NewsSWAHILI NEWS

Kuonana na nabii mbinde, malipo yake mamilioni-2

Dar es Salaam. “Kama una Sh500,000 nenda pale kaandikishe jina lako uende kumuona nabii.”

Hii ni kauli ya mhudumu wa kanisa mojawapo la maombezi, akiwatangazia waumini, ikiwa ni sehemu ya kile ambacho Mwananchi limebaini katika mfululizo wa uchunguzi wake kuhusu waumini wa makanisa hayo wanavyokamuliwa mamilioni ya shilingi na viongozi wa dini ili waombewe au kubarikiwa.

Katika sehemu ya kwanza jana, tulibainisha jinsi baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam yanavyowafukarisha waumini kwa kuwatoza fedha nyingi kwa ununuzi wa maji, mafuta, au vitambaa, huku wengine wakilazimika kuuza mali zao.

Leo tunaangazia jinsi ilivyo vigumu na aghali kuwafikia manabii na mitume wa makanisa hayo, zikihitajika fedha nyingi kati ya Sh500,000 hadi Sh1.5 milioni na wakati mwingine hata zaidi ya hapo, huku ikielezwa kuwepo ushuhuda wa kuandaliwa ili kuuhadaa umma.

Katika moja ya makanisa ambayo Mwananchi limeyatembelea wilayani Temeke, ili uonane na kiongozi wa kanisa hilo, sharti utoe ada ya Sh500,000, bila kuhesabu sadaka nyingine wanazotozwa waumini.

Mchungaji huyo hurusha matangazo kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kuhusu huduma zake, jambo ambalo limemvutia umati mkubwa wa waumini kusali kanisani hapo kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

Mwandishi wa Mwananchi alihudhuria baadhi ya ibada katika kanisa hilo, zikiwemo siku za Jumapili ambapo ibada huanza saa 1:00 asubuhi. Waumini hufika kanisani mapema asubuhi kusubiri uponyaji na unabii.

Kiongozi huyo mwenye walinzi wengi, aliingia kanisani saa 3 asubuhi akiwa kwenye msafara wa magari manne ya kifahari yaliyoandikwa jina lake.

Umati wa watu uliokuwa umefurika kanisani ulitoka kumlaki mtumishi huyo wa Mungu ambaye alishuka kutoka kwenye gari lake akiwa na walinzi sita. Moja kwa moja alielekea madhabahuni na kuanza ibada, ambapo baadhi ya waumini, hasa wanawake, walianza kupiga kelele na kugalagala wakidaiwa kuwa na mapepo na walitolewa nje.

Ndani ya ibada, mhudumu wa kanisa hilo alitangaza kuwa anayetaka kumuona mtumishi na kuombewa anatakiwa kutoa Sh500,000 ili atabiriwe na kupata uponyaji.

“Kama una Sh500,000 nenda pale kaandikishe jina lako uende kumuona nabii,” alisema msaidizi huyo.

Pia, alisema hadi saa nane mchana mtumishi alitangaza kila mtu awe amenunua maji yanayouzwa Sh2,000 ambayo yangeombewa, agizo ambalo waumini wengi walilitekeleza.

Kana kwamba haitoshi, waumini hao walitangaziwa kutoa sadaka yenye alama ya namba tatu, ikimaanisha Sh30,000, ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kufungua uchumi wa waumini hao.

Baada ya tangazo hilo, baadhi ya waumini walikimbilia bahasha zilizokuwa zikitolewa na mtumishi mwenyewe. Awamu iliyofuata, waliitwa wale kutoa Sh3,000, kima ambacho kilinyanyua wengi zaidi, na awamu ya mwisho ilihusisha kila mwenye kiasi chochote hata Sh100.

Baada ya kila mtu kutoa ‘alichonacho’, mtumishi huyo alitangaza ataonana na watu watatu tu waliotoa ada ya fomu ya Sh500, 000 na alifanya hivyo kwenye chumba maalumu baada ya kuhitimisha ibada.

Kutokana na umati mkubwa uliojaa karibu na chumba hicho, msaidizi wa mtumishi huyo alitoka na kutangaza kuwa wale tu walio na Sh500,000 ndio wangemuona mtumishi siku hiyo na kuwa wengine waliotoa pungufu wangeonana naye siku inayofuata.

Kila mtu aliyekuwa pale alijiandaa kuonana na mtumishi kwa viwango tofauti, wakidai Sh500, 000 ni nyingi. Wengine waliambatana na wagonjwa.

“Nipo hapa tangu jana nimelala hapa, tayari nimelipa Sh50,000 niliambiwa ningemuona leo, lakini leo naambiwa niongeze hela. Hii niliyotoa niliikopa na hapa nina nauli peke yake,” alisema Upendo Ngowi, mkazi wa Pwani, alipokuwa akiwabembeleza walinzi wa ‘mtumishi wa Mungu’.

Madai ya Upendo ni kuwa siku hiyo alikuwa amebakiwa na Sh10,000 za nauli ya kurudi nyumbani.

Jumapili aliambiwa aongeze fedha na arudi Jumatatu akiwa na walau Sh300,000, ili apate fomu ya kumuona mtumishi.

Hata hivyo, alishindwa na akawa anadai arejeshewe fedha zake akisema siku inayofuata asingeweza kuhudhuria ibada kwa kuwa anatokea mbali. Hata hivyo, fedha zake hazikurejeshwa.

Martha Urassa, mkazi wa Kimara ambaye anasumbuliwa na uvimbe kwenye titi, alisema amekuwa akihangaika kupata fursa ya maombi bila mafanikio.

“Niliambiwa nilipe hela ndio nionane na mtumishi, nimelipa Sh35,000 na bado sijamuona, naambiwa nikiwa na Sh500,000 ndio rahisi kumuona, huu umasikini ni mbaya sana,” alisema.

Kwa Suguye kwatajwa, afafanua

Katika Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM), mmoja wa wahudumu ambaye hakutaka kutaja jina lake alieleza utaratibu wa kumuona Nabii Nicolaus Suguye katika siku za Jumatatu, Jumanne au Jumatano nako ni lazima uende na picha moja kwa ajili ya usajili, kisha mengine yatafuata.

Ukishaandikishwa na kusajiliwa, alisema pale utakapoonana na nabii huyo utatakiwa uwe na sadaka kuanzia Sh150,000 hadi Sh350,000 kwa ajili ya kuombewa.

“Wale waliosajiliwa kuna viti vyao kabisa kwa ajili ya kuonana ana kwa ana na Suguye na unapoonana naye lazima uwe na hela ya sadaka kuanzia Sh150,000 hadi Sh350,000 na ukishatoa fedha hizo utapatiwa mafuta, stika, maji na kitambaa,” alisema.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 17 ya kanisa hilo, Suguye alikanusha kuwatoza fedha waumini wake.

“Hatutozi fedha katika kanisa kuombea watu, hata ukiwatafuta wanaokuja kujisajili mpaka sasa hakuna chochote na maombezi yangu ni bure na nayaendesha kwa kuwawekea mikono na baada ya hapo watu wanaondoka,” alifafanua Suguye baada ya kuulizwa.

Wakati Suguye akisema hayo, muumini wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Amina Salehe alidai yeye ana zaidi ya miaka mitatu anaabudu katika Kanisa la WRM na alitamani siku moja na yeye aguswe na nabii huyo lakini kutokana na kipato chake kuwa kidogo anashiriki kwenye ibada ya Jumapili pekee.

“Natamani na mimi nikutane na Nabii Suguye nifanyiwe maombi ya peke yangu, lakini kumuona ni gharama, kumuona kuanzia Sh150,000 na kuendelea, ila mimi nilienda kumuona nikiwa na Sh50,000, nilipofika kwa mtenda kazi (mhudumu) niliambiwa hela yangu ni ndogo,” alisema muumini huyo.

Mwandishi wetu aliyepiga kambi katika kanisa mojawapo lililopo Kimara, Dar es Salaam, aliambiwa ili kuonana na kiongozi wa kanisa hilo sharti alipe Sh1.5 milioni.

Mwandishi aliambiwa ajaze fomu inayoitwa jina ‘nguzo ya ujenzi’ ambayo alitakiwa kuilipia Sh1.5 milioni.

“Ukitoa hiyo sadaka, unamuona mapema sana, lakini hivihivi, itakulazimu usubiri foleni na ni kubwa mno,” alisema mtendaji ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akifafanua zaidi, mtenda kazi huyo alisema: “Kadi ya nguzo ni Sh1.5 milioni ambayo ukimaliza kuilipia inagongwa muhuri na baba mwenyewe (anamtaja jina) kisha unapewa nafasi ya kwenda kuonana naye moja kwa moja ofisini kwake, unamweleza matatizo yako,” alisema.

Alisema kadi hizo anazitoa mwenyewe (nabii) pale madhabahuni na zinaweza kulipiwa kidogo kidogo hadi mtu amalize.

“Ukimaliza kuilipia Kadi ya Nguzo hausubiri foleni, hiyo ni ‘fasta’ tu, gharama ya awali ya kuipata hiyo kadi ni Sh10, 000, kama unailipia kidogo kidogo, kila unapolipa sadaka yako inaandikwa hadi ukimaliza baba mwenyewe anaigonga muhuri, unapata kibali cha kwenda kumuona moja kwa moja,” alisema.

Katika uchunguzi wa makanisa hayo kumebainika udanganyifu na uwepo miujiza ya uongo inayoenea kwa kasi nchini Tanzania, ambapo watu binafsi wanatumiwa kutunga miujiza na ushuhuda kwa lengo la kuuaminisha umma.

Hii inahusisha kundi la watu, mara nyingi kutoka nje ya nchi, wanaodai kuteseka na maradhi sugu kama saratani na kisukari.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao wana ulemavu bandia kama wa kutokusikia na upofu.

Timoth (si jina halisi), mshiriki wa zamani kwenye moja ya makanisa, anaeleza kuwa huwa wanatoka nje ya eneo la ibada ili kuepuka kutambuliwa na kueleza tatizo fulani.

Baada ya miezi kadhaa, wanarudi wakidai wameponywa kimiujiza, jambo linaloshawishi wafuasi kuweka imani na fedha zao katika madhabahu hizo. Timoth anasema wachungaji huweka mazingira waumini kushindwa kufikiri kwa makini na kuwataka wajitenge na wapinzani.

Hata Beatrice (pia si jina halisi) anaeleza wameandaliwa kujifanya wameponywa wakati wa ibada na kupiga simu kupitia redio ay TV ambapo ‘mtu wa Mungu’ anatoa unabii.

Hali hii nchini inatia wasiwasi, ingawa haijafikia viwango vya Kenya na Afrika Kusini. Wachungaji hufikia hatua ya kutumia nguvu zisizo za kawaida kutoka Nigeria ili kuwavuta waumini.

Itaendelea toleo lijalo, tukiangazia vifaa mbalimbali wanavyonunua waumini ka uponyaji na miujiza. 

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!