NewsSWAHILI NEWS

Mbwa wenye kichaa watishia usalama wa wananchi Dar

Dar es Salaam. Halmashauri ya Ubungo imewataka watu wanaofuga mbwa kuwa na vibali  vitakavyowawezesha kutambulika na kuwa na usimamizi madhubuti wa mifugo hiyo.

Mpango huo, unalenga kuwatambua wafugaji ili iwe rahisi kukabiliana na matukio ya wanyama hao kuwashambulia watu kama ambavyo inajitokeza katika baadhi ya mitaa ya Kata ya Makuburi iliyopo wilayani Ubungo.

Katika kata hiyo, jumla ya matukio matatu ya watu kung’atwa na mbwa yamejitokeza kwa nyakati tofauti kiasi cha kuzua hofu na taharuki kwa jamii hasa nyakati za usiku na asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mifugo wa Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam, Archia Mtambo amesema  kuna watu wanafuga mbwa bila kuwa na vibali jambo ambalo haliruhusiwi.

 “Kuna wachache wanafuga mbwa na wavibali lakini waliowengi hawana vibali hivyo, nitumie fursa hii kuwataka waje ofisini kuchukua vibali,” amesema Mtambo.

Katika maelezo yake ofisa huyo amesema mbwa mwenye kichaa anajulikana baada ya kufanyiwa vipimo vya maabara  na  watu wengi hawafahamu hatua za kufuata baada ya kushambuliwa na mbwa wa aina hii.

 “Utaratibu unasema mtu aking’atwa na mbwa cha kwanza anatakiwa kuosha jeraha kisha anatakiwa kumuona ofisa mifugo ndipo anapewa barua ya kwenda hospitali,”amesema.

Mmoja wa walioshambuliwa na mbwa hao, Victoria Lashau ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Muongozo amesema aling’atwa na mbwa mwenye kichaa kwa mujibu wa taarifa ya majibu aliyopewa na  daktari wa Kituo cha Afya Mtaa wa Makuburi.

 “Mara baada ya kung’atwa walinipeleka kituo kidogo cha afya kilichopo karibu na dakatri baada ya kunipima alinipa majibu mbwa mbwa aliyening’ata anakichaa, ndipo aliniparuhusa ya kwenda Hospitali ya Sinza kwa matibabu zaidi na sasa naendelea vizuri,” amesema Lashau

Mjumbe wa Mtaa wa Muongozo, Eva Majanga amethibitisha kupata taarifa ya wananchi kunga’atwa na mbwa na kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa lakini hawakupewa ushirikiano wowote.

“Ripoti nishapeleka kwa mwenyekiti lakini hakuna chochote kinachoendelea hivyo wananchi wanajiandaa kwenda kwa mkuu wa wilaya labda watasaidiwa huko,” amesema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa serikali za mtaa huo, James Ngoitanile amesema hajawahi kupokea taarifa kuhusa matukio ya mbwa kunga’ata watu.

“Sijawahi kupata taarifa kutoka kwa mjumbe kwamba wananchi wake wamekutwa na changamoto kama hiyo na wala kupigiwa simu,”amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!