NewsSWAHILI NEWS

Chalamila alivyomaliza mgomo uliodumu kwa saa tano Simu2000

Dar es Salaam. Katika hali isiyotabirika, mgomo na maandamano ya wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga ulizuka kwa takriban saa tano katika Soko la Simu2000 jijini hapa.

Mzizi wa mgomo huo, ni kuishinikiza Manispaa ya Ubungo ifute uamuzi wake wa kukabidhi eneo linalotumiwa na wamachinga kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kwa ajili ya kujenga karakana.

Manispaa hiyo ilitoa taarifa ya kufanya uamuzi huo, Julai 4, 2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichoeleza, tayari baraza hilo na manispaa zimeridhia ombi hilo la Dart, baada ya vikao mbalimbali ikiwemo wakala huo na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko.

“Baada ya majadiliano hayo na baada ya madiwani kuonyeshwa mchoro mzima wa mradi huo na wao kutafakari na kuona wafanyabiashara waliopo pale watakwenda wapi, hivyo basi leo hii (Julai 4), baraza limeamua rasmi kwamba eneo litolewe kwa Dart,” alisema Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Nyaigesha.

Kutokana na taarifa hiyo iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii ukiwemo ukurasa wa Instagram wa Manispaa ya Ubungo, wafanyabiashara katika soko hilo wamesema kilichofanyika ni kama kuwafukuza katika eneo waliloaminishwa watakuwepo wakati wote.

“Tuliaminishwa eneo hili ndilo yatakuwa makazi rasmi ya biashara zetu baada ya kuhamishwahamishwa kutoka barabarani na maeneo mengine ndani ya manispaa hii, leo tunasikia habari za kuja Dart, wameamua kutufukuza,” alisema Mussa Ndile, Mwenyekiti wa kamati ndogo ya maboresho ya soko hilo ambaye pia ni mfanyabiashara sokoni hapo.

Mgomo na maandamano hayo yameanza leo Jumatatu saa 1 asubuhi kwa wafanyabiashara kujikusanya katika lango la kutokea kwenye Kituo cha Daladala cha Simu2000.

Kujikusanya kwao kuliambana na kuweka vizuizi katika milango yote la kuingilia na kutokea magari kwenye kituo hicho, huku kila duka na biashara sokoni hapo zikiwa zimefungwa.

Si hivyo tu, vizuizi pia viliwekwa katika barabara ya Simu2000 kwenda Sinza na hivyo kuzuia shughuli za usafirishaji wa abiria zilizokuwa zinafanywa na daladala.

Nyimbo za ‘hatutaki karakana tunataka soko letu’ ndizo zilizokuwa zikisikika katika eneo hilo, huku mabango yaliyoandikwa jumbe mbalimbali ikiwemo ‘hatutaki karakana Simu2000, Mama Samia njoo ututetee.’

Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilianza kuingia katika eneo hilo na kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara, bila mafanikio na saa 3 asubuhi alifika Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko na wafanyabiashara hao kumtaka aondoke katika eneo hilo kwa kile walichodai, walishamwita kwa takriban mara tatu, lakini aliwapuuza.

Kutokana na mabishano yaliyokuwepo kati ya wafanyabiashara na vikosi vya ulinzi na usalama, ilibidi Bomboko asogee kwa umbali na mita kadhaa kutoka eneo walilokuwepo wafanyabiashara, bila kufanikiwa kuzungumza nao chochote.

Shangwe na hali ya kuzomewa ilizuka kutoka kwa wafanyabiashara hao wakifurahia kusogea kwa kiongozi huyo.

Baada ya kusogea pembeni, Bomboko alizungumza na vyombo vya habari akihoji ni kiongozi gani aliyetangaza eneo hilo limebadilika matumizi na kwenda kwa Dart kwa ajili ya kujenga karakana.

“Taarifa hizi mmepata wapi, tusaidiane hapa ili tuone, sisi tumekuja kusikiliza baada ya kupata taarifa wafanyabiashara wenye maduka na bodaboda wanazuia daladala zisiingie ndani mawasiliano,” amesema.

Ameeleza ujio wake katika eneo hilo ni kujiridhisha na uhalisia wa taarifa alizosikia kuhusu kusitishwa kwa usafiri wa daladala, kadhalika taarifa inayodai soko limeuzwa kwa Wachina.

“Hii ni taarifa ninayosikia kutoka kwa wafanyabiashara ni Mchina gani aliyenunua soko, lakini kiongozi gani aliyetangaza kwamba hili eneo linakwenda kubadilishwa matumizi,” amehoji.

Kwa mujibu wa Bomboko, kuna siasa katika eneo hilo akisema ni vuguvugu lililoanza katika maeneo mengi zikilenga kuifanya Serikali iache kuendelea na mambo ya msingi.

“Ombi langu ni kwamba tuache wafanyabiashara wengine walio tayari kufanya biashara waendelee lakini wale ambao wana mashinikizo yao, Serikali ipo tayari kuwasikiliza,” amesema.

Wafanyabiashara wa Soko la Mawasiliano wakiwa wamefunga barabara leo Julai 8, 2024. Picha na Michael Matemanga

Saa 4 asubuhi mgomo na maandamano hayo yalisababisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila afike sokoni hapo.

Haikuwa kama kwa Bomboko, wafanyabiashara hao walimpokea kwa shangwe Chalamila huku nyimbo za kumsifu na kuonyesha tumaini kutokana na ujio wake zikiimbwa.

Katika mazungumzo yake, Chalamila ameahidi kukutana na wafanyabiashara hao Julai 13, 2024 akiwa na mamlaka zote zinazolalamikiwa ikiwa ni baada ya kuzisikiliza huko ziliko na kuja kuzisikiliza tena mbele ya wamachinga hao.

Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa mpango wa Dart kupewa sehemu ya eneo hilo, ingawa amedai alielekeza Manispaa ya Ubungo izungumze na wakala huo kisha iliwasilishe jambo hilo kwake.

“Hili linalosemwa kwa asilimia 100 lipo, lisemwalo lipo ndugu zangu, ingawa bado halijafika ofisini kwangu, lakini mlipaswa kushirikishwa,” amesema.

Amewataka wafanyabiashara hao wafungue biashara na kuendelea na shughuli zao, akisisitiza Julai watasikia kutoka kwa Serikali uhalisia wa jambo wanalogomea.

Lakini, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kabla ya uamuzi wowote ilikuwa muhimu wafanyabiashara kushirikishwa, akisisitiza “imetosha kuendelea kuwanyanyasa wafanyabiashara.”

“Leo ni Jumatatu naomba muendelee na kazi zenu hadi Jumamosi nitakuja nataka kumsikiliza mtu wa Dart na wengine wote, kisha kwa kuwa sio siri nikija Jumamosi nitakuwa nao ili wanieleze mbele yenu,” amesema.

Awali, kabla ya kuzungumza, Chalamika alitoa nafasi kwa wafanyabiashara waeleze sababu ya kugoma kwao, Ndile alikuwa miongoni mwa wazungumzaji.

Katika maelezo yake, Ndile ameonyesha hofu ya wafanyabiashara kuhamishwa katika eneo hilo kutokana na Manispaa ya Ubungo kuvunja ahadi yake ya kuwaacha waendelee kulitumia, badala yake inawakabidhi Dart.

Ameeleza licha ya Serikali kutumia takriban Sh300 milioni kwa ajili ya maboresho hayo, inaonekana manispaa hiyo haioni umuhimu wake, ndiyo maana inaamua kulikabidhi kwa wakala huo.

Amekwenda mbali zaidi akieleza pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali, wafanyabiashara nao wamewekeza fedha zao kuboresha vibanda hivyo.

“Tulikubali kuhamishwa barabarani na katika maeneo mengine ya barabara na tuliambiwa hapa ndiyo yatakuwa makazi yetu ya kudumu iweje leo anapewa Dart,” amehoji.

Baada ya Chamila kuzungumza na wafanyabiashara hao mgomo huo ulimalizika na wakaendelea na shughuli zao ikiwemo huduma za usafiri kituo cha Simu2000 kurejea.

Meya mstaafu wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob alichapisha katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), akisema atawarudisha wafanyabiashara hao barabarani.

Chapisho lake hilo, linatokana na kile alichoeleza, ni yeye akiwa Diwani wa Kinondoni mwaka 2010-2015 halmashauri hiyo ilinunua ekari tano za eneo hilo kutoka kwa Shirika la Posta lililokuwa linalimiliki.

Baada ya kununua, alisema liligawiwa kwa ajili ya matumizi ya stendi ya daladala, choo cha umma na soko la mazao na biashara ndogondogo mwaka 2013.

Baadaye mwaka 2016 alipokuwa Meya wa Kinondoni, alisema walizungumza na wafanyabiashara kuwaondoa katika maeneo ya barabara ikiwemo Ubungo Mataa na wote walikubali.

“Novemba 2017 baada ya mgawanyo wa Halmashauri ya Kinondoni na Ubungo, sisi wa halmashauri mpya ya Ubungo tuliwaomba wenzetu watuachie Stendi ya Mawasiliano na soko hilo la Simu2000,” aliandika.

Hilo lilitekelezwa kwa makubaliano kuwa, Manispaa ya Ubungo itaiachia Kinondoni Stendi ya Makumbusho na soko la Makumbusho na kwamba anashangazwa na uamuzi wa Julai 4, mwaka huu wa baraza la madiwani.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi juzi Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Aron Kagurumjuli alikiri kuwepo kwa mpango huo akifafanua hautaathiri uwepo wa wafanyabiashara wala kituo cha daladala.

Kwa mujibu wa Kagurumjuli, hakuna wamachinga watakaoondolewa katika eneo hilo kutokana na utekelezwaji wa mpango huo, zaidi ya kuboreshewa zaidi maeneo yao ya kufanyia shughuli zao.

“Kabla ya lolote wataboreshewa kwanza eneo la kufanyia biashara, likishakamilika kuboreshwa watapewa ni hapohapo wala si kwingine,” alisema.

Katika maboresho hayo, Mkurugenzi huyo alisema vibanda 989 vya wamachinga, fremu za maduka makubwa 186 na maeneo ya mama na babalishe yatajengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!