NewsSWAHILI NEWS

Upelelezi kesi ya kusafirisha kilo 332 za dawa za kulevya bado

Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusafirisha kilo 332 za Heroine na Methamphetamine inayomkabili, mvuvi wa samaki Ally Ally (28) na wenzake wanane.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Julai 8, 2024 kuwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 10561/2024, ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Kasala ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, ambapo amedai uchunguzi wa shauri hilo unaendelea, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, Hakimu Magutu ameahirisha kesi hadi Julai 22, 2024, itakapotajwa na washtakiwa wapo rumande kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana kwa mujibu wa sheria.  Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa mahabusu.

Mbali na Ally, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Bilal Hafidhi (31) ambaye ni mfanyabiashara, Mohamed Khamis (47) mvuvi wa samaki na muuza magari, Idrisa Mbona (33).

Wengine ni Rashid Rashid (24) mkazi wa Ubungo Maji, Shabega Shabega (24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.

Pia, yupo Dunia Mkambilah (52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke, mfanyabiashara Mussa Husein (35) mkazi wa Mwambani na Hamis Omary (25).

Katika kesi hiyo washtakiwa wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hotel ya White Sands, iliyopo Wilaya ya Ilala, walikutwa wakisafirisha kilo 100.83 za dawa aina ya Methamphetamine.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za Heroine, kinyume cha sheria.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!