NewsSWAHILI NEWS

Mchungaji kortini akikabiliwa na mashtaka matano Dar

Dar es Salaam. Raia wa Congo ambaye ni mchungaji, Daniel Mgonja (23) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kujishughulisha na shughuli za kichungaji bila ya kuwa na kibali.

Wakili wa Serikali, Rafael Mpuya akisoma hati ya mashtaka leo Jumanne, Julai 9,2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu amesema Juni 24, 2023 katika ofisi za uhamiaji zilizopo Kurasini jijini humo mshtakiwa huyo aliishi bila ya kuwa na kibali kinachomruhusu kuwepo nchini.

Katika shtaka la pili tarehe na maeneo hayo mshtakiwa huyo alitoa taarifa za uongo ili ajipatoe Kitambulisho cha Taifa (Nida) wakati akijua siyo kweli.

Katika shtaka jingine, tarehe hiyo na maeneo hayo mshtakiwa huyo alitoa nyaraka za uongo ikiwemo cheti cha kuzaliwa na Nida ambavyo alivipata kwa njia ya uongo ili aweze kujipatia hati ya kusafiria.

Mpuya amedai katika shtaka la nne mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kuwadanganya maofisa wa uhamiaji wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi aliwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia hati ya muda ya kusafiria.

Katika shtaka la mwisho mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kujishughulisha na shughuli za kichungaji bila ya kuwa na kibali cha kuishi nchini.

Wakili Mpuya baada ya kumsomea mshtakiwa huyo mashtaka yanayomkabili ndipo hakimu Magutu alimuuliza kama mshtakiwa huyo ametenda makosa hayo na amekiri kutenda.

Kesi hiyo inarudi Julai 12, 2024 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!