NewsSWAHILI NEWS

Tatizo la ajira kwa vijana latakiwa kupewa kipaumbele kuepuka yasiyofaa

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiwa katika maandalizi ya awali kabla ya kujifanyia tathmini ya mwenendo wa nchi kupitia Mpango wa hiari wa nchi za Afrika kujitathmini (APRM), wito umetolewa kwamba suala la ukosefu wa ajira lipewe kipaumbele kuepusha uwezekano wa ajenda hiyo kuwasukuma vijana kufanya mambo yasiyofaa.

Ripoti ya mwisho ya APRM iliyotolewa mwaka 2013 ililitaja suala la ukosefu wa ajira kuwa miongoni mwa changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi, lakini  utekelezaji wake haujafanyika kwa ufanisi, hali inayosababisha kuongezeka kundi la vijana wasio na ajira.

Akizungumza leo Julai 11, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wadau uliondaliwa na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba amesema Tanzania ina cha kujifunza kwa kinachoendelea katika nchi nyingine za Afrika, ikiwa ni matokeo ya vijana kukosa ajira.

Amesema nchi inapokuwa na vijana wengi wasio na ajira ni rahisi kushawishika kufanya mambo yasiyofaa, akitoa mfano wa maandamano yanayofanywa na vijana wa Gen Z nchini Kenya na yanayofanana na hayo katika nchi nyingine za Afrika.

“Ripoti ya APRM ya Tanzania mwaka 2013 ilisema suala la ajira hasa kwa vijana, ni bomu ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi linaweza kutuharibia utulivu na amani ambayo tumekuwa nayo kwa miaka mingi. Sasa tunapoelekea kwenye maandalizi ya kufanya tathmini ya pili ni muhimu suala hili likapewa kipaumbele,” amesema.

“Tujiulize tumefikia wapi katika kutatua changamoto hii ambayo inazidi kuwa kubwa siku hadi siku. Kila mwaka kundi kubwa la vijana linamaliza vyuo vikuu, hapo bado kuna wale wanaoishia ngazi za chini za elimu, na wengine hawana elimu kabisa, hawa wote wanakwenda wapi na hakuna ajira,” amesema Kibamba.

Amesema kama jitihada hazitafanyika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, upo uwezekano wa bomu hilo kulipuka kama ambavyo tayari imeshaonekana kwenye mataifa mengine, likiwamo jirani la Kenya ambalo vijana wameongoza maandamano wakisukuma ajenda ya mabadiliko.

Mkuu wa Programu ya Utawala na Diplomasia Afrika katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa Afrika Kusini (SAIIA), Steven Gruzd amesema nchi za Afrika zinapaswa kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotokana na tathmini hizo ili kupata matokeo chanya.

“Watu wasione shida kuzungumza mambo yanayoendelea kwenye nchi na yafanyiwe kazi. Kama ni masuala ya huduma za afya, utawala bora, umasikini, mfumo wa Serikali, madaraka ya Rais haya yote yasionekane magumu kuzungumziwa na huu ndiyo msisitizo tunauweka kwa nchi zote za Afrika,” amesema.

“Kukiwa na uwazi katika tathmini inasaidia kujua ni changamoto zipi zinaikabili nchi husika kuweka mipango ya kukabiliana nazo au kurekebisha maeneo yatakayoonekana hayako sawa. Haya yote yafanyike kwa kushirikisha asasi za kiraia kwa kuwa hizi zipo karibu zaidi na watu,” amesema.

Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Lamau Mpolo amesema utekelezaji wa mpango huo umejikita katika kuhamasisha dhana ya utawala bora ikiwa ni sehemu ya jitihada za nchi kutafuta maendeleo ya kiuchumi.

“Mpango huu ni wa hiari na nchi yetu imeonyesha utayari wa kukubali kujifanyia tathmini katika vigezo vilivyowekwa, tunafanya kila linalowezekana ili maliasili na jitihada zote zinazofanyika zinakuwa kwa manufaa ya wananchi,” amesema.

Mpolo amesema, “Kuna mazuri mengi yalionekana kwenye ripoti iliyopita, mfano uwepo wa lugha ya Kiswahili ulivyosaidia kutuunganisha, amani na utulivu na namna viongozi wetu walivyoachiana madaraka kwa amani na utulivu. Hayo tunajivunia na nchi nyingine zinajifunza kutoka kwetu.”

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!