NewsSWAHILI NEWS

Mbowe akerwa na kodi kwa masikini

Mwanga. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza kukerwa na utitiri wa kodi wanazotozwa wananchi bila kuzingatia uhalisia wa vipato vyao, akisema kinachofanyika ni kuwakandamiza zaidi.

Kwa mujibu wa Mbowe, kanuni sahihi ya utozaji kodi ni kuhakikisha anayelipa ni yule mwenye kipato cha ziada na sio wananchi wote.

Mbowe ameyasema hayo leo, Jumapili Julai 7, 2024 wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.

Amesema ni bahati mbaya wananchi wanatozwa kodi bila wenyewe kujua kwamba wanailipa kupitia maeneo gani, wakidhani walipaji ni wafanyabiashara pekee.

Amesisitiza hatua ya Serikali kuwatoza kodi wananchi wote wakiwemo wenye maisha duni ni kosa, waliopaswa kutozwa ni wale wenye kipato cha ziada.

“Inapaswa kuwatoza wenye vipato vya ziada, sio kumtoza masikini wa kutupwa, unamtoza mtu bila kujali amekula nini,” amesema.

Kwa mujibu wa Mbowe, fedha hizohizo za kodi ndizo zinazotumika kununua magari ya viongozi, akirejea bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ambapo Sh900 bilioni zimetengwa kwa ajili hiyo.

Amesema kila wanachopewa viongozi kutoka serikalini kinatokana na kodi za wananchi, akidokeza ndiyo sababu iliyowafanya Wakenya waandamane.

Amesema wananchi wa taifa hilo, waliandamana kupinga Serikali kupandisha bei ya mkate kupitia ushuru, kadhalika mishahara katika ofisi za wenza wa viongozi.

Mbowe amesema hatua hiyo, imemfanya Rais wa taifa hilo, William Ruto kuacha kutia saini katika muswada wa fedha uliohusisha bajeti na kodi hizo.

“Wananchi wanatambua haki zao. Kwenye bajeti ya Kenya kulipitishwa fedha nyingi za kuwahudumia mke wa Rais, Makamu wa Rais na kununua magari ya viongozi, wananchi wamelalamika Serikali imeondoa,” amesema.

Ameeleza wakati Wakenya wanaandamana kwa sababu hizo, Tanzania imepitishwa bajeti ya Sh900 bilioni kwa ajili ya kununua magari ya viongozi.

“Tumerogwa na nani? Na wala hamshtuki, ninyi wapare watani zangu sijui mnanielewa? Yaani nchi nzima hii viongozi wa Serikali hakuna anayetembea na bodaboda tayari wana magari, lakini mwake huu pekee wanatenga Sh900 bilioni kununulia magari,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, Mbowe amewataka wananchi watafute namna ya kufanya maamuzi yatakayoshinikiza mabadiliko, akiutaja wakati wa uchaguzi.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema aligusia wajibu wa wabunge ni kuwatetea wananchi na sio kuisifia Serikali na mkuu wa nchi.

“Ukishaona mbunge ni mpiga makofi hata Rais akisuka anapiga makofi, hata kiongozi akipaka piko anapiga makofi huyo si mbunge ni boya,” amesema.

Ameonyesha kushangazwa na umasikini unaoendelea nchini kiasi cha baadhi ya watoto kwenda kwenye mkutano huo bila viatu.

Lema amesema changamoto zote za kiuchumi zinazowakabili wananchi zimesababishwa na mwenendo mbovu wa utawala.

Akizungumzia ujenzi wa madarasa unaoendelea nchini, Lema amesema shule si madarasa na madawati, bali ni elimu yenye ubunifu wa kumfanya mtu masikini kupata ufahamu na maarifa ya kuwa na maisha bora.

Amesema wameenda kwenye mkutano katika eneo la Nyumba ya Mungu Wilaya ya Mwanga moja ya changamoto ambazo wananchi wameeleza ni upatikanaji wa maji safi na salama, na amedai wananunua ndoo moja kwa Sh1,000.

Amefafanua kuwa  changamoto nyingine waliyoelezwa ni upungufu wa walimu huku akisema shule yenye wanafunzi 500, ina walimu wanne.

“Tumezunguka leo Mwanga, ukiwa kwenye helikopta unaona mji kwa chini vizuri sana, unaona umasikini wa kupindukia, unaona nyumba za watu.”

“Tumetoka nyumba ya Mungu Kirya, kero ambayo wananchi wamemwambia Mwenyekiti Mbowe (Freeman Mbowe) ni kwamba wananunua maji ndoo Sh1,000, jiwekeni kwenye viatu vyao, yule mvuvi anakwenda kupata samaki au hapati, halafu akitaka kuoga yeye na mke wake na watoto anahitaji kununua maji Sh5,000.”

Aidha amesema, “Shule wanasema ina wanafunzi 500 walimu wanne, tumekwenda pia kule ziwa jipe, wazazi wanasema shule yetu hapa ina walimu wanne, maana yake watoto wenu wanaenda shule kukua.”

Amesema wanahitaji watoto wawe na maarifa, waweze kufikiria na kujua ujasiriamali, haki na biashara ili wakihitimu wasiwe mateka wa ulimwengu, bali wawe watu wenye tija katika ulimwengu.

“Tunataka watoto wetu wawe na maarifa, waweze kufikiria, wajue ujasiriamali, wajue haki, wajue biashara, wakimaliza shule wasiwe mateka wa ulimwengu wawe watu wenye tija katika ulimwengu,” amesema Lema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!