NewsSWAHILI NEWS

Makonda awaita wenye kesi za ubakaji, ulawiti

Arusha. Matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto na wanawake Mkoa wa Arusha yamemshitua Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda na kuamua kuwaita wadau wenye kesi hizo ofisini kwake ili kuchukua hatua zaidi.

Makonda amewaita watu hao wakiwamo waathirika, asasi pamoja na mashirika yanayoshughulika na kesi hizo kufika ofisini kwake Alhamisi hii ya Julai 11, 2024 kutoa malalamiko ya matukio hayo kwa ajili ya kufuatilia hatma ya upatikanaji wa haki zao.

Ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Julai 8, 2024 kwenye kikao chake na asasi zisizo za kiserikali zisizotengeneza faida zinazoshughulika maendeleo na huduma za jamii.

Lengo la kikao hicho kilichoshirikisha asasi na mashiriki zaidi ya 1200 ni kuangazia shughuli wanazozifanya na changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Miongoni mwa changamoto walizozibainisha ni matukio hayo ya ulawiti na ubakaji kukithiri mkoani humo hususan maeneo ya pembezoni, huku watuhumiwa wa matukio hayo wakiendelea kutamba mitaani.

Miongoni mwa kesi zilizoibuliwa ni kesi ya mwanamke mmoja mkazi wa Wilaya ya Arumeru anayedaiwa kubakwa na kulawitiwa hatimaye kukatwa mkono, lakini hakuna hatua yoyote ya kisheria iliyochukuliwa dhidi ya watekelezaji wa matukio hayo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Farida Halfani amesema mwanamke huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili), alitendewa vitendo hivyo April 4, 2024 na vijana watatu ambao ni wafanyabiashara wenzake.

“Vijana hao bado wapo mitaani wanadunda na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yao zaidi ya mwathirika kuzidi kufilisika kwa kuuza mifugo yake kujitibu na kutimiza mahitaji yake ya kulea watoto wake.Naomba Mkuu wa Mkoa useme jambo mama yule asaidike,” amesema Halfani.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Mimutye, Rose Njilo amesema matukio ya ubakaji na ulawiti ni mengi hususan jamii za pembezoni ambazo hawana sehemu ya kufikisha kilio chao.

“Matukio hayo yamesababisha zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi kushindwa kumaliza shule hasa Wilaya ya Ngorongoro. Chanzo kikuu ni matukio ya mimba za utotoni lakini wahusika hawachukuliwi hatua za kisheria zaidi ya kumalizana nyumbani,” amesema Njilo.

Mkurugenzi wa Husna Foundation, Husna Abubakari amesema Arusha Mjini matukio mengi ya ukatili hasa ubakaji na ulawiti yanashindwa kumalizika kutokana na kesi nyingi hatua za kisheria hazichukuliwi dhidi ya watekelezaji.

Tukio jingine ambalo Husna amelieleza ni la mtoto wa miaka mitatu anayedaiwa kulawitiwa na watoto wenzake, huku baba wa kufikia wa mtoto huyo kutajwa kuhusika.

Husna amesema mama wa mtoto huyo ambaye ni jirani yake anashindwa kuwa mkweli juu ya tukio hilo la mtoto wake wa kiume kuharibika vibaya kutokana na kufanyiwa vitendo vya ulawiti.

“Mheshimiwa mimi ndio nilikuwa wa kwanza kabisa kushughulikia suala hilo baada ya watoto watatu wenye umri wa miaka sita, tisa na 11 kukamatwa mtaani kwetu na kufikishwa kituo cha Polisi Muriet na baadaye nikawachukua mama wa mtoto na mtoto mwenyewe na kwenda kupimwa na kubainika ni kweli ameingiliwa sehemu zake za haja kubwa,” amesema Husna.

Amesema mbali na mtoto kubainika ni kweli ameingiliwa lakini kiasi alichoharibika kulinganisha na maumbile ya watoto waliotuhumiwa kutekeleza ukatili huo ulileta mashaka na kuamua kuanza uchunguzi wa chini chini.

“Katika upelelezi wetu ambao mama wa mtoto ameshindwa kutoa ushirikiano kwa asilimia 100, tulikuja kubaini mwanaume anayeishi naye ndio mhusika wa kwanza wa utekelezaji wa ukatili kwa mtoto huyo na mbaya zaidi amekuwa akimfanyia mtoto huyo pindi anapogombana na mkewe,” amesema Husna.

Wahusika wa tukio hili wametakiwa kufika ofisini kwa Makonda, kesho Jumanne, Julai 9, 2024 ili kuona jinsi ya kulishughulikia.

Hawa ni wachache kati ya wale waliozungumzia matukio hayo kwenye kikao hicho na baada ya hapo, Makonda amesema matukio yamekuwa mengi na kuwataka wadau hao kufika ofisini kwake Alhamisi hii Julai 11, 2024 kuona namna ya kufikia mwafaka wa kutokomeza masuala hayo.

“Njooni siku ya Alhamis ofisini kwangu tusemezane, mtu yoyote aliyefanyiwa ukatili au anayeshughulika na kesi ya ukatili na wahusika wapo tu wanadunda au hujui hata mwenendo wa kesi yako, njoo tuone na tushirikiane tukomeshe tabia hii,” amesema Makonda.

Mbali na hilo, amezitaka taasisi na asasi za kiraia kuja na mpango mikakati na mapendekezo ya jinsi ya kushughulika na kesi hizo ili kutokomeza kesi hizo Arusha.

“Unaweza usione madhara kwa sasa kwa sababu labda mwanao unamlinda sana au anasoma mbali ambako hakuna tabia hizo, lakini jua hawa wanaobaki mitaani unawaangalia ndiyo wanaotegemewa kuja kuwa wake au waume wa watoto wetu.

“Sasa lazima tuweke jamii ya watoto wetu salama ili angalau watoto na wajukuu zetu wapate kizazi chema baadaye,” amesema Makonda.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!