NewsSWAHILI NEWS

Rushwa, muhali vyatajwa mwiba kukabili vitendo vya ukatili

Pemba. Wakati jitihada za kupinga vitendo vya udhalilishaji zikiendelea kisiwani Pemba, muhali na rushwa vimetajwa kuwa mwiba wa kukomesha vitendo hivvyo.

Hayo yamebainika leo Jumanne, Julai 9, 2024 wakati wa uzinduzi wa mradi wa uwezeshaji wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa wadau wa kupambana na vitendo hivyo kisiwani Pemba.

Akizungumza katika mkutano huo, Sheha wa Shehia ya Kiungoni, Omar Khamis Othman amesema miongoni mwa sababu zinazochangia kutokumalizika kwa kesi hizo ni kuwepo kwa rushwa na muhali, mambo ambayo yanarejesha nyuma mapambano hayo.

Amesema linapotokea tatizo kama hilo, waathirika wanakwenda kuripoti polisi, lakini baadaye wanafuatwa na wanafamilia kupewa chochote na badala yake hafiki tena mahakamani kwenda kutoa ushahidi.

“Tatizo kubwa linalosumbua ni kuwepo kwa rushwa na muhali, mtu anakwenda kuripoti vizuri kesi yake, lakini baadaye anafuatwa na wanafamilia kupewa chochote na hatimaye kushindwa kwenda kutoa ushahidi na kesi kupotea,” amesema.

Akizungumza katika mkutano huo, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zuwena Mohamd Abdulkadir aliyewakilishwa na Hakimu wa wilaya ya Wete, Adam Abdalla Faki amewataka wadau wa mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kuongeza kasi katika mapambano hayo ili kuwakinga watoto wasiharibiwe akisema ndio kundi kubwa linalokabiliwa na changamoto hizo.

Amesema katika kumaliza tatizo hilo wadau kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kusimama imara na kutoa ushirikiano katika kupiga vita vitendo hivyo visiendelee kujitokeza.

“Bado vitendo hivi vinaendelea kujitokeza pamoja na juhudi zote zinazochukulia lakini tunatakiwa kuwa wamoja na kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo,” amesema

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Rashid Hassan Mshamata amesema mradi huo utajikita katika kuanzisha vilabu tofuti kwenye shehia, ikiwemo madrasa lengo ni kuona juhudi za mapambano hayo zinaimarika.

Amesema hatua hii ya unzishwaji wa vilabu kwenye maeneo mbalimbali kwenye shehia kwa kiasi kikubwa yanaweza kusaidia baada ya kupewa elimu juu ya athari za majanga hayo.

 “Lengo kuu la mradi huu ni kuona zile haki anazipata yule, mtu atakayekabiliwa na shida hizo tunataka kuanzisha vilabu katika maeneo mbalimbali kwenye shehia, ikiwemo madrasa tutawapa elimu naamini mpango huo utasaidia katika kuongeza kasi ya mapambano juu ya vitendo hivyo,” amesema Rashid.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau tofauti ikiwemo masheha, polisi, wasaidizi wa sheria walimu na madaktari asasi za kiraia ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo haki za binadamu na makosa ya udhalilishaji.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!