NewsSWAHILI NEWS

Mwabukusi afungua shauri mahakamani kupinga kuenguliwa urais TLS

Dar es Salaam. Wakili Boniface Mwabukusi amefungua shauri la maombi Mahakama Kuu, akiiomba kufanya marejeo ya uamuzi uliomwengua kwenye orodha ya wagombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mbali ya Mwabukusi, Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Ziwa, Steven Kitale naye amefungua shauri la mapitio ya mahakama dhidi ya chama hicho, akiomba kuweka zuio la mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 11, 2024, Mwabukusi amesema shauri hilo la mapitio amelifungua katika Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ndogo ya Dar es Salaam, dhidi ya TLS na limepangwa kutajwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi Julai 17.

Mwabukusi alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, 2024.

Wagombea wengine waliopitishwa kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 2, jijini Dodoma ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, na Sweetbert Nkuba.

Ikielezwa ni kwa sababu ya doa la kimaadili, Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TLS ilimuengua Mwakubusi kwenye kinyanganyiro hicho kitendo anachokipinga.

Mwabukusi anaiomba mahakama kufanya marejeo, akidai Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TLS imemuengua pasipo kumpa nafasi ya kusikilizwa.

Anadai kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na haki ya asili kwa kutoa hukumu bila kumshirikisha.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Ziwa, Kitale amefungua shauri la mapitio ya mahakama dhidi ya TLS akiomba kuweka zuio la mchakato wa uchaguzi.

Kitale akizungumza na Mwananchi jana Julai 10, 2024 alisema katika shauri namba 16018/2024 alilofungua Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, mbele ya Jaji Athuman Matuma, anaiomba Mahakama impe ruhusa kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama pamoja na amri ya muda ili kuzuia mkutano mkuu wa mwaka (AGM) 2024.

Pia anaiomba mahakama kuweka zuio la mchakato wa uchaguzi, kupinga uamuzi wa kamati ya rufaa ya uchaguzi kumuengua Mwabukusi kuwania urais wa TLS na kusimamisha uchaguzi huo hadi uamuzi wa maombi hayo utakapotolewa.

Hoja nyingine amesema ni  kupandishwa ada ya usajili wa washiriki wa mkutano mkuu wa TLS kutoka Sh118,767 na Sh100,000 kwa washiriki wa mtandaoni hadi Sh200,000, uamuzi ambao amedai haukupitishwa na baraza la uongozi la chama hicho.

Amedai hakuna uwazi hasa kwenye masuala ya uchaguzi na mkutano mkuu wa mwaka.

Kwa mujibu wa Kitale, uamuzi wa viongozi wa TLS na kamati ya rufaa ya uchaguzi kutofuata taratibu, unaweza kuleta madhara siyo tu katika uendeshaji wa shughuli za chama, pia utaathiri imani ya wanachama kwa uongozi wa chama hicho.

“Nimeomba Mahakama itoe amri ya kutupa nyaraka zinazohitajika na pia kusitisha shughuli zinazoendelea hadi haki itakapotendeka. Tunahitaji kuwa kitu kimoja na kushirikiana kuhakikisha chama chetu kinajiendesha kwa mujibu wa sheria na kanuni zetu,” amesema.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni TLS, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambao kisheria watatakiwa kuwasilisha kiapo kinzani Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza. Shauri hilo limepangwa kutajwa Julai 15, 2024 mbele ya Jaji Athuman Matuma.

Kukiwa na mashauri hayo mahakamani, Rais wa TLS anayemaliza muda wake Harold Sungusia alipotafutwa na Mwananchi kupitia ujumbe mfupi wa maneno (sms) ameandika:

“Hilo jambo tutajadili kesho (Julai 12) kwenye kikao cha Baraza la Uongozi.”

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!