NewsSWAHILI NEWS

Sintofahamu wamachinga Simu2000 kufunga biashara, barabara

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga katika Soko la Simu2000, jijini Dar eS Salaam wameanza mgomo asubuhi ya leo Jumatatu Julai 8, 2024 kwa kufunga barabara, huku wakiimba nyimbo za kudai haki yao.

Wamachinga hao wanadaiwa kulalamikia mpango wa sehemu ya eneo wanalofanyia kazi zao kukabidhiwa kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, Dart inapewa eneo hilo kwa ajili ya kujenga karakana ya mabasi yake mbadala wa ile iliyopo Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Kinachozusha hofu miongoni mwao ni kile wanachoeleza walikabidhiwa eneo hilo na kuahidiwa ndilo litakalokuwa rasmi kwa shughuli zao, baada ya kuhamishwa kutoka maeneo mbalimbali.

Sambamba na hayo, wamachinga hao wana hofu uwepo wa Dart katika eneo hilo, utawaondoa baadhi yao, pia kukiondoa Kituo cha Daladala cha Simu2000 ambacho ndicho tegemeo lao la kupata wateja wanaofika hapo kusubiri usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali.

Mbali na kufunga biashara zao, pia wameweka vizuizi katika barabara kuelekea Sinza na kuzuia magari kuingia na kutoka katika kituo hicho cha daladala.

Nyimbo za ‘hatutaki karakana, tunataka soko letu’ ndizo zilizokuwa zikisikika zikiimbwa na waandamanaji katika eneo hilo.

Wafanyabiashara hao pia walikuwa na mabango yenye jumbe mbalimbali, ikiwemo ‘hatutaki karakana Simu2000 Mama Samia njoo ututetee.’

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!