NewsSWAHILI NEWS

KESI YA UKAHABA: Mfamasia akiri kufanya ukahaba, alimwa faini

Dar es Salaam. Mahakamani hakukosi vituko. Unaweza kusema hivyo, baada ya binti wa miaka 23, Lobi Daudi kukiri shtaka lake la kufanya vitendo vya ukahaba, huku akisisitiza kibarua chake katika dula la dawa lililopo Mbezi, kitaota nyasi.

Lobi ambaye ametambulishwa kama mfamasi na mkazi wa Ubungo, jijini Dar es Salaam ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Francis Mhina, wakati kesi yake na wenzake, ilipoitwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali (PH).

Mshtakiwa huyo, ambaye anajitetea mwenyewe, amekiri shtaka hilo leo Alhamisi, Julai 11, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Dar es Salaam, kisha kuhukumiwa papo hapo kulipa faini ya Sh50, 000 au kwenda jela mwaka mmoja.

Mfamasia huyo amekiri shtaka hilo, muda mfupi baada ya upande wa mashtaka kuwasomea upya hati ya mashtaka.

Lobi ambaye alikuwa amekaa bechi la mbele akiwa amevalia dera rangi ya kijivu na mkononi ameshikilia kipochi kidogo maarufu ‘Nainai’ huku kichwani akiwa amesuka rasta za mawimbi ya kuchambua, alinyoosha mkono kuashiria anataka apewe nafasi na mahakama ya kuzungumza.

Baada ya kunyoosha mkono huo, Hakimu Mhina amemuuliza iwapo mshtakiwa huyo ana tatizo na sehemu ya mazungumzo ilikuwa ni kama ifuatayo:

Hakimu: Eeeh uliyenyoosha mkono

Mshtakiwa: Ndio mheshimiwa

Mshtakiwa: Mheshiwa hakimu kabla kesi haijaendelea, naomba kukiri kosa langu

Hakimu: Haya upande wa mashtaka mkumbushe mshtakiwa shtaka lake

Wakili wa Serikali Regina Kanyuni alimsomea upya shtaka lake.

Baada ya kukumbushwa shtaka lake, Lobi amekiri kutenda kosa hilo na hivyo upande wa mashtaka ulimsomea maelezo yake.

Baada ya kusomewa maelezo yake na kukiri, Mahakama ilimtia hatiani kama alivyoshtakiwa.

“Lobi, mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya vitendo vya ukahaba kinyume cha sheria,” amesema Hakimu Mhina.

Hakimu amefafanua kuwa kosa linalomkabili mshtakiwa huyo, adhabu yake ni faini ya Sh100, 000 au kifungo cha mwezi mmoja jela.

Mshtakiwa baada ya kutiwa hatiani, mahakama hiyo ilimpa nafasi ya kujitetea kwanini asipewe adhabu kali na sehemu ya maombi yake mshtakiwa yalikuwa kama ifuatavyo:

Mshtakiwa: Ni kweli mheshimiwa

Mshtakiwa: Ni kweli nilikamatwa na polisi nikiwa nimevaa nguo zisizo na stahaa

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, naomba mahakama yako inipunguzie adhabu kwa sababu mama yangu ni mgonjwa.

Naomba mahakama inisamehe, sitarudia tena. Nafanya kazi, hivyo kibarua changu kitaota nyasi.

Baada ya maombi hayo, Hakimu Mhina alimhoji mshtakiwa anafanya wapi?

Hakimu: Unafanya kazi wapi?

Hakimu: Unafanya kazi gani?

Mshtakiwa: Mimi ni mfamasia kwenye duka la dawa lililopo Mbezi.

Majibu ya Lobi yamewashtua washtakiwa wenzake na watu waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo, huku wengine wakiguna kwa mshangao na wengine wakimkodolea macho na wengine wametikisa vichwa.

Awali, kabla ya kutolewe kwa adhabu hiyo, upande wa mashtaka umedai hauna kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa huyo, lakini ukaomba mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

“Hatuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi mshtakiwa huyu, ila tunaiomba mahakama itoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria kwa sababu kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni kinyume na maadili,” amesema wakili Kanyuni.

Akitoa hukumu, Hakimu Mhina amesema mahakama hiyo imemtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kosa la kufanya vitendo visivyo vya staha katika maeneo ya umma kwa ajili ya ukahaba.

“Nimesikiliza utetezi wa mshtakiwa na ombi lililotolewa na upande wa mashtaka, ni kweli si matendo mazuri uliyofanya kwa sababu yanashusha heshima na utu wako kwa jamii, pia sio kitu kizuri katika jamii, watoto wadogo wanajifunza nini kutoka kwako? amehoji hakimu na kuongeza

“Kwa kuwa umekiri shtaka lako, mahakama hii inakuhukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh50, 000 na ukishindwa utatumikia kifungo cha mwezi mmoja jela na haki ya kukata rufaa ipo wazi kwa pande zote, iwapo hamjaridhika na adhabu hii,” amesema Hakimu Mhina.

Mshtakiwa baada ya kuhukumiwa na kesi huahirsihwa alijifunika mtandio wake wa dera kichwani na hivyo kupelekwa mahabusu kusubiri kulipa faini.

Katika kesi hiyo, Lobi alikuwa anakabiliwa na kesi jinai 17279 ya mwaka 2024, yenye shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, alikutwa akifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, akiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.

Juni 24, 2024, Lobi na wenzake walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka hayo na kukana.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo baada ya hukumu amefanikiwa kulipa faini hiyo na kuachiwa huru. Kesi inaendelea kwa washtakiwa wengine.

Endelea kufuatilia kwa habari na taarifa zaidi.

Una maoni yoyote kuhusu habari hii? Tuandikie kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!