NewsSWAHILI NEWS

GGML kukusanya Sh2.6 bilioni mapambano dhidi ya VVU

Chato. Licha ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kuonekana kupungua kwa watu wazima, juhudi za makusudi za kutoa elimu kwa vijana wenye wa miaka kati ya 15-24 zinahitajika ili kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya sifuri tatu yaani maambukizi mapya sifuri, kumaliza unyanyapaa sifuri na vifo sifuri  ifikapo mwaka 2030.

Na katika kuunga mkono juhudi hizo, Mgodi wa Geita wa Dhahabu wa Geita (GGML) kupitia Kampeni yake ya KiliChallenge -2024, imelenga kukusanya zaidi ya Sh2.6 bilioni kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).

Imeelezwa kuwa fedha hizo pamoja na mambo mengine, zitatolewa kwa mashirika ya kijamii  (CBO) mkoani humo ili yaweze kutoa elimu ya Ukimwi kwa vijana.

Akizungumza jana Jumamosi Julai 6, 2024 wakati wanafanya usafi sambamba na miti katika Hospitali ya Wilaya ya Chato, Meneja Mwandamizi na Uhusiano wa Jamii kutoka GGML, Gilbert Moria amesema ufanywaji wa shughuli hizo kwenye jamii unalenga kuhamasisha watu kujilinda ili kuepuka kupata maambukizi mapya ya VVU.

Moria amesema mwaka huu, watu 70 wakiwemo wafanyakazi wa GGML, Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) na wageni kutoka Australia na Afrika Kusini, wanatarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kwa siku saba kuanzia Julai 19-25 kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa fedha za mapambano dhidi ya VVU.

Amesema GGML kwa kushirikiana na Tacaids kila mwaka huandaa kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kwa mwaka huu, wamelenga kukusanya zaidi ya Sh2.6 bilioni.

Amesema fedha hizo zitatumika kutoa elimu ya VVU, kusaidia wanaoishi na VVU pamoja na kuziwezesha CBO kuwafikia wananchi walioko vijijini ili nao wapate elimu ya namna ya kupambana na Ukimwi.

“Tunatarajia kukusanya Sh2.6 bilioni na tutakuwa na wapanda mlima 70 ambao 45 watapanda mlima kwa miguu na wengine 25 watazunguka mlima kwa kuendesha baiskeli. “Mwaka huu ni mwaka wa 22 toka tuanze mwaka 2002 na fedha zinazokusanywa zimekuwa zikisaidia sana kwenye mapambano ya VVU,” amesema Mworia.

Naye Meneja wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Kiva Mvungi amesema tangu kuanza kwa kampeni hiyo ya KiliChallenge mwaka 2002, wamefanikiwa kuwasaidia watoto 100 wanaoishi kituo cha Moyo wa Huruma Mjini Geita, kujenga vituo vya kupumzikia kwa madereva wa magari makubwa (Malori) maeneo ya Manyoni na Tanga.

“Fedha hizi pia hutolewa kwa taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya mapambano ya VVU. Tumetoa kiasi cha fedha kukarabati hospitali ya Kifua Kikuu Kibon’goto, hii tuliikarabati kwa sababu asilimia 50 ya wenye VVU wanapata ugonjwa wa kifua kikuu, ndiyo maana tukaona kuna sababu ya kuboresha ile hospitali,” amesema Mvungi.

Takwimu zinaonesha maambukizi ya Ukimwi yamepungua kwa asilimia 88 kutokana na vifo vitokanavyo na Ukimwi kupungua kwa asilimia 50 kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi vifo 32,000 mwaka 2020.

Aidha, maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima yameshuka kutoka watu 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020.

Pamoja na mafanikio hayo, bado yapo maambukizi mapya kwa vijana ambapo takwimu zinaonyesha theluthi moja ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 huku wengi wakiwa vijana wa kike.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!