NewsSWAHILI NEWS

Moto wateketeza vyumba 11 vya wapangaji Ngarenairobi Siha

Siha. Nyumba yenye vyumba 11 vya wapangaji katika Kijiji cha Ngarenairobi, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro iliyojengwa kwa mbao, imeteketea kwa moto na kusababisha hasara.

Tukio hilo lilitokea Jana Jumamosi Julai 6, 2024 usiku, chanzo kinadaiwa ni jiko la gesi lililolipuka kwenye moja ya vyumba vya wapangaji.

Mtendaji wa Kijiji hicho, Seif Mwemgamba, akizungumza na Mwananchi kwa simu amesema moto huo umesababisha hasara kubwa kwa sababu hakuna mpangaji aliyeokoa kitu chochote.

“Yaani mtu alivyotoka ndivyo hivyo alivyo, kama nguo alizovaa ndiyo hizohizo, vitu vyote ndani vimeungua na wengine walikuwa wanalaza pikipiki ndani zimeteketea, yamebaki majivu tu,” amesema ofisa Mtendaji huyo.

Amesema eneo hilo wengi wamejenga nyumba za mbao na ndiyo maana vitu vyote vimeteketea.

 “Nadhani elimu tu ikiwaingia wananchi, tutaepuka hizi ajali za mara kwa mara pia watajenga nyumba imara kwani hizi za mbao likitokea janga la moto hakuna namna wanaweza kuokoa vitu,” amesema mtendaji huyo.

Mwananchi lilizungumza pia na mkazi wa Ngarenairo, Robart Mrisho ambaye amesema ili kuepuka ajali hizo za moto zinazounguza nyumba, ni vema wakaanza kuweka umbali wa kutosha kutoka nyumba moja hadi nyingine.

“Tukijenga hivyo itasaidia, nyumba moja ikiungua moto wake hauwezi kufika kwenye nyingine, pia tunapaswa kujenga nyumba za matofali sasa, changamoto ni gharama za ujenzi,” amesema Mrisho.

Mrisho amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka sambamba na wataalamu wa mipango miji, kutembelea eneo hilo hasa Kata ya Ndumeti na Ngarenairo wakazungumze na wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga nyumba za kudumu.

“Watu hawataki kuelewa pamoja na hali ngumu ya maisha, lakini nyumba bora ni muhimu, hizi hasara za kila siku zinawarudisha nyuma kimaendeleo wanaounguliwa nyumba zao, wengi wanapoteza kila kitu,” amesema.

Akilizungumzia hilo,  Dk Timbuka amesema, “nina taarifa ya tukio hilo, hivi tunapozungumza nipo njiani naelekea huko, moja ya mipango yetu ni kuwatafutia makazi mbadala kwanza hawa waliokumbwa na adha hii, lakini pia kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari zaidi ili kuepusha matukio ya namna hiyo,” amesema Dk Timbuka.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!