NewsSWAHILI NEWS

Tozo ya Sh500 kila siku yaliza madereva bajaji Moshi

Moshi. Baadhi ya madereva wa bajaji katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kutozwa Sh500 kila siku, bila kupewa risiti ya malipo halali, huku wakiwa hawajui matumizi ya fedha hizo.

Mwananchi Digital imepita katika njia ya KCMC na kushuhudia vijana wawili wakiwa eneo la Ushirika na wanasimamisha kila bajaji inayopita na kutoza Sh500, huku zile zinazogoma kusimama wakizikimbiza, kisha kuning’inia pembeni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madereva hao wamedai fedha hizo wamekuwa wakitozwa kwa nguvu na wanapokataa hukamatwa na bajaji zao kuzuiwa kwa siku nzima.

Wakizungumza wanaokusanya fedha hizo eneo la geti la Ushirika, wamesema fedha hizo ni makubaliano ya madereva bajaji kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa bajaji hizo na kiasi wanachokusanya wanajilipa kama posho.

Akizungumzia malalamiko hayo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyello amesema suala la madereva wa bajaji kutozwa Sh500, haliwahusu na kumtaka mwandishi wa habari awatafute viongozi wa bajaji na bodaboda.

“Kama wanachajiwa Sh500 nenda kwenye chama chao cha usafirishaji ukaulize, hakuna mamlaka yoyote sisi tunayowapa, wasimamizi wa ruti ni Latra, hivyo kama kuna changamoto, zungumza na mwenyekiti wao, ila mimi sina malalamiko, nasikia kama ninyi mnavyosikia.

“Tunaishikilia bajaji moja, ilikutwa haijabandika leseni ya usafirishaji kwenye kioo na hili ni kosa kisheria,” amesema.

Nyello amesema mmiliki wa bajaji hiyo (bila kumtaja jina) alipopeleka nyaraka walijiridhisha kuwa ameikatia leseni bajaji yake, lakini walipomuuliza kwa nini hakubandika kwenye kioo hakuwa na majibu.

“Tulimwambia asaini nyaraka yetu kuonyesha amekiri kosa lake, lakini alikataa na bajaji bado tunaishikilia,” ameeleza Nyello.

Akizungumzia hilo, Victor Kinabo, makamu mwenyekiti wa chama cha bodaboda na bajaji Manispaa ya Moshi, amekiri kuwepo kwa tozo hiyo ya Sh500 akidai ni kwa ajili ya posho ya vijana wanaofanya kazi ya kusimamia bajaji hizo na huwa hazipelekwi kwenye chama chao.

“Tulikaa vikao na kuteua viongozi ambao watasimamia kudhibiti vitendo vya kihalifu, kusimamia mali za abiria na vitu vingine ambavyo vinakwenda kinyume cha taratibu, hivyo wale ambao walichaguliwa ile kazi ilionekana kama ndiyo sehemu ya ajira yao.

“Hivyo ili kuweza kuwalipa watu hao, madereva waliamua watachanga Sh500 kila siku katika vituo ambavyo bajaji hupanga foleni kusubiria utaratibu wa kutoka kubeba abiria na fedha hizo wale wanaofanya kazi,” amesema.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini wanasimama barabarani kukusanya fedha hizo na si kwenye vituo ambako bajaji huanzia, amesema wanapokaa barabarani wanasaidia kudhibiti vitendo vya kihalifu na mvurugano wa bajaji kutoka njia moja kwenda nyingine.

“Pale barabarani wanasaidia kudhibiti uhalifu lakini pia mkorogano wa bajaji, kwani kila njia ina bajaji, hivyo kuna wakati bajaji za KCMC zinaenda Majengo, hivyo wale walioko barabarani wanasaidia kudhibiti hilo,” amesema

Mwenyekiti wa Bajaji na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro, Bahath Nyakiraria amesema leseni ya usafirishaji kwa bajaji na bodaboda haziandikwi ruti na kwamba kinachowaongoza ni vituo na ni watu wa kukodishwa kwa kuwa ni biashara huria.

“Leseni ya usafirishaji kwa bajaji na bodaboda, haziandikwi ruti na kinachoongoza ni vituo, wao ni watu wa kukodishwa, hivyo ni biashara huria, lakini zipo bajaji zilizoko kituoni zinazopakia kwenda KCMC, Pasua, Soweto, Majengo na kwingine,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!