NewsSWAHILI NEWS

Muuguzi aliyetoweka KCMC alitarajiwa kulipia mahari mwezi huu

Moshi. Wakati uchunguzi wa tukio la kutoweka kwa muuguzi wa Hospitali ya KCMC, Lenga Masunga (38) ukiendelea, familia yake imesema ndugu yao huyo alikuwa katika harakati za kufunga ndoa na mwezi huu wa Julai alikuwa atoe mahari.

Muuguzi huyo wa idara ya masikio, pua na koo (ENT) anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 2, 2024 nyumbani kwake katika mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akiishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Hospitali ya KCMC, Lenga alikuwa mapumziko ya siku mbili (off), Julai 2 na 3 na kwamba alitakiwa kuwepo kazini Julai 4, 2024 lakini hakuonekana, hali iliyoibua mashaka na kusababisha uongozi wa hospitali hiyo kumtafuta kupitia simu zake za mkononi ambazo hazikupatikana hadi sasa.

Jana, mwenye nyumba alikokuwa akiishi muuguzi huyo, Robert Mwakalinga alidai kuwa Lenga aliondoka usiku wa Julai 2, 2024 na kuacha mlango wa chumba chake ukiwa wazi hadi kulipokucha asubuhi Julai 3, 2024.

Akizungumza na Mwananchi, kaka wa muuguzi huyo, Paschal Jeremiah ambaye ametokea mkoani Shinyanga, amesema ndugu yake alikuwa akitegemewa na familia yake na mwezi huu wa Julai alikuwa na mpango wa kutoa mahari na watangaze siku ya ndoa yao.

Amesema tukio la kutoweka kwake limewapa mashaka makubwa na kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kujua alipo ndugu yao huyo.

“Nilipigiwa simu na ndugu yangu ambaye yupo hapa Kilimanjaro akiniarifu mdogo wangu anayefanya kazi KCMC amepotea na hajulikani alipo, nami nilijaribu kumtafuta kwenye simu zake, lakini sikumpata hali ambayo imenifanya nifunge safari hadi Kilimanjaro kujua kilichotokea,” amesema ndugu huyo.

Amesema baada ya kufika Kilimanjaro, alikwenda kituo cha polisi kuandika maelezo ya ndugu yake kupotea na baadaye kuzungumza na uongozi wa hospitali ya KCMC ambao walimweleza suala hilo lipo polisi ambalo wanaendelea nalo na uchunguzi.

Nyumba alikokuwa akiishi Muuguzi wa hospitali ya KCMC idara ya masikio, pua na koo iliyopo mtaa wa Rau Pangaleni, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.Picha na Omben Daniel

“Tunaiomba serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi na usalama kutusaidia katika suala hili, maana hadi sasa tupo gizani hatuelewi kama ndugu yetu yupo mzima au yupo kwenye hali gani,” amesema Jeremiah.

Kaka yake huyo amesema hajui ni kitu gani kimemtokea ndugu yake huyo ambaye tayari alishamtambulisha mchumba wake ambaye ni mkazi wa Moshi na mwezi huu walikuwa wapeleke mahari na kupanga tarehe ya ndoa yao.

“Januari mwaka huu, alitupa taarifa kwamba amepata mchumba huku Kilimanjaro, tukamwambia sawa, akatuambia tuje tuelewane na upande wa mwanamke kuhusu suala la mahari ambapo tulimtuma mwakilishi, wakafanya mazungumzo ya mahari, tukapanga mahari ni kiasi gani na tukaelewana,” amesema na kuongeza:

“Mahari tulikuwa tutoe Juni au Julai, hivyo mwezi huu wa Julai nilikuwa nije mimi na baba kutoa mahari, sasa nimeshangaa ni kitu gani ambacho kimetokea, Juni 25, niliongea naye nikamwambia nakuja tutoe mahari na baada ya hapo tupange tarehe ya harusi.”

Familia ilivyolipokea tukio

Akizungumzia namna familia ilivyopokea taarifa za kutoweka Lenga, amesema wazazi wake wamekosa amani kwa kuwa mtoto wao huyo alikuwa ni tegemeo kubwa katika familia yao.

Paschal Jeremiah, ndugu wa Muuguzi wa KCMC, Lenga Masunga aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha akizungumza na waandishi wa habari nyumbani alikokuwa akiishi ndugu huyo. Picha na Omben Daniel

Amesema Lenga ambaye ni mtoto wa nane kuzaliwa katika familia yao, familia ilitumia gharama kubwa kumsomesha ili baadaye aweze kuwasaidia na kwamba kilichotokea kimewavunja moyo kwa kuwa hawajui kama ndugu yao ni mzima au nini kimetokea.

“Ni mtu ambaye tulikuwa tukimtegemea sana, maana familia ilitumia gharama kubwa kumsomesha ili baadaye aikomboe familia, tunaomba serikali iharakishe uchunguzi lakini mengine tunamwachia Mungu, maana hatujui kama ni mzima au la,” amesema ndugu huyo wa Lenga.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Uhusiano wa hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo amesema suala hilo kwa sasa wameliachia Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi wake.

“Suala hili tumeliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wake, sisi kama uongozi wa hospitali tunaendelea na jitihada za kila namna kumtafuta kujua amepatwa na changamoto gani au ni nini kimemtokea,” amesema na kuongeza:

“Kinachotushtua zaidi ni kwamba simu zake hazipatikani hadi sasa na kama uongozi tuna mshtuko mkubwa maana hatujui nini kimetokea.”

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi ni kwamba tukio hilo tayari limeripotiwa kituo cha Polisi cha Longuo na kutolewa RB namba LNG/RB/33/2024 na uchunguzi unaendelea.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!