NewsSWAHILI NEWS

Kukosekana kwa maandishi ya DPP kwamuacha huru aliyehukumiwa miaka 20 jela

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu iliyomtia hatiani Kelvin Kimbila kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na vipande 15 vya nyama ya ngiri.

Hiyo ni baada ya kubainika kuwa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ya msingi, haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi.

Kelvin alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Mbarali, katika kesi ya Uhujumu Uchumi iliyokuwa inamkabili.

Katika kesi hiyo, Kelvin alishtakiwa kwa kosa la kukutwa na vipande 15 vya nyama ya Ngiri kinyume na kifungu cha 86 (10 (2) (b) na (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.

Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 14 (d) jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200 (EOCCA).

Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama aliposomewa shtaka, Kelvin alikiri kutenda kosa hilo hivyo Mahakama ya Wilaya ya Mbarali ilimtia hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo.

Hata hivyo, baadaye alikata rufaa ya kwanza Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, iliyosomeka rufaa ya jinai namba 94/ 2021, kupinga hukumu hiyo.

Lakini Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilioutoa Desemba 22, 2021 ikizingatia kifungu cha 360 (1)) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinachokataza rufaa dhidi ya hukumu zilizotolewa baada ya mtu kukiri kosa,  iliitupilia mbali rufaa hiyo.

Hata hivyo hakuridhika na akakata rufaa ya pili kwenye Mahakama ya Rufani, rufaa namba 71/2021 akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Mahakama ya Rufani katika hukumu yake imeridhika kuwa Mahakama ya Wilaya ya Mbarali iliyomtia hatiani mrufani Kelvin na kumhukumu adhabu hiyo, haikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Kwa kawaida kesi za uhujumu uchumi husikilizwa na kuamuriwa na Mahakama Kuu pekee kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka hayo kisheria.

Lakini Mahakama za chini (Mahakama ya Wilaya na za Hakimu Mkazi) zinaweza kusikiliza na kuamua kesi hizo kwa ridhaa ya maandishi na cheti kutoka kwa DPP ikizipa mamlaka hayo.

Katika kesi hii, Mahakama ya Rufani imebaini kuwa ingawa kumbukumbu za kesi hiyo zinataja kuwepo kwa ridhaa hiyo ya DPP, lakini hakuna ushahidi kuthibitisha kuwa mahakama hiyo ilipokea ridhaa hiyo kutoka kwa DPP kabla ya kukaa kuisikiliza na kutoa uamua juu ya kesi hiyo.

Hivyo kutokana na kasoro hiyo, Mahakama ya Rufani imesema mwenendo wote na hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Mbarali iliyomtia hatiani Kelvin na mwenendo na hukumu ya rufaa wa Mahakama Kuu iliyokubaliana na hukumu ya Mahakama ya Wilaya Mbarali, ni batili.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumatatu Julai 8, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na mwenyekiti wake, Jaji Barke Sehel, Ignas Kitusi na Issa Maige, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo.

Katika hukumu hiyo, majaji hao wakinukuu moja ya aya kutoka kwenye rufaa ya jinai namba 319/2029, Ismail Ndone dhidi ya Jamhuri, inasema kuwa:

“… Ridhaa na cheti kilichotiwa saini tarehe 10 Aprili, 2018 havikupokelewa rasmi na mahakama ya mwanzo hivyo, kwa kukosekana kwa ridhaa na cheti cha DPP, mahakama ya awali ilikosa mamlaka ya kusikiliza kesi hii inayoendesha mwenendo mzima wa kesi ubatili.”

Jaji Kitusi anasema wanakubali wasilisho la Wakili Mwita kuwa kutokupokea kibali na cheti kinachotoa mamlaka kwa mahakama ya awali, kunafanya mwenendo wote wa kesi ya msingi na wa rufaa ya kwanza kuwa batili. 

Amesema mahakama hiyo imetumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa kubatilisha Mwenendo wa shauri zima la mahakama ya awali na Mahakama Kuu.

Jaji Kitusi amesema mahakama hiyo imetoa muda usiozidi miezi 18 kwa DPP, endapo atakuwa na nia ya kumshtaki tena mrufani huyo, kutekeleza hilo ndani ya muda huo wa miezi 18.

“Tumetafakari kuhusu swali kama tunapaswa kuagiza kusikilizwa upya kwa mujibu wa sheria, au la, tumeona agizo kama hilo litapingana na haki ya kesi hii, badala yake  tunakubaliana na Mwita tumwachie mrufani na kuliacha suala hilo kwa DPP kuamua kushtaki tena au la,” amesema Jaji Kitusi na kusisitiza:

“Tutafanya vivyo hivyo lakini kwa masharti kwamba uamuzi huo wa DPP lazima uchukuliwe si zaidi ya miezi 18 tangu tarehe ya kutolewa kwa hukumu hii, kwa hiyo, tunaamuru kuachiliwa kwa mrufani mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.”

Jaji Kitusi amesema; “Mahakama hiyo baada ya kuamua hivyo, inadhani hoja hiyo ambayo imechangiwa vyema na Wakili Mwita inatosha kuondoa shauri hilo, hivyo hawahitaji kushughulikia sababu za rufaa.”

Katika rufaa hiyo ya pili aliyoikata Mahakama ya Rufani, Kelvi, alibainisha jumla ya sababu 10 za rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyokubaliana na hatia na adhabu aliyohukumiwa na Mahakama ya chini, wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo hakuweza kuzielezea hata moja.

Hata hivyo, hoja hiyo iliungwa mkono na wakili wa mjibu rufani (Jamhuri), aliyedai hakukuwa na ushahidi unaonyesha kwamba ridhaa na cheti cha DPP iliipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ilipokelewa na mahakama hiyo kabla ya kuanza kusikiliza.

Wakili huyo alirejea kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga kuwa ni Mahakama Kuu pekee iliyopewa mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhujumu uchumi.

Alieleza kuwa mahakama nyingine za chini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hutoa ridhaa ya maandishi chini ya kifungu cha 26 cha Sheria hiyo.

Amesema katika kesi hiyo, ridhaa ya DPP ilidaiwa kuwepo ila hakukuwa na ushahidi kwamba ilipokelewa na mahakama hiyo kabla ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo.

Katika kutoa uzito wa hoja yake, Wakili wa mjibu rufani aliirejesha Mahakama katika rufaa namba 35/2020 ya Aloyce Joseph dhidi ya Jamhuri na rufaa ya jinai namba 632/202o ya Joseph Ngadupa na mwenzake dhidi ya Jamhuri, kwamba ridhaa au cheti ambacho hakijaidhinishwa ni sawa na hakipo.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!