NewsSWAHILI NEWS

Rais Ruto atangaza siku sita za mazungumzo kujadili matatizo ya wananchi

Kenya. Katika kutafuta suluhu juu ya yale wanayolalamikia na Wakenya, Rais wa nchi hiyo William Ruto ametangaza siku sita za mazungumzo ya kitaifa kuanzia Jumatatu ya Julai 15 ili kujadili changamoto zinazokabili taifa hilo.

Taarifa hiyo imetolewa hii leo Jumanne, ikiwa ni baada ya kushauriana na viongozi wa Azimio, wakiongozwa na Raila Odinga wa Chama cha ODM na Kalonzo Musyoka wa Chama cha Wiper.

Rais Ruto amesema katika kongamano la mazungumzo hayo kutakuwa na wawakilishi kutoka sekta mbalimbali wapatao 150 ambapo 50 watapaswa kuwa ni vijana ambao kwa kipindi cha wiki kadhaa wamekuwa mwiba.

“Nafasi 100 zilizosalia zitakuwa ni makundi mengine yenye maslahi kama jumuiya ya kidini, jumuiya ya kiraia, makundi ya kitaaluma, pamoja na vyama vya siasa.

Akihutubia wanahabari katika ukumbi wa mikutano wa KICC jijini Nairobi leo Julai 9, 2024, Rais Ruto amesema mazungumzo hayo yatahusisha wawakilishi kutoka vyama vya kisiasa, mashirika ya kidini, mashirika ya kijamii, waajiri na vijana wa nchi hiyo.

Aidha, kwa nia ya kubana matumizi Rais Ruto amesema wote hao watajigharamia kwa kuwa Serikali haitawalipia ikiwa ni njia ya kupunguza gharama.

“Katika kuhakikisha tunaishi kulingana na uwezo wetu; washiriki wote watagharamia mahudhurio yao wenyewe. Haya ni matokeo ya mashauriano ambayo tumefanya asubuhi ya leo,” amesema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto mkutano huo wa mazungumzo una lengo la kuandaa suluhisho katika yale yanayowakabili Wakenya, aidha amewataka washiriki waliotajwa wawateue wawakilishi wao kufikia mwisho wa wiki hii.

Katika hilo Rais Ruto ameungwa mkono na kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyekuwepo katika hotuba hiyo hii leo ambapo amesema mpango huo ni mkakati mwafaka wa kukabiliana na mzozo wa sasa wa kitaifa.

Odinga ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo akiwa ameongozana na wabunge wa upinzani amesema mkutano huo unatoa fursa kwa Wakenya kutoa madukuduku yao na kushughulikia masuala yanayoisumbua nchi kuelekea kupata suluhu la kudumu.

“Kuna changamoto nyingi zinazoathiri Wakenya, lakini zote zinaweza kutatuliwa,” amesema Odinga huku akizitaja baadhi kuwa ni ukosefu wa ajira, ukabila, usimamizi wa uchumi, rushwa, ufisadi na madeni.

Hatua hiyo ya Rais Ruto inakuja ikiwa kuna maandamano makubwa yanayoratibiwa na vijana maarufu kama Gen Z ya kupinga kutozwa ushuru na kutoridhika na utawala wa Rais Ruto.

Maandamano hayo yalitokana Muswada wa Fedha wa mwaka 2024, hata baada ya Rais Ruto kukataa kutia saini muswada huo kuwa sheria Juni 26.

Naibu Rais, Rigathi Gachagua amewataka vijana wa Gen Z kusitisha maandamano na kuruhusu serikali kushughulikia masuala yao.

Katika hatua nyingine Rais Ruto ametia saini muswada wa marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya 2024.

Kuunda upya baraza la uchaguzi ni miongoni mwa mambo yaliyogusiwa na waandamanaji katika wiki kadhaa za maandamano ikiwa ni baada ya mvutano wa mwaka 2022 baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Kenya ilikumbwa na maandamano katika wiki kadhaa ambapo imeripotiwa watu 39 walipoteza maisha tangu maandamano hayo yaanze Juni 18, kulingana na tume ya kitaifa ya haki za binadamu.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!