NewsSWAHILI NEWS

Sababu zatajwa Geita kubeba maadhimisho Siku ya Idadi ya Watu Duniani

Geita. Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya idadi ya watu, leo Julai 11, 2024, ambayo kitaifa inafanyika mkoani Geita na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo.

Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Mataifa (UN) ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu masuala yanayohusiana na matukio ya kidemografia na kaulimbiu ya mwaka 2024 ni “Idadi ya watu kitakwimu ni muhimu kwenye kufanya uamuzi sahihi katika sera na mipango ya maendeleo yenye usawa kwa wote”.

Ofisa Mipango kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Umrat Mohamed amesema wiki ya maadhimisho hayo imetumika kutoa elimu kwa vijana na wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango na faida ya matumizi sahihi ya takwimu za idadi ya watu katika kujiletea maendeleo.

Mkoa wa Geita umechaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa kutokana na mkoa huo kuwa na kasi ya ongezeko la watu la aslimia 5.4 huku kitaifa ukuaji wa idadi ya watu ikiwa ni asilimia 3.2.

Amesema katika kuadhimisha siku hiyo, mambo mbalimbali yamefanyika ikiwemo kongamano la vijana lililowezesha zaidi ya vijana 1,300 kupatiwa elimu ya afya ya uzazi na afya ya akili pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa njia ya Mkoba.

Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kutoa elimu ya umuhimu wa vijana kushiriki kutoa maoni yao kwenye  Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na leo kwenye kilele cha siku hiyo kunatarajiwa kufanyika kongamano la viongozi litakalojadili  masuala ya watu na maendeleo .

Mchambuzi wa masuala ya idadi ya watu pamoja na maendeleo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa na Idadi ya Watu (UNFPA), Ramadhan Hangwa amesema kasi ya ongezeko la ukuaji wa idadi ya watu ni moja ya sababu zilizofanya maadhimisho hayo kufanyika mkoani humo.

Hangwa amesema wakati wastani wa watoto ambao mwanamke anaweza kuwa nao kitaifa ni wane, kwa mkoa wa Geita, mwanamke mmoja ana idadi ya watoto sita.

Takwimu hizo pia zinaonyesha watu wenye ulemavu kitaifa ni asilimia 11.2 lakini kwenye mkoa huo ni asilimia 10.2, hivyo kuifanya Serikali na wadau kuona umuhimu wa kuadhimisha siku ya idadi ya watu Geita ili pamoja na mambo mengine elimu ya afya ya uzazi itolewe kwa wananachi.

“Masuala ya idadi ya watu zipo changamoto ambazo watu wanakutana nazo kama vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi na mimba za utotoni, haya ni mambo yanayojadiliwa ili kupeleka ujumbe wa changamoto zinazoikumba dunia na Tanzania ikiwemo,” amesema Hangwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Uchechemuzi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Marie Stopes, Oscar Kimaro amesema wao kama wadau wa maendeleo wanashiriki siku hiyo kuhamasisha matumizi ya takwimu sahihi zilizopo ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za Serikali kufikia maendeelo ya Taifa.

“Kama wadau wa idadi ya watu duniani, tunatoa elimu kwa jamii na kuwafundisha juu ya umuhimu wa namna wanayoweza kufanya uamuzi juu ya idadi ya familia wanayopaswa kuwa nayo.

“Siku hii inatukumbusha kuhusu kuwezesha taasisi binafsi na zile za Serikali, namna tunavyoweza kutumia takwimu zinazozalishwa kuleta ujumuishi katika maendeleo,” amesema Kimaro.

Amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu katika mkoa huo, msisitizo zaidi unawekwa kuhakikisha takwimu za watu zinatumika kutoa taarifa juu ya maendeleo yaliyopo kama Taifa.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, amesema ili mipango mizuri yenye tija kwa kizazi cha sasa na badae iweze kupangwa, kuna umuhimu wa kuhakikisha kila aliyepo sasa anatumia taarifa za takwimu zilizopo kuweka mipango itakayofanya kazi hadi 2050.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi yam waka 2022, Mkoa wa Geita una watu 2,977,608 na kati ya hao, wenye umri wa miaka 0 – 17 ni 1,657,365 sawa na asilimia 55.6 ya idadi ya watu wote katika mkoa huo.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!