NewsSWAHILI NEWS

‘Bado Afrika haijawa tayari kuwekeza kwenye mifumo’

Unguja. Wakati mabadiliko ya teknolojia yakiendelea kukua kwa kasi duniani kote, imeelezwa nchi za Afrika bado zinakumbwa na changamoto katika matumizi ya teknolojia hizo.

Hayo yamebainika katika mkutano wa kupanga mikakati ya kwenda kidigitali kisiwani Zanzibar.

Akizungumza katika mkutao huo uliofanyika hivi karibuni, Mkurugenzi Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu, Ushauri wa Kodi na Biashara (BDO) kutoka Afrika Kusini, Mark Stewart amesema wana wajibu wa kuweka mikakati itakayosaidia ubunifu na kukuza teknolojia hususani matumizi ya akili bandia.

“Changamoto ambayo ipo Afrika ni kutokuwa tayari katika kubadilisha mitazamo ya kuwekeza katika mifumo ya kidigitali,” amesema Stewart.

Hata hivyo, amesema wapo tayari kuishauri Serikali na wadau wengine kuingia katika mifumo hiyo ili kuboresha ufanisi wa kazi zao.

Mbia Mwandamizi kutoka BDO Tanzania, Yusuf Chanyika amesema kwa sasa matumizi ya teknolojia hayakwepeki kwa kuwa dunia inaelekea huko.

Hata hivyo, amesema licha ya kuwapo wasiwasi kwamba matumzi ya akili bandia yanaondosha kazi za watu wengine, amesema jambo hilo sio kweli bali teknolojia inaongeza ufanisi na kuleta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali.

“Ninachowaambia watu wasiogope kuja kwa teknolojia hii kwa kuhofia watapoteza kazi zao, waingie ili kuongeza ufanisi wa kazi, kwani bado teknolojia inaendeshwa na binadamu mwenyewe” amesema Yusuf.

Sambamba na hilo amesema teknolojia hiyo itaboresha mifumo mingi wanayotumia kwa sasa, hivyo ni wakati sahihi wa Serikali nayo kuingia ili kuongeza ufanisi wa kazi.

“Teknolojia inaenda kasi, hivyo ukiwa hujaingia katika teknolojia hiyo utakuwa umeachwa mbali sana na itasababisha urasimu katika kazi zako, jambo linalotakiwa kufanywa kwa siku moja unalifanya mwezi mmoja,” amesema Yusuf.

Mkurugenzi Mtendaji wa BDO Afrika Mashariki, Sandeep Khapre amesema wamekutana kutengeneza mikakati itakayokidhi mahitaji katika ubunifu na kutatua changamoto za kijamii.

Amesema mfumo huo ni muhimu kutumiwa na kisiwa cha utalii cha Zanzibar kwa kuwa utasaidia katika uwekezaji na kuongeza thamani ya biashara kwao.

Teknolojia hiyo inatumika katika sekta zote ila kwa upande wa utalii itasaidia kuongeza mvuto kwa watalii kwa kuwa nchi nyingi zinatumia mfumo huo katika kuongeza ubora kwa wateja wake.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!