NewsSWAHILI NEWS

Shahidi aieleza mahakama Alex Msama alivyomwachia eneo

Dar es Salaam. Raymond Shao ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jinsi mfanyabiashara Alex Msama alivyomwambia amuachie eneo liliopo Mbezi Beach ili amlipe fidia ya mali ikiwemo nyumba mbili pamoja na fidia ya mali Sh100 milioni.

Inadaiwa kati ya Aprili hadi Oktoba 2016, jijini  Dar es Salaam mshtakiwa Alex Msama aligushi hati yenye namba D/KN/13504/3/TMM iliyotolewa Septemba 28, 1979 ikiwa na jina Ndelikyama Mweleli ikionyesha namba ya kiwanja 160 cha Mbezi Beach ni eneo la Ndelikyama Mweleli wakati akijua siyo kweli.

Shahidi huyo wa tisa, Shao akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Kafuko mbele ya Hakimu Mfawidhi, Is-Haq Kuppa amedai mwaka 2000 hadi 2016 alikuwa anaishi Mbezi Beach Mtaa wa Bless pamoja na ndugu zake.

Amedai walielezwa na baba yao mlezi kuwa eneo la Mbezi Beach lilikuwa la babu yao anayeitwa Ndelikyama Mweleli ambaye alifariki dunia mwaka 1969 na alizikwa eneo la Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.

“Eneo hili tulionyeashwa na baba mlezi akiwemo na baba mdogo walitueleza eneo la Mbezi ni la babu yangu na lingine lipo eneo la Madale tulishauriwa tujenge nyumba ila hatukuwa na nyaraka za umiliki,” amedai Shao.

Amedai walijenga nyumba mbili katika eneo la Mbezi Beach baada ya miaka miwili kupitia alijitokeza mhindi aliyejitambulisha kwa jina la Mazakhan na kuwaeleza ni eneo wanaloishi ni la kwake huku akiwaamuru waondoke lakini walimbembeleza awalipe fidia kwa kuwa walikuwa wamejenga aliwakatalia.

Baadaye alikuja mshtakiwa Msama akiwaeleza wamuachie eneo hilo ili awalipe fidia ya mali kwa kuwa Mazakhan ameshindwa kuwalipa.

“Baada ya wiki tatu Msama alinipigia simu na kunieleza niende benki ya NBC nikachukue Sh100 milioni kama tulivyokubaliana,” amesema Shao.

Shao amedai baada ya mwaka mmoja Msama alimpigia simu na kumweleza ameitwa katika ofisi za Takukuru hivyo anamtaka amwambie kitu anachotakiwa kuwaeleza Takukuru lakini alimkatalia na kumweleza eneo lao halikuwa na nyaraka za umiliki.

Amedai baada ya wiki moja alipigiwa simu na Ofisa wa Takukuru, Jonson Kisaka aliambiwa afike makao Mkuu ya Takukuru kwa ajili ya mahojiano akiwa yeye pamoja na ndugu zake.

Baada ya shahidi huyo kutoa maelezo hayo kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 15, 2024 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!