NewsSWAHILI NEWS

Sugu akumbuka maumivu ya mama yake akihutubia wananchi Kabwe

Mbeya. “Tutawasamehe lakini hatutasahau.” Ni kauli aliyozungumza Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ katika mkutano wa kwanza wa hadhara jijini Mbeya.

Sugu aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa baada ya kushinda uchaguzi uliofanyika Mei 29, 2024 alipombwaga Mchungaji Peter Msigwa ambaye kwa sasa ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza leo Jumatano, Julai 10, 2024 katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika stendi ya daladala Kabwe jijini Mbeya, Sugu amesema hawezi kusahau mateso aliyopitia hadi kuwekwa ndani na kusababisha kumpoteza mama yake mzazi.

Desderia Mbilinyi ambaye ni mama mzazi wa Sugu alifikwa na mauti Agosti 26, 2018, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu. Mwili wake ulisafirishwa hadi Mbeya kwa mazishi.

Katika mkutano huo wa hadhara, Sugu amesema awamu iliyopita ilihitaji kuiua moja kwa moja Chadema, ikiwamo kuzuia mikutano na vikao vya ndani vya kichama akieleza kukamatwa kwake akiwa mbunge kulimsababishia mama yake kukosa uvumilivu hadi kuugua na baadaye kufariki dunia.

“Wengine tuna machungu binafsi, tutasamehe ila hatutasahau, Mama yangu akahoji ikawaje mtoto wangu hakuwahi kukamatwa akiwa muuza mitumba Mwanjelwa,  mpiga Hip Hop duniani iweje kwa sasa mbunge akamatwe na kufungwa akakosa uvumilivu hadi kulazwa na kisha kufariki,” amesema.

Sugu amesema vitendo vilivyokuwapo miaka ya nyuma hasa utekaji vimeanza kurejea akitaja mtu mmoja Sativa aliyepotea Dar es Salaam na kukutwa mkoani Katavi akieleza kuwa analaani na kukemea vikali vitendo hivyo.

Sativa ambaye jina halisi ni Edgar Mwakabela, Mkazi wa Mbezi, jijini Dar es Salaam alitoweka katika mazingira tatanishi Juni 23 na kupatikana Juni 27 pori la Hifadhi ya  Katavi akiwa na majeraha katika mwili wake.

Alisafirishwa hadi Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa matibabu. Kwa sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Mwanasiasa huyo ameongeza kwa sasa matarajio yake baada ya kupewa nafasi ya uenyekiti wa Kanda ataunganisha makundi yote, kushinda uchaguzi ujao kwa kata zote 181 na kujenga ofisi za chama kwa ghorofa eneo la Uyole huku akieleza Chadema ni ya wananchi.

Amesema mabadiliko ya watumishi katika wizara au taasisi yoyote hayana tija badala yake kinachohitajika ni mabadiliko ya sheria ambazo hazina manufaa kwa wananchi.

“Wafanyabiashara hiki ndicho chama chenu, 2025 tunarudi upya, uchaguzi uliopita nilishinda kwa kura nyingi ila walinipora, hivyo tunaomba nafasi tena tuweze kumaliza changamoto zenu, kama ni kodi, Chadema tutakuja na kodi moja ambayo mwananchi atapata haki zote ndani,” amesema.

 “Kuondoa utitiri wa kodi na tozo zisizo za msingi, mkiweka mazingira mazuri ya sekta binafsi mtasaidia vijana kupata ajira kuliko kusubiri utumishi wa Serikali,” amesema.

Mwenyekiti huyo ameeleza kupanda kwa deni la Taifa kunasababishwa na matumizi yasiyo na tija kwa kuwanufaisha baadhi ya viongozi huku wananchi wakiendelea kupata changamoto.

Amesema wakazi wa Mbeya wanaomba utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya sherehe za wakulima (Nanenane) kufanyika jijini humo kwa miaka yote kama ilivyo Dar es Salaam na sherehe za Sabasaba.

“Katika uchaguzi ujao wagombea msikubali kuambiwa suala la barua za mabalozi, wale CCM wanazo balozi zao kumikumi, mtu akikwambia ishu ya balozi mwambie Chadema inayo balozi 20, 20, tutakuwa makini sana kwenye hilo,” amesema.

Mmoja wa makada wa chama hicho, Yusuph Mwambene amesema kwa sasa wanatarajia uchaguzi huru na wa haki huku akiomba tume huru na Katiba mpya, akieleza kuwa kilio cha wananchi ni kuona mabadiliko chanya.

“Tumeona awamu ya sita imeruhusu mikutano ya hadhara na hii ndio demokrasia ya kweli, tunatarajia hata uchaguzi utakuwa wa haki na huru japokuwa bado katiba hatuoni kinachoendelea,” amesema Mwambene.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!