NewsSWAHILI NEWS

Baba mbaroni akidaiwa kumnyonga hadi kufa mtoto wa kambo

Dodoma. Stephen Mabula (44), mkazi wa kijiji cha Mheme, Kata ya Huzi, Tarafa ya Mpwayungu wilayani Chamwino anashikiliwa na Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumnyonga mwanae wa kambo, Godluck Mathias (5).

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Julai 8 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji hicho.

“Walitoka baa wakiwa wamelewa, alipofika nyumbani kukatokea ugomvi mwanaume akimtuhumu mkewe kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine,” amesema.

Amesema kutokana na ugomvi huo, mwanamke huyo alikimbilia kwa jirani na kumwacha mwanaume na watoto.

“Huku nyuma mwanaume aliamua kulipiza kisasi kwa mtoto wa mwanamke huyo kwa kumnyonga. Tumemkamata, tukikamilisha uchunguzi tutamfikisha katika vyombo vya sheria,” amedai.

Kamanda Theopista amesema wameanisha visababishi vya ukatili wa kijinsia ni pamoja na ulevi wa pombe, hali inayosababisha watu kuchomana visu na hata kuuana.

“Waache vitu ambavyo tunawakataza maana vinasababisha kwenda jela maisha na kuwaacha watoto wao wakiteseka kwa kukosa matunzo,” amesema.

Mmoja wa ndugu wa familia hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema maziko ya mtoto huyo yamefanyika leo katika Kijiji cha Mheme.

“Sikuweza kwenda (kwenye maziko) kwa sababu siwezi kutembea, lakini nimepata taarifa kuwa shemeji aligombana na dada yangu, lakini katika ugomvi huo dada alifanikiwa kukimbia na aliporudi asubuhi ndio akakuta mwanae amenyongwa,” amesema.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF), inaonyesha Dodoma ni miongoni mwa mikoa mitatu nchini inayoongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo, mauaji na ubakaji.

Takwimu hizo zilizotolewa Novemba 2023 zinaonyesha mikoa mingine inayoongoza kwa ukatili Mara na Kagera.

Related Articles

Back to top button
Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker!