NewsSWAHILI NEWS

Mwabukusi kupinga kortini kuenguliwa uchaguzi TLS

Dar es Salaam. Baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kumuengua Boniface Mwabukusi katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa chama hicho, wakili huyo ametangaza kusudio la kwenda mahakamani.

Sambamba na hatua hiyo, amewataka wanachama wengine wa TLS kutoshiriki uchaguzi huo, ili kuishinikiza Kamati ya Uchaguzi iwarejeshe wagombea wote iliowaengua.

Hata hivyo, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TLS, Nelson Frank amesema suala la kwenda mahakamani ni haki ya kila mtu na ipo kikatiba pale anapohisi hajatendewa haki au hajaridhika na uamuzi.

“Kusema ameonewa kwa sababu alizosema, siko kwenye nafasi nzuri ya kumjibu isipokuwa nakala ya hukumu itatolewa na atatumiwa aweze kuoanisha hizo sababu anazosema,” amesema Nelson.

Katika maelezo yake, Nelson amesisitiza kamati hiyo ilifanya shughuli yake kwa weledi kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.

Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 2, 2024, jijini Dodoma, Mwabukusi alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliotia nia ya kuwania urais, kurithi mikoba ya Harold Sungusia anayemaliza muda wake kwa mujibu wa sheria na katiba ya chama hicho.

Wagombea watano waliobaki kuendelea na hatua inayofuata ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba.

Akizungumza leo Jumapili Julai 7, 2024 jijini Dr es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwabukusi ameeleza kutokana na kile anachodai kuonewa, anatarajia kwenda Mahakama Kuu kudai haki yake.

“Mchakato wa kwenda Mahakama Kuu umeshaanza na kesho nitakuwa huko, nipo na mawakili wangu tunashirikiana kuwa nyaraka zetu sawa, ili tuanze kufungua kwa njia ya mtandao na tutawajulisha,” amesema.

Wakati akisubiri hatua za kisheria ambazo ameeleza huchukua muda, Mwabukusi amedokeza ameshaanza mchakato wa kuwashawishi wanachama wasishiriki uchaguzi kushinikiza wagombea wote warejeshwe.

“Nina haki ya kugombea na wawapuuze wanaofurahi kuondolewa kwangu. Wanatakiwa kuniunga mkono na yeyote atakayesema kwa kuwa Mwabukusi ameondoka waendelee basi watambue ni msaliti na ni miongoni mwa waliofanya njama mimi niondolewe,” amesema.

Hata hivyo, wakili huyo ameeleza safari yake tangu mwanzo wa mchakato haikuwa rahisi, kwani ilikumbwa na pingamizi nyingi, lakini kamati ya uchaguzi iliyaondoa kwa kuwa iliona hazina hoja za msingi.

“Pingamizi la kwanza lilikuwa linasema mimi mwanasiasa na sheria wala kanuni zetu hazikatazi kuwa mwanasiasa, bali zinakataza mtu kuwa kiongozi wa chama cha siasa na mhusika alishindwa kuwasilisha ushahidi,” amesema.

Amesema pingamizi la pili lilikuwa linasema alikuwa amepatikana na kosa la kimaadili kwa hiyo hakidhi matakwa ya kanuni ya 13 inayoelezea maadili, huku akieleza mashtaka yalikuwa yamkabili hayana nguvu ya kumzuia kugombea.

Amesema uamuzi wa kuondolewa kwake ni uonevu kwa kile alichoeleza, kila alichokifanya ilikuwa ni kuzungumza ukweli na asingeweza kufumbia macho.

“Uamuzi wa kamati ya nidhamu ulikuwa wa kunionea ulinihukumu kwa sababu eti nimewakosea viongozi wakuu wa nchi, eti sikutakiwa kuzungumza ukweli. Siko njia ya kufumbia macho ujinga hakuna kiongozi wa juu aliyeko juu kuliko Katiba na sheria za nchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, mtu yeyote anapaswa kukosolewa kwa kuzingatia ukweli, huku akieleza kuondolewa kwake kumetokana na kuwakosoa viongozi wa juu, ilhali alikuwa anasema ukweli.

“Mkataba ule wa makubaliano ya nchi na nchi (IGA) uliosainiwa kati ya Tanzania na Dubai unaiba rasilimali za nchi kinyume na sheria,” amesema.

Katika maelezo yake, ameitupia lawama kamati ya uchaguzi kwa kile alichodai ilimhukumu bila kumpa taarifa ya rufaa, badala yake alishtukizwa jioni na kuambiwa nafasi ya rufaa ni kesho yake.

“Niliwauliza mbona sina hiyo taarifa? imetoka kwa nani? wakajibu wamenitumia kwenye email (barua pepe) na sikuona na ili mjue hili ni zengwe hata wagombea wengine hawakuwahi kupigiwa simu kwamba kuna rufaa. Mjue kama rufaa yangu ilikuwa imepangwa,” amesema.

Pamoja na kupewa taarifa ghafla na saa chache kabla ya muda wa kusikiliza mapingamizi, Mwabukusi amesema alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha anafika na mawakili wake na walifanikiwa.

“Nilipambana tukahudhuria na mawakili wangu, mwenyewe nikiwa kwa njia mtandao licha ya kupewa muda mfupi. Tulikanusha pingamizi aliyepeleka hakuwa na miguu mbele ya kamati ya uchaguzi ya rufaa,” amesema.

Katika kamati hiyo, amesema kulikuwa na rufaa tano kati ya hizo, nne zilieleza jambo moja na hazikuwa na mlalamikaji hivyo kamati haikuridhia kuzipokea.

“Nilishangaa baada ya kufika kwenye uamuzi walikubali pingamizi kwa kuanza kuingiza siasa na hekima zao ambazo hazipo kisheria wala kanuni.

 “Ukisema mleta rufaa hana miguu maana yake hakuna kinachoendelea, sasa niwaulize kamati wamepata wapi hiyo sheria ya kuendelea na rufaa waliyotumia kuniadhibu,” amesema.

Mwabukusi amesema hatakubali kurudi nyuma hadi haki yake ipatikane, huku akieleza atakataa ndani ya chama hicho na nje ya Mahakama kwa kuwa uchaguzi huo umekuwa wakilaghai unaenda kuendeleza mfumo wa kunyonya wanachama.

“TLS haijali mambo ya nchi wala wanachama, kuna kikundi cha baadhi ya watu wamejifungia wanatafuna michango ya watu hakuna utaratibu uchaguzi ukifika wanaanza kuwaundia mizengwe watu, ili wapange nani anapaswa kuwa kiongozi ndani ya TLS,” amesema.

Mwabukusi amesisitiza hana kosa linalomzuia asigombee TLS, lakini kuna mawakili wakongwe wanafanya mizengwe hiyo ambayo haipo kisheria, huku akitoa wito kwa mawakili wenzake kukemea hicho kilichotokea.

“Wagombea wenzangu acheni kukubali viti maalumu na kubebwa, onyesheni wanachama mnaoamini demokrasia katika utawala wa kisheria na uwazi, ili mimi nirejeshwe tukashindane kuomba kura, kwani wananiogopa mimi  ni nani katika nchi hii,”amesema.

Amesema kwa hatua aliyofikia hatoogopa wala kutishwa na hatakata tamaa katika kupigania haki yake kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi inayoamini katika msingi wa utawala wa kisheria.

“Natakuwa Rais wa TLS, ili tuwajibike kwa wananchi hatuwezi kukaa tunalipa mamilioni ya michango kuendesha chama, halafu wahuni wachache wanavuruga kanuni zilizopo kwa maslahi yao binafsi,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!