NewsSWAHILI NEWS

Mbowe ataka Watanzania kuvaa sura ya ujasiri

Moshi/Dar. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka Watanzania kuvaa sura ya ujasiri kupigania hatima ya maisha yao badala ya kuwategemea viongozi wanaojali masilahi yao binafsi.

Mbowe amesema hayo leo Alhamisi, Julai 11, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Soko la Manyema, mjini Moshi katika mwendelezo wa operesheni +255 Kanda ya Kaskazini.

“Watanzania wenzangu tukitegemea miujiza yeyote kwa viongozi waliopo madarakani tumeliwa, kwa sababu tuna viongozi wengi hewa, hawajali shida zetu.

Nchi yetu ina matatizo makubwa mawili, kwanza Watanzania tulio wengi hatuna hasira na maisha yetu na pili kwa muda mrefu tumewaheshimu, kuwaabudu viongozi wanaotutesa katika maisha, lakini chanzo cha mateso yetu hatujui ni kina nani,” amesema.

Mbowe amesema Watanzania ni lazima wabadilike kwa kuwa na hasira na maisha yao, kwa kupinga mambo yasiyokubalika kama wanavyofanya Kenya ili wawe na unafuu wa maisha.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Moshi wakimsikiliza, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe (hayuko pichani) katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika Soko la Manyema lilipo kwenye manispaa hiyo, mkoani Kilimanjaro. Picha na Yesse Tunuka

Katika mkutano huo, Mbowe amehoji wingi wa mashangingi kwenye misafara ya viongozi huku akisema ni anasa na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Msafara wa viongozi una mashangingi 20, 30, 40, bila Watanzania kuvaa sura ya ujasiri maisha yetu yanaendelea kuwa magumu. Serikali inafanya matumizi ya anasa,” amesema Mbowe.

“Ni hivi… kiongozi wa nchi, waziri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya hawajui kulipa kodi ya nyumba, hajui kulipa umeme, analipa kwa kodi yako, maji nyumbani kwake analipiwa, akikaa ofisini analipwa mshahara, akitoka kukagua shule analipwa posho, huyu mpaka vinywaji nyumbani kwake analetewa kama zawadi,” amesema.

Mbowe amesema wakati wananchi wanalia maisha ni magumu, viongozi wao wanaishi kama wapo peponi.

“Hawa watu ukiwaambia wananchi maisha yamebana, hawaelewi kwa sababu wanaishi peponi, wana magari ya bei ambayo hata wafanyabiashara nchi hii hawawezi kununua, wanatembelea wao. Tunasema sawa, mafuta ya magari yao wanawekewa na kodi zetu, madereva wao wanalipwa na kodi zenu, hawa watu ukiwaambia gharama za maisha zimepanda hawaelewi,” amesema Mbowe.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema Tanzania ikipata uongozi unaofikiri vizuri itapiga hatua kutokana na utajiri wa rasilimali zilizopo.

“Mipango yetu mingi haifanikiwi kwa sababu tu hatuna viongozi wanaofikiri vizuri. Mfano sekta ya utalii ingejengewa mikakati dhabiti ilikuwa na uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na Taifa kunufaika,” amesema.

Lema amesema hakuna mbinu nyingine ya kufanya katika kukabiliana na jambo hilo, zaidi ya kuvaa ujasiri kupiga kura kwa wingi na kulinda katika vituo vya kura wizi usifanyike.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kuhusu kushinda chaguzi zijazo katika mkoa wa Kilimanjaro hawana shaka, ni suala la muda tu.

Amesema isingekuwa figusu katika uchaguzi uliopita wa 2020, viti vingi vya udiwani na ubunge walistahili kushikilia wao.

“Pamoja na yote hayo tusiende kinyonge na tusikubali kuendelea kutokea ya mwaka 2020,” amesema.

Mwalimu ambaye ni mwenyekiti wa operesheni ya 255 iliyozinduliwa Kigoma, amesema kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini  imefikisha siku 25 ikianzia Karatu.

“Tunazunguka nchi nzima ili kuondoa ganzi za miaka mitano iliyopita na turudi kwenye mstari wa kufanya siasa kama ilivyokuwa zamani,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!