NewsSWAHILI NEWS

Mgambo apigwa na wamachinga, akimbilia kanisani

Mwanza. Askari anayedaiwa kuwa wa Jeshi la Akiba maarufu mgambo ambaye jina lake halikupatikana amekimbilia kanisani kunusuru maisha yake baada ya kushambuliwa na wafanyabiashara ndogondogo maarufu Wamachinga.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Julai 10, 2024, eneo la Soko la Buhongwa jijini Mwanza, wakati mgambo hao walipochukua matunda ya Wamachinga wanaofanya biashara eneo hilo.

Katika eneo hilo saa 3.20 asubuhi, Mwananchi imeshuhudia kundi la Wamachinga wakiwa wamezingira uzio wa Kanisa Katoliki Kigango cha Buhongwa wakishinikiza mgambo aliyeingia kwenye uzio huo atolewe, wakidai wamechoshwa na tabia yao ya kuwanyang’anya na kuharibu bidhaa zao.

Machinga katika eneo hilo, Abdallah Mohammed amesema mgambo hao waliwasili Buhongwa saa 3.00 asubuhi, wakaanza kuchukua matikiti na mananasi ya mfanyabiashara, ndipo Wamachinga wengine walipomzingira mmojawao na kuanza kumpiga.

Mohammed amesema baada ya kuzidiwa, dereva wa gari lililowabeba mgambo hao aliliondoa eneo hilo, huku wengine wakikimbia na kudandia, lakini mgambo huyo akabaki.

Amesema alipopata upenyo, alikimbia na kuingia kwenye chumba kilichopo ndani ya uzio wa kanisa hilo.

“Wafanyabiashara eneo la Buhongwa wamechoka kwa sababu wapo sehemu sahihi, lakini wanashtukizwa na bidhaa zao kuchukuliwa. Wanapojaribu kujua haki zao, wanapigwa. Sasa wamechoka,” amesema Mohammed.

Baadhi ya machinga wakiwa wamezingira uzio wa Kanisa Katoliki Kigango cha Buhongwa jijini Mwanza wakishinikiza mgambo atolewe.  Picha na Mgongo Kaitira.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buhongwa jijini Mwanza, Pily Naman amesema baada ya kupata taarifa za vurugu hizo, alifika eneo hilo akiwa na mgambo wa kata ili kuimarisha ulinzi machinga wasivunje uzio wa kanisa hilo na kuendelea kumshambulia mgambo huyo.

“Mgambo wa halmashauri wakiwa kwenye operesheni zao wameshambuliwa kwa kurushiwa mawe katika harakati za kuondoa gari la jiji, gari lilitoka likamsahau mwenzao ambaye ili kujiokoa akakimbilia kanisani. Lakini OCD amefika hapa na kumnusuru yule mgambo,” amesema Pily.

Baada ya kuzingira uzio wa kanisa hilo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD), Virginia Sodoka akiwa na gari la polisi (Defender) iliyokuwa na askari wenye silaha, walifika lilipo kanisa hilo na kuzingira uzio kisha kumchukua mgambo huyo na kumpakia kwenye gari lao.

Machinga hao hawakuridhishwa na uamuzi wa polisi, wakaanza kurusha mawe uelekeo lilipokuwa gari lao, dereva aliliondoa kwa kasi, huku machinga wakiendelea kurusha mawe.

Mwananchi lilipomtafuta msimamizi wa Askari wa Akiba wa Jiji la Mwanza, Philotus Ngosi amekanusha mgambo kupigwa (bila kumtaja jina) na kukimbilia kanisani, akidai aliyenusuriwa na polisi huenda akawa amefananishwa na askari wake.

“Tumefika Buhongwa na kuendesha operesheni yetu kisha tukaondoka japo kuna vurugu ziliibuka lakini tulifanikiwa kuondoka na askari wangu wote, hivi ninavyozungumza na wewe niko ofisi za jiji hapa na askari wangu wote hata hao unaosema wamevaa jezi ya Yanga wapo hapa wako salama,” amesema Ngosi.

Mfanyabiashara mwingine, Sauda Hussein amesema uzoefu unaonyesha mgambo wanapofika walipo machinga huchukua bidhaa na kutokomea nazo jambo linaloathiri mitaji yao.

Ameiomba Serikali kutafuta mwarobaini wa mvutano baina ya machinga na mgambo.

“Tunamwambia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba tumechoka na hizi kero za kunyang’anywa mizigo, samaki na matikiti. Tunakaa bila Amani, tunachomuomba atutafutie nafasi nyingine tunapoweza kukaa. Tunakomalia hapa kwa sababu kuna msongamano wa watu na biashara yetu inategemea watu,” amesema Sauda.

Mchuuzi wa mbogamboga ambaye hakutaka jina lake kutajwa amesema mgogoro baina ya machinga, mgambo na Serikali hautakoma akidai masoko waliyopangiwa machinga yamejengwa maeneo yasiyo na msongamano wa watu jambo linalosababisha wakose wateja wa bidhaa zao.

“Wamama tumechoka tuna Vicoba, mikopo na tunasomesha watoto, tunakopa ‘mkopo kausha damu’ unakuja unahemea mzigo mgambo anakuja anabeba. Masoko mliyotupangia mmetupeleka porini, kule porini tukauzie ngedere,” amehoji.

Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo ameitaka Serikali kuangalia upya uamuzi wa kuwapanga machinga katika masoko aliyodai yamechangia kuwafilisi kutokana na kukosa wateja, ndiyo maana wanarejea maeneo yenye msomgamano wa watu.

“Viongozi tulipeleka mapendekezo ya maeneo ambayo machinga wanatakiwa kupangiwa wafanye biashara zao kwa utulivu, ikiwemo kuomba baadhi ya barabara za katikati ya jiji zifungwe lakini Serikali haikutusikiliza, imejenga masoko maeneo ambayo machinga hatukuyapendekeza,” amesema.

Tembo ametaja maeneo yaliyopendekezwa kuwa ni yenye msongamano wa watu ikiwemo Buhongwa, baadhi ya barabara zilizoko katikati ya Jiji la Mwanza, Igoma na Nyakato ‘National’ badala yake Serikali iliwaondoa machinga katikati ya jiji la kuwapanga katika Soko la Mirongo, Mbugani, Ukwaju, Mbao Nyegezi, Mabatini, Dampo, Igoma, Nyaburogoya, Mchafukoga, Igogo, Mkuyuni na Iseni.

Julai 5, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alikutana na menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kikiwemo ‘kikosi kazi’ cha mgambo kusikiliza taarifa ya Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba ya kuwaondoa machinga maeneo yasiyo rasmi.

Alimtaka kuandaa fomu maalumu ambayo itajazwa na mfanyabiashara kila mgambo atakapobeba bidhaa zake.

Mtanda alitoa kauli hiyo kutokana na wafanyabiashara kuwalalamikia mgambo kuchukua bidhaa zao na baadaye kupokea au kurudishiwa zikiwa pungufu.

Kibamba alisema jiji hilo linakadiriwa kuwa na machinga zaidi ya 11,850.

Amesema wafanyabiashara wapya wanaingia kila siku jijini humo miongoni mwao ni wahitimu wa shule na vyuo mbalimbali nchini.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!