NewsSWAHILI NEWS

‘Mgogoro’ waibuka machinga Simu2000, mgomo wanukia

Dar es Salaam. Hofu imezuka kwa wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga katika Soko la Simu2000, jijini hapa, baada ya kuwepo mpango wa sehemu ya eneo hilo kukabidhiwa kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, Dart inapewa eneo hilo kwa ajili ya kujenga Karakana ya mabasi yake, mbadala wa ile iliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam.

Kinachozusha hofu miongoni mwao ni kile wanachoeleza, walikabidhiwa eneo hilo na kuahidiwa ndilo litakalokuwa rasmi kwa shughuli zao baada ya kuhamishwahamishwa kutoka maeneo mbalimbali.

Sambamba na hayo, machinga hao wana hofu uwepo wa Dart katika eneo hilo, utawaondoa baadhi yao, kadhalika kukiondoa Kituo cha Daladala cha Simu2000, ambacho ndicho tegemeo lao la kupata wateja wanaofika hapo kusubiri usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali.

Kutokana na mazingira hayo, Mwananchi linazo taarifa za maandalizi ya mgomo wa machinga katika soko hilo, unaotarajiwa kuanza kesho Jumatatu, Julai 8, 2024, wakishinikiza Serikali iwasikilize na kubadili uamuzi wake.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo lilipo eneo hilo, Aron Kagurumjuli amesema pamoja na Dart kujenga karakana yake katika eneo hilo, hakuna mfanyabiashara atakayeathirika zaidi ya kuwekewa mazingira mazuri.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Julai 7, 2024, mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema kinachowapa hofu ni uamuzi wa makabidhiano ya eneo hilo kufanywa bila wafanyabiashara kushirikishwa.

Ameeleza walipaswa kushirikishwa tangu Dart ilipowasilisha kusudio au ombi la kupewa eneo hilo, ili wajadili kwa pamoja kama inawezekana au vinginevyo.

“Hatukushirikishwa na tunashangaa juzi (Julai 4, mwaka huu) Manispaa inatangaza kuwa eneo hilo la stendi na soko wamepewa Dart ili wajenge Karakana ya mabasi,” amesema.

Lakini hilo, amesema limefanyika wakati tayari wafanyabiashara hao walishakuwa na tetesi za Dart kupewa eneo hilo tangu Oktoba 2023 na hawakuwahi kuambiwa rasmi.

Katika tetesi za Oktoba 2023, amesema wafanyabiashara waligoma na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba alikwenda na kuwaambia hakuna mpango wa Dart kupewa eneo hilo.

“Hata mwaka mmoja haujaisha tangu eneo hili liboreshwe na Serikali na wafanyabiashara kutumia fedha zao kukamilisha maboresho hayo Manispaa ya Ubungo inatangaza imewapa Dart,” amesema.

Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Amos amesema kinachomuumiza ni uwekezaji wa kumalizia ujenzi wa banda la biashara alioufanya ambao hatimaye unakwenda kupotea.

“Nimetumia karibu Sh500,000 kuboresha banda langu, leo hii tunapoambiwa Dart wanakuja na tumezoea kuhamishwahamishwa inatupa wakati mgumu. Kwa nini tusingeambiwa mapema ili tujadiliane,” amesema.

Uamuzi huo wa Manispaa ya Ubungo, umemkatisha tamaa ya biashara Neema Swai anayefanya biashara katika soko hilo.

Neema amesema alidhani Simu2000 ndiyo eneo la mwisho kuhamia kibiashara, lakini kwa dalili anazoziona muda si mrefu atahamishwa tena na Serikali.

“Kila nilipohamishwa nilipoteza mtaji, kuhama kunafilisi huku nako wametufuata kwa nini wasingepewa maeneo mengine kwani Ubungo ina Simu2000 pekee,” amehoji.

Mwananchi Digital linazo taarifa eneo hilo lina jumla ya mita za mraba 36,000 na kati ya hizo, Manispaa imepanga kuipa Dart 30,000 na mita za mraba 6,000 ndizo zitumike na wafanyabiashara.

Katika soko hilo, kuna wafanyabiashara zaidi ya 1,000 na wanaeleza mita za mraba zitakazoachwa kwa ajili yao hazitatosha.

Hofu nyingine za wafanyabiashara kutokana na uamuzi huo wa Manispaa ni kuondoka kwa kituo cha daladala, wakisema kikiondolewa hakutakuwa na mzunguko wa biashara.

Baraza la madiwani laridhia

Katika taarifa ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ubungo ya Julai 4, 2024, Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Nyaigesha amesema baraza hilo limeridhia kuipa Dart eneo hilo.

“Baada ya kutafakari maombi hayo (ya Dart), hatimaye Manispaa ya Ubungo imekubaliana na ombi hilo. Ombi hilo limeridhiwa baada ya kupitia vikao mbalimbali ikiwemo kwa Mkuu wa Wilaya na vikao vya wataalamu wa manispaa,” amesema.

Sambamba na vikao hivyo Nyaigesha amesema kamati ya fedha ya baraza la madiwani la manispaa nalo lilijadili kisha baraza la madiwani kwa ujumla wake limejadili.

“Baada ya majadiliano hayo na madiwani kuonyeshwa mchoro mzima wa mradi huo na wao kutafakari na kuona wafanyabiashara waliopo pale watakwenda wapi, hivyo basi leo hii (Julai 4), baraza limeamua rasmi kwamba eneo litolewe kwa Dart,” amesema.

‘Baraza limegawa kimagumashi’

Licha ya taarifa hiyo ya Nyaigesha, Mwananchi imearifiwa, kilichoelezwa na Meya huyo si msimamo wa baraza la madiwani.

Kadhalika, chanzo hicho ambacho ni sehemu ya wajumbe wa kikao cha baraza hilo, kimesema hawakuwahi kujadili kuhusu kukabidhi eneo hilo kwa Dart isipokuwa waliwahi kupewa elimu tu.

“Hata hicho kikao cha Julai 4, hakikuwa cha kujadili kuwapa Dart eneo, tuliitwa kwa ajili ya kupewa elimu ya namna Dart itakavyolitumia eneo, lakini tunashangaa baadaye inatoka taarifa kwamba tumeridhia, wamepewa kimagumashi,” amesema.

Chanzo hicho, kinadai kuna watu wamenunuliwa kuhakikisha suala hilo linapitishwa na Baraza la Madiwani kwa haraka.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli amekiri kuwepo kwa mpango huo akifafanua hautaathiri uwepo wa wafanyabiashara wala kituo cha daladala.

Kwa mujibu wa Kagurumjuli, hakuna machinga atakayeondolewa katika eneo hilo kutokana na utekelezwaji wa mpango huo, zaidi ya kuboreshewa maeneo yao ya kufanyia shughuli zao.

“Kabla ya lolote wataboreshewa kwanza eneo la kufanyia biashara, likishakamilika kuboreshwa watapewa ni hapohapo wala si kwingine,” amesema.

Katika maboresho hayo, Mkurugenzi huyo amesema vibanda 989 vya machinga, fremu za maduka makubwa 186 na maeneo ya mama na babalishe yatajengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Amesisitiza tathmini imeshafanyika na imebainika eneo litakalojengwa kwa ajili ya wafanyabiashara litawatosha waliopo na mengine yatabaki.

Baada ya hatua hiyo, amesema ndiyo utekelezaji wa ujenzi wa karakana ya Dart utaanza na kwamba hakutakuwa na mwingiliano kati ya biashara za machinga na mradi huo.

Kuhusu kituo cha daladala, amesema hakitaathirika.“Hakitaathirika litakuwa eneo bora zaidi kuliko maeneo mengine yote na litakuwa na biashara kubwa zaidi, ukizingatia kitaunganishwa na kituo cha uwekezaji cha Ubungo,” amesema.

Kwa mujibu wa Kagurumjuli, mipango ya Serikali juu ya maendeleo ya wananchi inabadilika kila siku na utekelezwaji wake unazingatia tija iliyopo.

“Hakuna mpango wa maendeleo unaopangwa na Serikali unaokuja kuwa shida baadaye kwa wananchi wake,” amesisitiza.

Alipoulizwa ni lini mradi huo utaanza, amesema kwa sasa wapo katika hatua ya kukamilisha michakato ya ndani kisha kwenda kuzungumza na wafanyabiashara kuwaelimisha kuhusu mpango wote ulivyo.

“Wasubiri waambiwe waangalie utekelezaji wa programu yenyewe ndiyo waseme changamoto,” amesema.

Historia ya machinga na eneo hilo

Chimbuko la biashara za machinga katika soko hilo ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la Septemba mwaka 2021 alipotaka wafanyabiashara hao wapangwe kutoka barabarani hadi katika maeneo rasmi.

Manispaa ya Ubungo chini ya Mkuu wa Wilaya wa wakati huo, Kheri James iliratibu jambo hilo na kuwahamisha machinga kutoka maeneo mengine yote na kuwapeleka Simu2000.

Hatua hiyo ilifuatiwa na maboresho ya soko hilo yaliyozinduliwa na Amos Makalla (alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), Juni 2022 na Sh70 milioni zilitolewa kufanikisha hilo kwa awamu ya kwanza.

Baadaye Mei 2023 Manispaa ya Ubungo ilitoa Sh100 milioni kwa ajili ya maboresho zaidi yaliyohusisha ujenzi wa mabanda na kisha ilitoa Sh39 milioni na kufanya jumla ya vibanda vilivyojengwa vifikie 234.

Kati ya vibanda hivyo, 170 viligawiwa kwa wafanyabiashara Septemba mwaka jana na vingine 41 viligawiwa baadaye.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!