NewsSWAHILI NEWS

Kibano kwa vituo holela vya massage ‘uswahilini’

Dar es Salaam. Wakati vituo vya kusinga mwili vikiendelea kuanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali inakusudia kusimamia ipasavyo sheria inayowataka kujisajili na kuwa na wahudumu waliosomea lasivyo watakumbana na faini isiyopungua Sh500,000, jela miaka miwili au vyote kwa pamoja.

 Mbali na hilo, Serikali imebaini wahudumu wengi wanaofanya shughuli hizo maeneo mbalimbali nchini hawana sifa ya kutoa huduma hizo kwa sababu hawajasomea.

 Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Msajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Martin Magogwa amesema wanafahamu yapo maeneo ya kutolea huduma hizo zilizosajiliwa na yanatoa huduma kwa mujibu wa sheria na yapo pia ambayo  hayajasajiliwa.

Kauli hii imekuja ikiwa ni baada ya kuwapo kwa matamko mbalimbali yaliyotolewa na viongozi ambayo baadhi yanaonyesha kuwa vituo hivyo vimegeuzwa madanguro.

Magogwa anasema kwa miaka minne sasa wamekuwa wakisajili vituo hivyo  ili kuhakikisha maeneo yote yanasajiliwa kwa mujibu wa sheria wanafanya kazi kwa kushirikiana na waratibu wa mikoa na halmashauri ili kusimamia utoaji wa huduma zote tiba asili na mbadala.

“Nyingine zinaibuka kila leo (maeneo ya kusinga), kutokana na changamoto uhaba wa vitendea kazi na watumishi huwezi kuwa unashughulikia changamoto zinazotokea kila siku,” amesema Magogwa

“….lakini mipango ya kushughulikia ambao hawajajisajili ipo kwani sheria inasema atatozwa faini ya Sh500,000, kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja na ni kosa kufanya huduma hizo bila kusajiliwa.

Kwa mujibu wa Magogwa katika mwaka ulioishia Juni 2024, walifanya ukaguzi kwa maeneo yanayotoa huduma hizo zaidi ya 50 na katika hizo baadhi walikuwa wamesajiliwa na wengine hawajasajiliwa na baada ya kuonyeshwa kuwa wanaendesha shughuli kinyume na taratibu baadhi walijisajili.

“Wengi wao walisajiliwa, wengine bado hawajakamilisha kulipa, hivyo mipango yote tuliyonayo ni kuhakikisha huduma zote za tiba asili na mbadala zinarasimishwa kwa wanaozitoa kujisajili ili waweze kuzingatia miiko na maadili ya huduma zao,” amesema Magogwa.

Amesema huduma ya kusinga watu ni tiba mbadala ambayo mtu anapaswa kuwa amesomea fani hiyo na si kutoa huduma bila kuwa na sifa yoyote.

“Ni fani ya kusomea, siyo fani ya kufanyia mazoezi, lazima uwe umesomea kutoka katika vyuo vinavyotambuliwa na serikali, ukifuzu masomo katika fani ya usingaji, ukapewa cheti ni sifa ya kwanza ya kusajiliwa kama mtoa huduma,” amesema Magogwa.

Kwa sasa Tanzania hakuna chuo kinachotoa mafunzo hayo licha ya uwepo wa kozi mbalimbali zinatolewa na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi stadi (Veta) huku akibainisha kuwa wapo katika mkakati wa kushirikiana na chuo hicho ili kuangalia namna ya kuwasaidia kupata mafunzo ili wawe na vyeti.

Hali hiyo imefanya kwa sasa maeneo mengi yanayotoa huduma hiyo yanatumia watu ambao hawajasoma na hawana sifa ya kutoa huduma jambo ambalo linafanya wasisajiliwe

“Kwa sababu tunajua hii ni sehemu ya watu wengi wasiokuwa na ajira kujipatia kipato, tunaangalia namna ya kuwapa ujuzi kupitia chuo kinachotambuliwa ili wasajiliwe. Athari ya hii ni kama muuguzi au daktari ambaye hajaenda shuleni kutibu mgonjwa,” amesema Magogwa.

Taratibu za kufungua kituo cha kusinga

Ili mtu afungue kituo cha usingaji viungo ni lazima apewe barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa anapoishi, muhtasari wa kikao wa serikali za mitaa sehemu ambayo huduma zinapotolewa.

“Hatuwezi kumsajili hivi hivi, mdhamini wake ni serikali za mitaa anapoishi, ndiyo vigezo vya kusajiliwa na ada ya kulipia ni Sh100,000 kwa mwaka,” amesema Magogwa.

Akizungumza na Mwananchi, Mmoja wa wamiliki wa maeneo hayo ambaye hakutaka jina lake kutajwa amesema licha ya kutokuwa na vyeti kutoka vyuo vinavyotambulika na Serikali lakini huwafundisha watoa huduma wake.

“Tunawapa mafunzo ya mwezi mzima, namna wanavyoweza kuhudumia wateja katika namna inayofaa, vitu gani vya kuepuka na miiko ya kazi tunawapatia,” amesema mmiliki huyo.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!