NewsSWAHILI NEWS

TCRA yaeleza makosa huduma za utangazaji nchini

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka 2021/22 na 2022/23 kuhusu maudhui ya redio, televisheni na mitandao yenye leseni ulionesha  asilimia 26 ya ukiukwaji ulihusu kutozingatia kanuni za kumlinda mtoto.

Kanuni za utangazaji na za maudhui zinawataka watoa huduma kuepuka maudhui yasiyofaa kwa watoto wakati wa familia nzima kusikiliza redio au kutazama televisheni; kuzingatia kanuni za utoaji taarifa za watoto waathirika wa uhalifu na namna ya kuwahoji.

Asilimia 15 ya ukiukwaji ulihusu kutokuzingatia muda wa kutoa vipindi vinavyofaa kuangaliwa na watu wote huku asilimia 15 nyingine zilikuwa matumizi mabaya ya lugha, kutokuzingatia mizania, kuweka maoni binafsi kwenye maudhui.

Mengine yaliyojitokeza ni taarifa nyingi zimejaa kuhama kutoka kwenye ukweli kwa makusudi, kuongeza chumvi au kuacha baadhi ya taarifa na kupotosha maana. Pia kumekuwa na utoaji taarifa zinazohamasisha uchochezi na vurugu.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Saida Mukhi amesema watoa huduma walifikiwa na kamati hiyo kwa elimu na majadiliano ya kanuni wameongeza kiwango cha uzingatiaji.

Hata hivyo, amesema bado kuna ukiukwaji kwenye televisheni za mitandaoni; jambo ambalo amesema kamati inaendelea kulishughulikia.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari amesema mamlaka hiyo inasimamia huduma za utangazaji ili watoa huduma wasitoe maudhui ambayo yatadhuru watazamaji au wasikilizaji kwa namna yoyote ile.

Amesema TCRA inasimamia maudhui hayo kutokana na upekee wa redio na televisheni kama njia ya mawasiliano kwa umma kwa kuwa utangazaji ni njia pekee ya mawasiliano inayowafikia watu wengi kwa haraka.

Kwa kuwa utangazaji unahusisha maudhui ambayo yanaathiri watu kwa namna tofauti, TCRA ina wajibu wa kuwalinda.

TCRA inasimamia utangazaji kwa kubuni na kuratibu mipango ya kuendeleza sekta ya mawasiliano, kutoa masafa ya redio na televisheni, kutoa leseni za utangazaji na za uwekaji mitambo inayowezesha utangazaji. Inasimamia na masharti ya leseni zinazotolewa na pia kanuni na miongozo ya utangazaji.

Lengo ni  kuhakikisha weledi na uzingatiaji wa maadili ya utangazaji na pia ubora wa huduma uliowekwa kikanuni.

Takwimu za hali ya mawasiliano Tanzania hadi Aprili 2024 zinaonesha kuwa vituo vya kurusha matangazo ya televisheni vimeongezeka kwa asilimia 4.6, kutoka 65 mwaka 2023 hadi 68 Aprili, 2024.

Televisheni za waya zimeongezeka kwa asilimia 5.3; kutoka 57 Aprili 2023 hadi 60 Aprili 2024.  Vituo vya redio vimeongezeka kwa asilimia 7.4, kutoka 215    mwaka 2023 hadi 231 Aprili 2024.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!