NewsSWAHILI NEWS

Kibano daladala zinazokatisha njia mbioni

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) imeanza safari ya kutafuta suluhu ya mabasi ya abiria madogo ‘daladala’ nchini nzima yenye tabia ya kukatisha safari kwa kuanzisha Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTD).

Kuanzishwa kwa mfumo huo ni baada ya kuonyesha mafanikio kwa mabasi ya mikoani ambayo yamefungwa ikiwemo kupunguza mwendokasi wa mabasi.

Mkurugenzi wa Barabara na Uchukuzi wa Latra, Johansen Kahatano ameliambia gazeti dada la The Citizen kuwa ufungaji wa VTD unalenga kuboresha ufanisi na uaminifu wa usafiri wa umma kwa manufaa na usalama wa abiria kwa ujumla na utaratibu wa mifumo ya usafiri wa mijini.

“Kanuni za Leseni za Usafiri (Public Service Vehicles), 2020 zinataka mabasi yanayofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya nchi hii yawekwe VTD,” amesema.

Amesema ni katika kutekeleza kanuni hizo ndipo Latra imeanza na mabasi yaendayo mikoani ambayo sasa yanafanya kazi kwa ufanisi.

“Sasa tunaanza kufunga VTD katika mabasi ya abiria (daladala),” amesema.

Kwa sasa Latra inashirikisha na wadau mbalimbali wakiwemo waendesha mabasi kupitia vyama vyao na watu binafsi, huku akisema uwekaji wa VTD utarahisisha kuunganisha mabasi ya abiria na Mfumo wa Kufuatilia Magari wa Latra (VTS).

Amesema mfumo huo utaiwezesha Latra kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ikiwemo ya ucheleweshaji wa daladala na kuwatambua baadhi ya watu wenye leseni lakini hawatoi huduma.

“Hali hii inafanya kuwa na changamoto za kutokuwapo kwa uwiano wa upatikanaji wa vyombo vya usafiri na baadhi ya madereva na makondakta wa mabasi kushindwa kufika sehemu zinazotakiwa,” amesema Kahatano.

Alibainisha nyakati za jioni, baadhi ya madereva huwa wanakatisha safari kabla ya kufika mwisho.

“Hii ni moja ya changamoto kubwa ambayo Latra inakabiliana nayo katika uendeshaji wa shughuli zake hasa miji mikubwa ikiwemo Dar es Salaam,” amesema Kahatano.

Ufungaji wa VTD utarahisisha uendeshaji bora wa daladala na hata kuonyesha baadhi ya ushahidi wa maandishi juu ya kile kilichotokea wakati wa utoaji wa huduma.

“Tuna matumaini kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutaanza ufungaji wa VTD kwa mabasi ya abiria. Kwa hiyo, sasa tuko katika awamu ya kuwashirikisha wadau na kupata maoni ya namna bora ya utekelezaji,” amesema.

Kwa upande wa Katibu wa Umoja wa wamiliki wa Daladala (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema ni mapema sana kusema lolote.

Akizungumzia suala hilo, Mkazi wa Segerea jijini Dar es salaam, Anna Mugala amepongeza hatua hiyo akisema itasaidia Watanzania kurejea nyumbani mapema.

Mugala ambaye anafanya kazi katika moja ya maduka ya Mlimani City amesema madereva wana tabia ya kutumia njia za mkato hasa nyakati za jioni na usiku.

Anachokisema Mugala ni sawa na Mary Andrew, Mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza anayesema: “Hii tabia ya daladala kukatisha ruti inakera sana, sasa kama huo mfumo utaweza kudhibiti itasaidia.”

Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Latra (Latra CCC), Daud Daudi amesema mfumo huo utaleta matokeo chanya kwa wamiliki wa daladala kwa sababu wataweza pia kufuatilia magari yao.

VTD pia itabadilisha tabia za madereva, na hivyo kuongeza thamani ya usafiri.

“Madereva wanapokuwa hawazingatii kanuni za Latra na kufanya u-turn inakuwa vigumu kuhalalisha kama ni kweli au la isipokuwa mtu atashuhudia tukio hilo,” amesema.

Amesema kilicho muhimu ni hitaji la kila mdau kukubali mabadiliko yanayokuja na VTD.

“Pia tunahimiza Latra kuendelea kuja na mifumo ya habari kwa ajili ya usalama wa abiria,” amesema.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!