NewsSWAHILI NEWS

Katibu tawala aonya uchafu Moro wakisaka ridhaa ya kuwa jiji

Morogoro. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima akiendelea na harakati za kuhakikisha Manispaa ya Morogoro inakuwa jiji, Katibu Tawala wa mkoa huo, Mussa Ally Musa amesema ili jitihada hizo zifanikiwe lazima usafi ufanyike tofauti na hali ilivyo sasa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Julai 7, 2024, Katibu tawala huyo amesema wakazi wa manispaa hiyo wanatakiwa kuacha tabia ya kutupa taka hovyo.

Amesema kuna haja ya kuweka mikakati mahususi ya kukabiliana na uchafu ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria ndogo za usafi wa mji walizojiwekea.

“Ninasikitika sana kuona manispaa hii inakuwa na mazingira machafu kwa muda wote, pale  soko la Mawenzi hapatazamiki kutokana na uchafu, naziagiza mamlaka mbalimbali kuja na njia mbadala ya kuhakikisha maeneo yenu yanakuwa safi muda wote tofauti na hali ilivyo sasa,” amesema Ally.

Hivi karibuni katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Malima alisema mkakati wake ni kuona Morogoro inakuwa jiji kwa haraka zaidi.

“Kupitia ujio wa treni ya kisasa SGR, hii itakiwa chachu ya maendeleo katika mkoa huu hivyo ninaendelea kupambana kuhakikisha manispaa hii inakuwa Jiji. Hamtaweza kuwa jiji kama pia makusanyo ya mapato yenu ni hafifu, pamoja na kwamba mnaongoza kwa kukusanya mapato kwa mkoa mzima bado mnatakiwa kuongeza ukusanyaji zaidi kwa dhamira ya kukidhi kigezo cha kuwa jiji,” alisema Malima.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa amesema pamoja na changamoto ya uchafu, lakini upo mpango wa kuupanga mji huo ili uwe wa kisasa na wakuvutia zaidi.

“Changamoto zinazotajwa tutazifanyia kazi ipasavyo lakini kilichopo mbele yetu ni kuupanga huu mji ili uwe wa kuvutia zaidi pamoja na kuondoa vibanda ambavyo haviko kwenye utaratibu, lengo ikiwa ni kukidhi matakwa ya manispaa hiyo kuwa Jiji,” amesema Rebeca.

Wasemavyo wafanyabiashara

Mwananchi ilifunga safari hadi soko la Mawenzi kwa lengo la kuzungumza na wafanyabiashara juu ya hali ya usafi.

Alfredy Yasini ni mfanyabiashara wa soko hilo la  amesema Manispaa ya Morogoro inapaswa kuboresha miundombinu sambamba na kuzoa taka zinazozalishwa ndani ya soko hilo kwa wakati.

“Morogoro kuwa Jiji inawezekana, lakini kwenye suala la usafi bado kuna changamoto hususani kwenye soko hili, ukiangalia mazingira ya hapa ni machafu na watu wa halmashauri wanatusahau, unakuta takataka zinazagaa hapa sokoni hazizolewi Kwa wakati hii ni kero yetu kubwa,” amesema Yasini.

Naye Suzana Katielda mfanyabiashara sokoni hapo amesema soko hilo haliwezi kuwa safi kama manispaa haitadhibiti maji taka yanayotiririka sokoni hapo.

“Tukitaka kuwa jiji, lazima tuwe wasafi kwanza, mfano hapa sokoni, chemba za maji taka zinafumuka hovyo tu lakini viongozi wakati mwingine wanakuwa kimya mpaka inakuwa kero, hivyo kama mkakati wa kuwa jiji upo, basi mazingira yasafishwe na watu wapewe elimu ya kila mara watunze mazingira,” amesema Katielda.

 Kwa upande wake Diwani wa Mji mkuu, Samwel Msuya amesema pamoja na ushauri na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Serikali kuhusu manispaa kuimarisha usafi lakini pia wananchi wanalo jukumu la kubadili tabia, kwa kuacha kutupa taka hovyo na kutiririsha maji machafu kwenye nyumba zao.

“Manispaa inaweza kusimamia usafi na kuja na mikakati ya kuufanya mji uwe safi lakini wapo wakazi wa manispaa hii wanaokusanya taka kwenye nyumba zao na baadaye kwenda kuzitupa kwenye mitaro na maeneo ya wazi, wengine wanatiriri sha maji machafu ya vyooni,” amesema Msuya.

Amesema Baraza la Madiwani linajitahidi kuisukuma ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kusimamia suala la uzoaji wa taka, lakini baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo hurudisha nyuma jitihada hizo kwa kuendelea kuzitupa hovyo

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!