NewsSWAHILI NEWS

Majaliwa: Halmashauri zitumie fedha za ndani kujenga miradi inayoonekana

Mufindi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa moja ya mapungufu ya baadhi ya halmashauri ni kutotumia fedha za ndani kujenga miradi inayoonekana.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumapili Julai 7, 2024, alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya sekondari ya wasichana Iramba iliyoko wilayani Mufindi.

Ujenzi wake utagharimu Sh1.78 bilioni hadi kukamilika kwake huku gharama za ujenzi wa shule hiyo zikihusisha jengo la utawala moja, madarasa manane, ofisi nne, maabara tatu, chumba cha Tehama kimoja, nyumba za walimu tano, bwalo moja la chakula na mabweni manne.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa shule hiyo iliyopo Kijiji cha Iramba, Kata ya Itandula, wilayani Mufindi, mkoani Iringa, Majaliwa amewapongeza madiwani kwa wazo lao la kutenga fedha na kujenga mradi huo.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Iringa kwa ziara ya kikazi ya siku nne, ameitaka Halmashauri ya Mufindi iendelee kubaini vyanzo vitakavyoongeza fedha ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Moja kati ya mapungufu ya baadhi ya Halmashauri ni kutotumia fedha za ndani kujenga miradi inayoonekana, ujenzi wa shule hii ni mfano wa kuigwa na halmashauri zote, ongezeni kasi ya mkamilishe mradi huu kwa wakati,” amesema Majaliwa.

Pia, amewataka watumie vizuri fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ili mradi ulingane na thamani ya fedha iliyotumika.

“Fanyeni mapitio ya fedha mliyopanga kutumia kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu, shilingi milioni 100 ni nyingi kwa nyumba moja,” amesema.

Pia ameagiza madawati yote ambayo hayana eneo la kuweka daftari kwa ajili ya wanafunzi yaondolewe na kurudishwa kwa fundi kwa sababu hayakidhi viwango vya madawati ya shule za msingi na sekondari.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Divisheni ya Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Daniele Mapillya amesema mpaka sasa Sh363.8 milioni zimepokelewa zikijumuisha Sh2.2 milioni zilizotolewa na wananchi na Sh361.6 milioni zimetolewa na halmashauri ya Mufindi.

 Amesema wameanza utaratibu wa kuisajili shule hiyo ili iweze kutumika kama ya kutwa na isaidie kupunguza umbali kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule mama ya Itandula ambayo ina wanafunzi 1,015.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa miundombinu kwenye Hospitali ya Mji wa Mafinga ambao unahusisha wodi ya wagonjwa wa daraja la kwanza, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya wazazi, jengo la wagonjwa mahututi (ICU) na jengo la kufulia ambavyo vyote vitagharimu Sh1.24 bilioni.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!