NewsSWAHILI NEWS

Janga la maadili pasua kichwa kwenye jamii

Dar es Salaam. “Maisha ya zamani yalijawa hekima ambayo mtoto alikuwa si wa kwako peke yako, bali wa jamii nzima, alifundishwa maaadili ya namna ya kuishi na watu.

“Akitokea mzee amebeba mzigo, mtoto anaenda anamsalimia kisha anamuomba kumpokea mzigo alioubeba na kuutanguliza kule anakoelekea mzee huyo.

“Sasa hivi hayo yote yamepotea, hata wazee wenyewe hawaukubali utamaduni huo, ndiyo kwanza hujiuliza akikubali kupokewa huo mzigo, utafika salama? Hukumbwa na wasiwasi kutokana na mmomonyoko wa maadili uliopo sasa.”

Haya ni maneno ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, aliyoyatoa wakati akizindua kitabu chake kiitwacho ‘Mmomonyoko wa Maadili Nani Alaumiwe?’ Jumatano ya Julai 3, 2024.

Msingi wa alichokizungumza Mufti unatokana na mmomonyoko wa maadili hivi sasa ambapo serikali, dini, wazazi hata walimu wanapambana kila mmoja kwa nafasi yake kuweza kurejesha maadili yanayoendelea kuporomoka.

Jambo hilo ndilo lililomsukuma Mufti kutunga kitabu hicho kinachouliza nani wa kulaumiwa.

Katika tafsiri ya maadili ya Kitanzania katika kitabu hicho, kinaeleza ni kama seti ya kanuni na imani zinazokubalika katika jamii ambayo hutumika kama kielelezo cha mwenendo na tathmini ya yaliyo sawa na yasiyo sawa.

“Kwa mujibu wa jamii ya Kitanzania, maadili ni utamaduni, mambo ambayo inayatekeleza katika maisha ya kila siku kama heshima, mavazi, uwajibikaji, na utunzaji wa watoto, wazee, vijana, pamoja na walemavu,” kimeeleza kitabu hicho cha Mufti.

Wakati Mufti Zuberi anayabainisha hayo, suala la maadili limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa wazazi, viongozi wa dini na wa Serikali, kutokana na kasi ya mmomonyoko iliyopo sasa.

Inaelezwa kwamba, hivi sasa kila mmoja anaishi anavyotaka na anafanya atakalo, bila kujali athari itakayopatikana.

Baadhi ya watu wanavaa nusu utupu, wanaume wanavaa hereni, na kuna mwenendo wa kuvaa mavazi yasiyo ya heshima, kunajisiana, kubakana na mapenzi ya jinsia moja. Mambo haya yote ni matokeo ya kupotea kwa maadili.

Mufti anasema kuna baadhi ya mambo ambayo wazazi wameyaacha, ikiwemo kama mtoto asiposalimia asubuhi wageni anaonywa, kulia bila sababu, akipigwa asipolia anapigwa tena ili alie, na akijibu vibaya wakubwa anaonywa. Hizi ni baadhi ya tamaduni za Watanzania zinazopotea.

Mufti anasema kila mmoja anahusika katika mmomonyoko wa maadili, kuanzia baba, mama nyumbani, wazee mtaani, kina dada, kina mama, na kina kaka. Wote wanastahili kuhusika kwa pamoja.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kitabu hicho, anasema kuna kila haja ya jamii kuanzia vijana, wazazi, wanafunzi, Serikali na jamii kwa ujumla kusimamia maadili mema ya Kitanzania. Anasema ni bora mtu uitwe mshamba lakini usimamie misingi na tabia zote zilizo njema zinazokupa utamaduni unaotambulika na kuachana na maadili yasiyofaa.

“Niwakumbushe Watanzania wenzangu taifa letu lazima lishiriki katika makuzi na maadili ya watoto kwa kutenga muda wa kuona watoto wetu wanaishije.

Niwaambie, taifa lolote ambalo halina utamaduni unaojivunia na linakumbatia utamaduni wa wenzake, maadili ya taifa hilo yamekufa.”

Ajenda ya malezi imekuwa pia mdomoni mwa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye mara kadhaa amekuwa akikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Mei 7, 2021, ikiwa ni miezi miwili tangu aapishwe kushika kiti cha Urais, alikutana na wazee wa jiji la Dar es Salaam na katika mengi aliyozungumza nao, aliweka msisitizo kwenye suala la malezi na maadili.

“Kama mtoto anamuangalia mzee amesimama kwenye chombo cha usafiri, basi kuna dosari. Watanzania turudi kwenye malezi yenye maadili.

“Inashangaza kuona kijana amekaa kwenye kiti halafu mzee amesimama. Tunaona matukio ya uhalifu watu wanasingizia hali ngumu, hali ngumu ya uchumi haifanyi mtu awe jambazi. “Naomba turudi kuangalia watoto wetu ili watunze ulinzi na usalama wa mali zetu. Niwaombe pia wazee mzungumze na vijana wenu na wote kwa pamoja turudi kwenye maadili kuwa raia wema,” aliwahi kusema Rais Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akizungumzia mmomonyoko wa maadili unavyoendelea kusumbua familia nyingi nchini.

Septemba 11, 2022, akihutubia maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata), Rais Samia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake kusimama imara katika malezi ili kutengeneza taifa la watu wenye maadili, akitilia mkazo matumizi sahihi ya teknolojia kwa vijana.

“Tuwalee watoto na vijana wetu katika maadili mema wakitambua wana kazi ya kuendeleza kanisa na taifa, mzigo wa kulea taifa, tunataka vijana waaminike, wakubalike wawe waaminifu na wenye matendo mema, tumepewa wanawake.

“Wawata msisite kutoa elimu ya uongozi kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwa na uthubutu, twendeni kifua mbele, tukafundishane na kulinda watoto wetu, kwani sisi ni mashujaa na tuna heshima.

“Wazazi tunasimama wapi kwenye kuwaelekeza vijana matumizi sahihi ya teknolojia hiyo. Maadili katika vyombo hivi hakuna, tusiwaache watumie wanavyotaka,” alisema Rais Samia.

Septemba 11, 2023, wakati akifungua mkutano maalumu wa Baraza la vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia, pia alitoa wito kwa jamii kubeba mzigo wa malezi kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana ili kulinusuru taifa.

Alisema changamoto hiyo kwa sasa inalisumbua taifa na kuna hatari hali ikawa mbaya zaidi endapo wazazi, walezi, viongozi wa dini, wazee na jamii kwa ujumla hawatasimama kikamilifu kuhakikisha watoto na vijana wanalelewa kwa kuzingatia maadili.

“Maendeleo na utandawazi isiwe sababu au kisingizio cha kuruhusu vitendo vya mmomonyoko wa maadili, kinyume na hapo taifa litapotea.

Tuna kilio kikubwa cha mmomonyoko wa maadili kwa vijana wetu, wazazi ndio sisi.

Sisi tumekuzwa katika maadili mengine, tulichokizaa sisi kinakuja cha aina nyingine kwa kisingizio cha utandawazi na maendeleo. Nasema hapana, kwa sababu maendeleo ni pamoja na kuangalia silka, mila na desturi zetu. Maadili tuanze huku chini na mara nyingi linapozungumzwa suala hili msukumo unaenda serikalini na shuleni, lakini huyu mtoto hakuzaliwa na shule, nyumbani ana wazazi, hebu tujiulize tunatimiza wajibu wetu. Nalisema hili twendeni tukalitazame vizuri, watoto wanatupotea,” alisema Rais Samia.

Akizungumza na Mwananchi, Salum Mwalimu anasema suala la mmomonyoko wa maadili halipaswi kuonewa haya.

“Kuna mambo yanayorudisha nyuma ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla, kama watu mnapambana na mmomonyoko wa maadili unaotokana na uadilifu kwa namna moja au nyingine unazorotesha ukuaji wa maendeleo ya nchi, hivyo kila mmoja awajibike. Tujikite kwenye malezi ya familia na tuache yale mawazo ya mmoja kuona mtoto wako ni wako, bali mtoto anapaswa kuwa wa jamii,” anasema Mwalimu.

Pili Chande, yeye anatamani kila kiongozi wa dini hapa nchini aweke nguvu kwenye suala la maadili katika kuwafundisha waumini wake.

“Heshima ya mkubwa kwa mkubwa sasa hivi haipo, natamani viongozi wa dini kwa pamoja waungane katika hili, kwa kuwa mafundisho yao yanaingia moja kwa moja kwa waumini ambao ndio jamii,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima anasema maendeleo ya Tehama yana madhara na kama viongozi na walezi lazima wapande mbegu nzuri, ikiwemo ya hofu ya Mungu kwa watoto wao.

“Kitabu hiki kimetuongezea rejea katika kampeni yetu ya kupambana na mmomonyoko wa maadili na tutakuwa bega kwa bega kukiweka katika programu zetu na kama Wizara tutanunua vitabu vya Sh7 milioni,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule anasema lazima tukubaliane kuna tatizo kwenye jamii, kwamba kuna mmomonyoko wa maadili, ikiwemo vipigo kwa watoto, kina mama, dawa za kulevya, utupaji taka hovyo.

“Yote haya yanatokea lakini Tanzania haijakaa kimya. Serikali imekuwa ikisisitiza yale yaliyo mema. Kitabu hiki pia ni kielelezo cha kuutafuta mwarobaini wa mmomonyoko huo,” amesema.

Ally Ngeruko, mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, anasema wazazi wanapaswa wakae na watoto wao na familia zao kwa ujumla watafakari mmomonyoko wa maadili uliopo, kwa kutazama hata mavazi ya watoto wao, hususan wa kike.

“Baba mzazi, mtoto wako wa kike amevaa mavazi yaliyo nje na maadili, halafu unamtazama. Sasa wakati umefika wa kukemea maovu na kufundisha mema, ili jamii yetu itoke hapa ilipo iende kuwa bora na nzuri, watu watakaoishi bila husda na chuki,” anasema Ngeruko.

Mzazi wa watoto wawili, Mariam Mohammed, anasema umefika wakati wa kujadili tabia chafu katika jamii, kwani yanayoendelea kwa sasa yanaogopesha.

“Natamani kila mzazi nyumbani asisitize kila liwezekanalo, ikiwemo kuwafuatilia kila walifanyalo ili watoto wanaokua wakue katika tabia njema,” anasema Mariam.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!