NewsSWAHILI NEWS

Lema ataja chanzo cha umaskini kwa wakulima

Same. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kukosekana kwa sera nzuri za kilimo na uchumi nchini kumesababisha wakulima wengi washindwe kufanikiwa kupitia kilimo.

Amesema hatua hiyo pia imesababisha kuwepo kwa kundi kubwa la vijana mitaani ambao hawana ajira, licha ya baba na mama zao kuwa na mashamba makubwa yanayofaa kwa kilimo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho leo Julai 6, 2024 kwenye operesheni +255 Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Lema amesema uchumi ni ubunifu na kungekuwa na sera nzuri za kiuchumi, tatizo la  ajira lisingekuwa kubwa kama ilivyo sasa.

“Kinachofanya wakulima wengi nchi hii wasifanikiwe, kwamba leo unaona vijana wengi barabarani lakini mama zao na baba zao wana mashamba makubwa, ni kwa sababu hatuna sera nzuri za uchumi zenye mkakati wa mikopo ya kifedha ambayo inaweza kumuondoa kila mtu kutoka katika umaskini.

Amesema kungekuwa na sera nzuri za kilimo, wakulima wangeweza kunufaika kupitia kilimo na kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Lema ametumia pia nafasi hiyo kuwataka wanachama na viongozi wa chama hicho kujipanga vizuri katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuhakikisha hakuna mwenyekiti wa kitongoni wala kijiji kutoka CCM ambaye atashinda.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura ili kuwa na sifa ya kushiriki katika uchaguzi na kuwachagua viongozi wanaowataka.

Mbowe amesema katika uchaguzi mkuu mwakani, asilimia 65 ya wapiga kura watakuwa ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 35 hivyo ni jukumu la vijana wote wenye sifa wakajiandikishe ili kushiriki kufanya mageuzi.

“Julai 20, mwaka huu, hatua ya  kuandikisha wapigakura katika daftari la kudumu la mpiga kura itaanza, hakikisheni wote mnajiandikisha na kwa taarifa, uchaguzi wa mwakani asilimia 65 ya wapigakura watakuwa ni vijana wenye umri chini ya miaka 35.”

“Vijana ndio watakaoamua uchaguzi wa mwakani uweje na siyo wazee, vijana ndio watakuwa na maamuzi kwa sababu ndiyo wengi, hivyo tunaomba wote mkajiandikishe na wale ambao mlishajiandikisha mkahakiki taarifa zenu na kuhakikisha shahada zenu ziko salama ili mwakani muweze kufanya mageuzi,” amesema.

Mbowe amesema Wilaya ya Same ni moja ya zilikuwepo tangu ukoloni ikijulikana kama Wilaya ya Pare, lakini jambo la kushangaza katika eneo hilo, biashara kubwa ni maji ya kunywa kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo.

“Same ni wilaya ya kihistoria, ilikuwepo toka ukoloni ikiitwa Wilaya ya Pare, eti leo ukija Same biashara kubwa ni maji ya kunywa kwa sababu hakuna maji ya bomba, leo watu wanafikiri biashara ni kusambaza maji ya kunywa badala ya kusambaza viwanda. Wananchi wananunua maji kwa bei mbaya wakati maisha ni magumu,”amesema Mbowe.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!