NewsSWAHILI NEWS

Mkulima asimulia wafugaji walivyomlazimisha aache ng’ombe wale mpunga

Kilosa. Mkulima wa kijiji cha Mabwegele, Hamisi Waziri aliyeshambuliwa na wafugaji akivuna mpunga shambani kwake, amesema sababu ya shambulizi hilo ni kuwazuia kuwalisha ng’ombe mpunga aliouvuna.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Julai 7,2024  baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambako alikuwa akitibiwa majeraha aliyoyapata kwenye shambulio hilo, amesema kuwa kosa lake lilikuwa ni kuwazuia kulisha ng’ombe mpunga wake.

 Anasimulia siku ya tukio akiwa shambani kwake anavuna mpunga na kijana wake aitwaye Omary, walitokea wafugaji wawili wa jamii ya Kimasai wakiwa na kundi la ng’ombe ambapo waliwaingiza shambani kwake na kuwalisha mpunga aliovuna, huku wakimwambia maneno makali na kumtishia kwa sime.

“Baada ya kuingiza mifugo nikawauliza kwa nini wanalisha ng’ombe mpunga wangu. Walijibu niwaache ng’ombe wale mpunga. Nikapambana nao wakaondoka kunywesha ng’ombe maji mtoni. Waliporudi  waliongezeka wenzao wengine wawili, jumla wakawa wanne na kulazimisha kulisha mifugo yao,” anadai Waziri.

Anasema alipokuwa anapambana nao, kijana wake naye akaamua kuingilia kati na kuanza kupambana nao pia.

“Ndipo mfugaji mmoja akachomoa sime na kunikata mkononi na akanirushia rungu lililonipata usoni nilidondoka chini na kupoteza fahamu,” anasimulia Waziri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake. Picha Hamida Shariff

Hata hivyo, anasema wakati wafugaji hao wakiendelea kumshambulia pale chini alipodondoka, kijana wake alianza kupiga kelele kuomba msaada.

“Ndipo wakatokea akina mama wa Kimasai wakaanza kuwabembeleza wale vijana waache kunishambulia, lakini hawakufanya hivyo wakamgeukia naye mtoto wangu walimkata na sime, ambapo alifanikiwa kupiga simu kwa ndugu zangu, walikuja na kutuchukua na kutuwahisha Hospitali ya Mtakatifu Joseph Dumila,” anasema.

Anasema siku tatu alizolazwa hospitalini hapo, hajui kama mpunga wake aliouacha shambani uko usalama au uliliwa wote na ng’ombe.

“Ila nimesikia wafugaji hao walirudi tena shambani kuendelea kulisha mifugo yao mpunga wangu,” anadai Waziri.

Naye Juma Waziri, ambaye ni kaka wa Waziri, anasema baada ya kupigiwa simu na kupewa taarifa za kushambuliwa kwa mdogo wake na kijana wake, alikodi bodaboda na walipofika shambani, alimkuta mdogo wake akiwa ameanguka chini na hana fahamu. Pamoja na wasamaria wema wengine, walitafuta usafiri na kuwapeleka kituo cha polisi ambako walipewa fomu namba tatu (PF3) na kisha kwenda Hospitali ya Mtakatifu Joseph Dumila kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya kufika hospitali na kupatiwa matibabu ya awali, daktari alitushauri huyu mdogo wangu tumpeleke Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kupatiwa vipimo vikubwa vya kichwa, kwa sababu alikuwa na wasiwasi kwamba rungu alilopigwa lingekuwa limempa madhara makubwa,” anasema Juma.

Anasema baada ya kufika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, mdogo wake alifanyiwa vipimo vikubwa na kuonekana hajapata madhara ya ndani. Walimruhusu kutoka hospitali na alipatiwa dawa za kuendelea kutumia akiwa nyumbani.

Kuhusu kijana aliyekatwa sime, Juma anasimulia ameshonwa na sasa anaendelea vizuri.

Silvatory Sege, aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Kilosa 2020 kwa tiketi ya Chadema na mkazi wa Kilosa, ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha wote watakaokamatwa kwa tuhuma za kumshambulia mkulima huyo wanafikishwa mahakamani.

Sege amesema hatua zikichukuliwa huenda likawa fundisho kwa wafugaji wengine wenye tabia kama hizo za kusababisha migogoro.

Aidha, ameiomba Serikali ya wilaya kuwachukulia hatua viongozi wa vijiji wanaouza ardhi kiholela na kusababisha migogoro ambayo husababisha majeraha na hata vifo.

Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wake na wananchi, alisema pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, bado viongozi wa vijiji wameendelea kuuza maeneo kiholela na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi.

“Hawa viongozi wa vijiji ndio chanzo kikubwa. Wao ndio wanaouza ardhi kinyume cha sheria. Sasa kama Serikali hatutakubali migogoro itokee tutashughulika na yeyote atakayevunja sheria, kuchochea ama kusababisha migogoro,” alisema Shaka.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio.

Amesema Waziri alishambuliwa kwa kupigwa rungu akiwa shambani kwake akivuna mpunga.

Kamanda Mkama amesema tayari vijana wawili ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimasai wameshakamatwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo.

“Ni kweli tukio hilo limetokea, lakini kwa ushirikiano wa wananchi, tayari tumeshawatia mbaroni watu wawili ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimasai na sasa tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani,” amesema Kamanda Mkama.

Amewataja vijana hao waliokamatwa ni pamoja na  Petro Samuleke na Samwel Mkochoi wote wakazi wa Kilosa.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!