NewsSWAHILI NEWS

Kwa mara ya kwanza Katavi kuungwa na gridi ya Taifa kuanzia Oktoba 2024

Katavi. Imeelezwa tangu Tanzania ilipopata Uhuru mwaka 1961, eneo lote la Mkoa wa Katavi halijawahi kufikiwa na umeme wa gridi ya taifa jambo ambalo linafanya mkoa huo kuwa nyuma kimaendeleo.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Julai 9, 2024 mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Njia Kuu ya kusafirisha umeme Msongo wa KV 132 kutoka Tabora hadi Katavi na Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme kilichoko Mpanda.

Kutokana na hilo, Dk iteko amesema Mkoa wa Katavi sasa unatarajiwa kuingizwa katika matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa ifikapo Septemba, 2024 baada ya kuikosa huduma hiyo kwa zaidi ya miaka hiyo 60 ya Uhuru.

Amesema kitendo cha kutokuwa katika Gridi ya Taifa kimeunyima mkoa huo fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanya uzalishaji wa uhakika na tatizo hilo limedumu kwa miongo kadhaa.

“Nawashukuru wananchi kwa imani mliyoonesha na kuhakikisha miradi inajengwa na inamalizika kama ilivyo katika ujenzi wa mradi huu, natarajia mradi huu utakamilika Septemba, mwaka huu na nimetoa hadi Oktoba ili kutoa mwanya kama kuna dharura inayoweza kutokea,” amesema Dk Biteko.

Amesema kwa sasa hakuna tena visingizio kwa nini wananchi wasipate umeme wa uhakika ijapokuwa Serikali inatoa kipaumbele katika huduma mbalimbali za jamii.

Kwa sasa wakazi wa mkoa huo wanatumia jenereta kuzalisha umeme unaosambazwa kwenye makazi ya watu na hata maeneo ya uwekezaji.

Hivyo, inaelezwa kukamilika kwa ujenzi wa njia hiyo na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Mpanda, kitasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya Mkoa huo kwa sababu umeme wa uhakika utapatikana, amesema John Siwale mfanyabiashara wa mkoani Katavi.

Awali akitoa maelezo mbele ya Dk Biteko, Meneja wa Mradi, Sospeter Oralo amesema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 97 na ujenzi wa laini umekamilika kwa asilimia 63.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mridoko amesema wananchi wa vijiji vyote 172 na maeneo ya ziada 114, wanatamani kupata umeme wa uhakika na kuondokana na mgawo wa umeme jambo litakalowawezesha kuzalisha bidhaa mbalimbali katika kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Mrindoko ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma na kuridhia ujenzi wa kituo kwa ajili ya kupokea, kupoza na kusafirisha umeme wa uhakika ambao uko mbioni kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa huo, Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi amepongeza juhudi za serikali za kupeleka umeme wa uhakika kwa wananchi ili watumie kujiletea maendeleo.

Ameiomba serikali kupitia mpango wa kupeleka umeme wa gridi kwa mikoa ya pembezoni, kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuboresha na kuanzisha matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu Biteko amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki na kumsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kufanya ziara Mkoani Katavi hivi karibuni.

“Niwatake mjitokeze kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Rais wetu, Samia ambaye anatarajia kufanya ziara hapa mkoani,” amesema Dk Biteko.

Amesema Rais Samia ni kinara wa utatuzi wa changamoto za wananchi, ana imani akifika mkoani humo, atasaidia utatuzi wa mkwamo wa baadhi ya mambo yanayoukabili mkoa huo.

Katabi James, mkazi wa Kampani Manispaa ya Mpanda, amesema, “Tutafurahi mradi huu ukianza kufanya kazi kwani utatunufaisha sana maana kwa sasa tunashida kubwa ya umeme kukatakata na hauna nguvu, kitu ambacho kinatufanya kushindwa kupata maendeleo kwa haraka.”

Naye Jazila Jumanne, mkazi wa Manispaa ya Mpanda, ameiomba Tanesco ihakikishe huduma bora za umeme zinatolewa mkoani humo muda wote.

Amesema hali ya upatikanaji wa umeme hairidhishi, hali inayowapa wakati mgumu.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!