NewsSWAHILI NEWS

Matumizi ya ‘drones’ kupima ardhi yawaibua wadau, watahadharisha

Dar es Salaam. Wananchi na wadau wametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kusimamia kwa weledi kazi kwenye sekta ya ardhi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira, ujenzi holela pamoja na migogoro ya ardhi.

Maoni hayo yametolewa leo Jumapili, Julai 7, 2024 baada ya kutembelea kwenye maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) walipoonyeshwa ndege isiyokuwa na rubani (drone) inayochukua picha za anga na kutoa taarifa za awali.

Mwananchi kutoka Kigamboni, Dar es Salaam, Jabir Aziz amesema kutumika kwa kifaa hicho ni hatua nzuri lakini kikwazo kipo kwenye urasimishaji wa ardhi na kuwa chanzo cha ujenzi holela na migogoro ya ardhi.

“Ni hatua nzuri na itasaidia katika uendelezaji wa miji lakini wakati wa uchukuaji wa taarifa wanazosema wanatakiwa kufuatilia kwa karibu wanaporasimisha matumizi ya ardhi, haitakuwa na maana kama hakuna weledi wa kazi wanazofanya,” amesema Jabir.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Ofisa wa Haki Ardhi, Cathbert Tomitho amesema teknolojia hiyo ni nzuri lakini inafaa kwenye nchi ambazo hazina migogoro ya ardhi kutokana na upangaji wa miji.

“Teknolojia ni nzuri na inafaa kwenye uchukuaji wa picha na taarifa muhimu lakini hapa kwetu tayari kumeshakuwa na migogoro endapo tutatumia kifaa hicho tunatakiwa kushirikisha wananchi na mamlaka za chini, ili kuona ni namna gani wanaweza kupanga miji,” amesema Tomitho.

Ili kukusanya taarifa zilizo sahihi kupitia picha za anga na kusaidia upangaji wa miji na utatuzi wa migogoro ya ardhi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeamua kuanzisha kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Kijiografia (TNGC).

Hayo yameelezwa na Msimamizi wa Utawala TNGC, Isabella Chilumba ambaye amesema lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kuongeza uwezo wa wataalamu nchi, kukidhi mahitaji ya ufundi na ujuzi katika kutoa taarifa za kijiografia kwa kutumia kifaa cha kisasa cha upigaji picha za anga.

“Kituo hiki kimeanzishwa kutokana na pengo la wataalamu waliobobea katika ukusanyaji wa taarifa za kijiografia ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kupanga na kupima ardhi na kudhibiti majanga,” amesema Isabella.

Amesema kituo kitakuwa kitovu cha teknolojia ya kisasa na itasaidia kuhakikisha taarifa zote zinazokusanywa kwa kutumia teknolojia ya upigaji picha za anga kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani (drone).

Amesema katika kuhama kwa kutochukua taarifa zisizo sahihi zenye changamoto nyingi, wameanza kuchukua taarifa za anga katika masuala yote ya upimaji wa awali.

Kituo hicho kitahusika kwenye urushaji wa ndege isiyokuwa na rubani drone ambayo itakuwa inatoa taarifa ya mipaka na majanga yanayojitokeza nchini.

Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2023 kwa kuanza na wataalamu wafundishaji waliopatiwa mafunzo na wataalamu kutoka Korea ambao wamebobea kwenye teknolojia ya upimaji wa ardhi na Julai 2024 wameanza mafunzo rasmi.

Mtaalamu wa kupiga picha za anga, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Siri Mrisho amesema drone hiyo inaruka mita 100 na katika uchukuaji wa picha wanakata kwa mita 16 ili kupata picha yenye ubora zaidi.

Wakala wa uuzaji wa viwanja Kibaha, Honesti Msuya amesema upimaji wa kutumia drone inarahisisha hata kwenye matumizi ya mashine za kupimia viwanja ambapo hiyo itakuwa imetoa ramani sahihi katika maeneo wanayohitaji.

Ofisa Mipango Miji, Taunlus Kitosi amesema kuwepo kwa teknolojia hiyo kutasaidia kwenye upangaji wa miji ambazo ni za lazima kwenye taarifa za awali.

Amesema ndani ya dakika tano wanapata taarifa ya sehemu husika kwa ukubwa na wataalamu wakapata picha na kuweza kupanga miji kwa kuweka alama zinazohitajika.

Pia, amesema inaweza kusaidia katika kutabiri na kukabiliana na majanga kama vile mafuriko, ukame na matetemeko ya ardhi, kwa kutumia data za kijiografia na kuiwezesha Serikali kuandaa mikakati ya kuzuia au kupunguza madhara ya majanga hayo.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!