NewsSWAHILI NEWS

Ma-DC watatu wapata ‘mashangingi’ mapya Mara

Musoma. Wakuu wa wilaya tatu za mkoa wa Mara za Bunda, Rorya na Serengeti wamekabidhiwa magari mapya ili kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwamo usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Magari hayo matatu ni miongoni mwa ‘mashangingi’ sita ambayo Serikali inatarajia kuwapatia wakuu wa wilaya zote sita za Mkoa wa Mara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25, kutokana na kutokuwa na magari baada ya magari yao ya awali kuharibika.

Wakuu wa wilaya hizo wamekabidhiwa magari yao leo Alhamisi Julai 11, 2024 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa magari hayo, wakuu hao wa wilaya wameeleza kwamba magari ni nyenzo muhimu katika kufanikisha utendaji kazi wa kila siku wa viongozi wa Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vincent Mashinji amesema ni vigumu kutimiza wajibu kama kiongozi kama hana usafiri wa uhakika, hivyo suala la kiongozi wa Serikali kuwa na usafiri wa uhakika ni la lazima na si anasa.

“Wanasema mchimba kisima huingia mwenyewe, kwa hiyo ukikosa gari ndiyo utajua umuhimu wa gari na hasa ukiwa kiongozi. Ukiwa kiongozi ukakosa gari utaona namna gani mambo hayaendi,” amesema Dk Mashinji.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema ingawa hakuna kazi iliyosimama wilayani kwake kutokana na gari la ofisi yake kuharibika, lakini zipo changamoto ambazo alikuwa akikutana nazo kutokana na kutokuwa na usafiri wa uhakika.

“Nilikuwa nalazimika kuazima gari kutoka kwenye taasisi za Serikali wilayani pamoja halmashauri, hivyo kazi zilikuwa zinafanyika japo kuna changamoto.

“Mfano, nakumbuka kuna wananchi walipata shida fulani huko vijijini, kwa hiyo nilitakiwa nifike haraka lakini nilifika kwa kuchelewa,” amesema Chikoka.

Chikoka amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi, hivyo ni wajibu wake kuikagua na kusimamia maendeleo ya miradi hiyo na hilo inawezekana kama una usafiri wa uhakika.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema gari hilo litasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi katika wilaya yake.

“Wilaya yangu ina zaidi ya watu 420,000 ambao wanahitaji huduma mbalimbali za kiserikali, mfano kusikilzia kero zao na kusimamia miradi inayotekelezwa na hili linawezekana kama una usafiri wa uhakika,” amesema Dk Naano.

Akizungumza baada ya kukabidhi magari hayo, Evans Mtambi amesema lengo la Serikali kutoa magari kwa wakuu wa wilaya ni kutaka kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati bila kuwepo na kikwazo chochote.

Amesema awali wakuu hao wa wilaya walikuwa na changamoto ya usafiri, hali iliyokwamisha utekelezaji wa majukumu yao kwa haraka, hivyo anaamini kupatikana kwa magari kutachochea kasi ya usimamizi wa miradi na utatuzi wa kero za wananchi kwa muda mwafaka.

Akiwasilisha bajti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema Serikali itafumia Sh190.57 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa na wilaya kwa mwaka 2024/2025.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!