NewsSWAHILI NEWS

Makalla atwishwa kero nne Ilala, awataka watendaji kuzitatua

Dar es Salaam. Kero nne za barabara, ardhi, umeme na huduma za afya zimewasilishwa na wananchi wa Chanika wilayani Ilala, mbele ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla wakiomba kiongozi huyo kuwasaidia kuzitafutia ufumbuzi.

Changamoto hizo zimewasilishwa leo Jumapili Julai 7, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Makalla uliofanyika uwanja wa Chanika City jijini Dar es Salaam. Makalla ameanza ziara ya siku sita katika mkoa wa Dar es Salaam, akianzia wilaya ya Ilala.

Aliyefungua dimba kuelezea kero hizo alikuwa ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dougras Masaburi ambaye ni diwani wa Chanika aliyemweleza Makalla kuwa pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali, lakini bado wanakabiliana na changamoto za barabara katika jimbo la Ukonga.

“Ukitoka Chanika kuelekea Msumbiji barabara haipitiki, ukitoka Masantura hadi kwa Mjeshi barabara hazipitiki, kwa ujumla barabara ni mbovu.

“Mheshimiwa (Makalla) waswahili wana msemo mgeni njoo mwenyeji apone, leo upo hapa naomba tukubebeshe mzigo uweze kutusaidia wananchi wa jiji la Dar es Salaam,”amesema Masaburi.

Ukiachana na Masaburi wananchi wa Chanika waliwasilisha kero zao zilizosomwa hadharani na Makalla aliyekuwa jukwaani akiwahutubia, akiwataja kwa majina mmoja baada ya mwingine na changamoto walizoziandika ili kupatiwa ufumbuzi.

Akisoma kero hizo Makalla alianza kwa kusema, “Zabron Kiboko amesema mpaka wa Kisarawe na Dar es Salaam bado una changamoto, Godwij Mtei amesema umeme hakuna, baadhi ya nyumba zimerukwa, Mbaraka Kipendo amesema barabara za mitaa ni shida. Wakati Anna Bernard ameniandikia wajawazito wanalazimika kutoa fedha ili kupata matibabu kituo cha afya cha Nguvu Kazi Chanika.

Baada ya kusoma kero hizo, Makalla aliwaita watendaji wa jiji la Dar es Salaam, kuzijibu akianza na Mganga Mkuu wa jiji hilo, Dk Zaituni Hamza aliyeahidi kulifanyia kazi kwa kuweka kambi kesho Jumatatu katika hospitali hiyo, akiwa na timu yake.

“Nimesikiliza kero za wananchi, nimeshafanya mawasiliano kesho nitakuwa hapo hospitalini ili kushughulikia,” amesema Dk Hamza.

Kuhusu umeme, meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Chanika, Salum Kagambo amesema katika maeneo yaliyotajwa kuna fedha zimetengwa zitakazokwenda kutekeleza mradi wa kuondoa changamoto.

Wakati Meneja wa  Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura)

jiji la Dar es Salaam, John Magoli amekiri uwepo wa changamoto hiyo, iliyosababisha na mvua zilizonyesha kwa nyakati tofauti katika wilayani humo, lakini Serikali imeshatenga fedha za kuzishughulikia barabara hizo kwa kiwango cha lami.

Kuhusu mgogoro wa mpaka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema analitambua suala hilo na kuahidi kulifanyika na kumpa mrejesho Makalla.

Katika hatua nyingine, Makalla amewataka WanaCCM kukaa mkao wa kula wa kuwapokea wageni mbalimbali watakaojiunga na chama hicho wakitokea vyama vya upinzani.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!