NewsSWAHILI NEWS

Dk Nchimbi akemea kauli za kibaguzi CCM

Iringa. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuepuka kutoa kauli za kibaguzi au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.

Kauli ya Dk Nchimbi imekuja kutokana na video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha mmoja wa makada wa CCM, akitoa kauli zinazoashiria ubaguzi katika kupata haki.

Katika video hiyo iliyorushwa mitandaoni jana Jumatano Julai 10, 2024 na leo Alhamisi Julai 11, anaonekana kada wa CCM ambaye bado hajafahamika jina wala eneo, akisema mtu wa CCM akiwa na kesi ni rahisi kupata msamaha tofauti na Chadema. 

“Ukipata tatizo kesi ya mwana CCM au mwana Chadema ni vitu viwili tofauti, hata iwe polisi au kwa mwenyekiti wa kijiji.

“Huyu (CCM) anaweza, hebu pisha usirudie moja, mbili na tatu wewe usirudie kufanya, lakini tukikujua wewe ni wa…(anaonyesha alama ya vema inayotumiwa na Chadema), tutahangaika na wewe, eeeh tukubali hii nchi kwa sasa hivi,” alisema kada huyo.

Hata hivyo, akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa UVCCM ngazi za mikoa na wilaya zote, Ihemi mkoani Iringa leo Alhamisi Julai 11, 2024, Dk Nchimbi amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.

“Niwasisitizie UVCCM ni umuhimu kwa watendaji wetu, viongozi wetu na wanachama wetu kutambua kuwa mnabeba taswira ya chama chetu kila wakati, katika mnayosema au kutenda.

“Kama kuna jambo tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania,” amesema Balozi Nchimbi.

Katika maelezo yake, Balozi Nchimbi amewataka UVCCM kuwa mstari wa mbele kulinda taswira hiyo muda wote na kujiepusha na kauli au matendo yanayoharibu taswira ya chama hicho tawala.

“Katika kila unachokisema au kukitenda lazima utafakari, je kina athari gani kwa CCM na nchi yetu,”amesema Dk Nchimbi.

Hii sio mara kwanza kwa Balozi Nchimbi kuingilia kati na kukemea vitendo hivyo, mathalani kauli iliyotolewa Aprili mwaka huu na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan ya kulitaka jeshi la polisi kutowatafuta vijana wanaotukana na viongozi pindi wanapopotezwa.

“Leo akiibuka kijana wa UVCCM akisema wapinzani wetu wakifanya hivi tutawapoteza huyu ni kijana wetu, lakini amesema jambo la kijinga lazima tutalipinga kwa sababu mwisho wa siku nchi hii ni yetu sote, sio ya chama cha siasa, dini wala kabila,” alisema Dk Nchimbi.

Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi amewapongeza UVCCM kwa kuweka ya kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa walipozindua mkakati wao wa ‘Tunazima zote, tunawasha kijani’, akiwataka wasonge mbele, watumie ushawishi walionao kwa vijana nchini.

Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa UVCCM,  Mohammed Ali Kawaida, amekishukuru chama hicho kwa namna  kinavyoendelea kuwalea na kuwaamini vijana kukitumikia chama na jumuiya zake na nchi.

Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo amesema mafunzo hayo yatawasaidia viongozi na watendaji wa jumuiya hiyo kwenye mikoa, wilaya na hatimaye kushuka ngazi nyingine nchi nzima kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaohitajika.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!