyopaswa kuwa navyo unapotaka kwenda kupanda treni hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kila kinachofanyika kinalenga kulinda usalama wa abiria, kadhalika viwango vya ubora wa treni na huduma kwa ujumla.

Kwa sasa treni hiyo tangu ilipoanza kutoa huduma wiki tatu zilizopita, inafanya safari za kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kwamba kufikia Julai 25, mwaka huu safari zitaongezwa hadi Dodoma.

Sio kama wengi walivyozoea, unapotaka kupanda treni hiyo, yapo mambo ya msingi unapaswa kuzingatia.

Kwa mujibu wa TRC, abiria wanashauriwa kukata tiketi zao kupitia tovuti ya shirika hilo au katika madirisha yaliyopo vituoni angalau saa mbili kabla ya kuondoka ili kuepuka msongamano.

Abiria wakiwa ndani ya treni ya SGR inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Kufika mapema katika stesheni ni jambo lingine linaloshauriwa na TRC kufanywa na abiria, ikisema angalau abiria afike kwenye eneo hilo saa moja kabla ya kuondoka.

Mifuko ya plastiki, silaha, chakula, vinywaji, ndoo na mapipa si sehemu ya vitu anavyopaswa kuwa navyo abiria anayesafiri kwa treni hiyo.

Kama una mnyama wako awe wa kufugwa au mwingine haruhusiwi katika treni ya umeme.

Wale wenzetu wa mabegi ya ‘shangazi kaja’ treni hiyo haijawafikia, pia si ruhusa kupanda ukiwa na aina hiyo ya mfuko.

Mizigo yenye uzito uliopitiliza pia si ruhusa katika treni hizo, abiria wa daraja la biashara anapaswa kuwa na mzigo usiozidi kilo 30, huku daraja la uchumi usizidi kilo 29.

TRC ilianza huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro Juni 14, mwaka huu, huku Julai 25 safari zikitarajiwa kuongezeka hadi Dodoma.

Kwa mujibu wa TRC, miongozo hiyo inalenga kuhakikisha viwango vya usalama na uendeshaji vinazingatiwa.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!